• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
service photo

YESU NI MCHUNGAJI MWEMA.

Yohana 10:14-15

Bwana wetu Yesu Kristo alitufundisha habari za upendo wake kwetu akitumia mfano wa Mchungaji mwema anayetoa uhai wake kuokoa kondoo wa malisho yake. Anaeleza jinsi alivyowaongoiza kondoo kwa upole na kondoo wake wanavyomfuata kwa vile wanamjua na wanamsikia sauti yake.

Ndiyo maana Bwana Yesu anajifananisha na mchungaji mwema kwa kuwa anawajjali wanaomuamini, kiasi cha kutoa uhai wake kwa ajili yao (Yh 10:3,15b).

Ninapotafakali neno hili nakumbuka jinsi ambavyo nilipokuwa mdogo, wakati naishi na babu a bibi tulikuwa tunachunga ng’ombe na mbuzi na kondoo za babu Shaidi, baba Ghuheni , baba Paulo na baba Marko.

Kwa kawaida aliajiriwa mchungaji alikuwa anaitwa Nondo. Alikuwa mwenyeji wa Burundi, na alikuwa siku za Jumapili anapewa “Off”na sisi watoto tulikuwa wawili wawili kwa zamu kuchunga. Zoezi hili tulilifurahia sana kwani lilitupa fursa ya kucheza na tulipata kuunda urafiki na kuelewana na wale wanyama vizuri sana. Tuliweza hata kuwapanda wanyama wale kama farasi na walikuwa wapole sana kwetu.

Walitujua kiasi kwamba ukitangulia mbele wanakufuata nyuma. Kwa vile tulikuwa wawili , mmoja hutangulia mbele na mmoja huja nyuma.Kuna wale wanyama watiifu hufuata nyuma bila shida , lakini kuna wale , hasa mbuzi, walio wakorofi huchepuka na kuingia kwenye mashamba ya watu kwa hiyo Yule mchungaji aliyenyuma huwadhibiti kwa kutumia fimbo.

Somo hili linatufundisha kuwa Bwana wetu anatuonyesha kuwa kila mmoja wetu ni mchungaji katika level mbali mbali katika maisha yetu. Sisi hatuhitajiwi kutoa maisha yetu kwa ajili ya kondoo wetu, lakiini kila mmoja wetu anao kondoo ambao wako chini yake. Kama wewe ni baba au mama nyumbani , wale walioko nyumbani kwako , watoto uliopewa na Mungu , ndio Kondoo wako .

Mwishowa safari yetu hapa duniani tutatakiwa kutoa hesabu yao mbele za Bwana. Kama wewe unao madaraka kazini kwako na unawatu chini yako, nao pia ndio kondoo wako. Unawateteaje katika kazi zao, hata unawaletaje kwa Yesu na kuhakikisha wako salama. Watoto Mungu alikupa pamoja kuwa ni wa nyumba moja, wanahitaji malezi tofauti ili waweze kufikia vipaji vyao.

Kuna watoto wengine ni watiifu bila ubishi katika malezi kuna watoto wengine mpaka mzazi afoke kidogo watatii, lakini wengine ni mpaka kwa fimbo ndio wataenda. Mzazi anawapenda watoto wotebila ubaguzi ingawaje wakati mwingine wengine wanaweza kufikiri mzazi anapenda watoto wengine kuliko wengine. Mtoto aliye mtiifu bila kushurutishwa mara nyingi mzazi anamtuma yeye kwa haraka kuliko wengine kwa vile ni mwepesi kutii.

Wazazi wanawajibu wa kuelewa hulka ya watoto wao na tofauti zao ili waweze kuwatendea haki waweze kufikia hatua yao kama Mungu alivyowapangia. Tusipokuwa makini katika hili inakuwa majuto uzeeni, ukitazama nyuma na kuona ulokosea katika malezi ya watoto Mungu alikupa kama kondoo.

Mungu atupe busara zake katika maisha tupate kujua njia ya kufuata ambayo haituletei majuto. Tumuombe Roho Mtakatafu, Mwalimu wetu mkuu atumulikie njia iliyo sahihi ili nyuma yetu tuache watoto wanaomjua na kumuogopa Mungu ili ukoo wetu uendelee kushikamana na Mungu muumba wetu na Baraka zake ziendlee kuonekana kwetu kizazi hata kizazi. Somo hili limetolewa na Nangela Elangwa Mcharo siku ya rando ya Enikunda Shaidi.

Bofya Hapa kupata picha na video za tukio- https://drive.google.com/drive/folders/1SPGyO6BRbAFAcTBTSk34gX_PZT0eEZQr?usp=drive_link