WASIFU WA BABA YETU MPENDWA DR. CLEOPAS SILA MSUYA
Taarifa binafsi:
⢠Baba yetu mpendwa Dr. Cleopas Msuya alizaliwa Moshi Kilimanjaro Machi 12, 1942 akiwa ni mtoto wa tatu na wa mwisho wa Bwana na Bibi Sila Msuya.
⢠Alipokea sakramenti za ubatizo na Kipaimara katika kanisa la Rau, lililokuwa katika usharika wa Moshi Kati.
⢠Alipata sakramenti ya ndoa Desemba 19, 1965 katika usharika wa Same.
⢠Alibarikiwa kupata watoto wanne, wawili wa kike na wawili wa kiume Neli, Sila, Linda (Aliyetwaliwa Juni 1, 2015) na Simon. Aidha aliweza kujiendeleza kupitia kozi fupi na warsha katika nchi mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Elimu
⢠Alisoma shule ya msingi Kiwalaa na baadaye shule ya kati (middle school) Kidia na baadaye kuhamishiwa Marangu.
⢠Alifaulu na kuchaguliwa kwenda shule ya Sekondari Ilboru aliposoma kidato cha kwanza hadi cha nne.
Safari yake katika tasnia ya afya ilianza Mwaka 1960 alipochaguliwa kwenda kusomea Udaktari Usaidizi katika chuo cha Afya Bumbuli ambapo alihitimu mwaka 1962, akatunukiwa Diploma na kupata leseni ya utabibu.
Mwaka 1969 hadi 1973 alikwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Wittenberg, kilichopo Springfield jimbo la Ohio Marekani alipofuzu na kutunukiwa Shahada ya kwanza ya Sayansi katika fani ya Bio Chemisty.
Mwaka 1977 hadi 1979 alikwenda kusoma katika chuo kikuu cha North Carolina kilichopo Chapel Hill, Jimbo la North Carolina Marekani na kutunukiwa shahada ya Uzamili ya Afya ya jamii katika udhibiti wa magonjwa ya milipuko na Elimu ya Afya. Alipokuwa chuoni alifanikiwa kuandika muongozo wa elimu ya afya kwa jamii, ambao umeendelea kutumika kwa marejeo katika chuo hicho kwa miaka mingi. Mwaka 1980 aliteuliwa kuwa mkufunzi katika chuo hicho.
Aidha aliweza kujiendeleza kupitia kozi fupi na warsha katika nchi mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kazi
Alianza kazi katika hospitali ya Bumbuli ambapo alikutana na mama Eninka ambaye naye alipangiwa kufanya kazi hapo baada ya kumaliza masomo yake ya uuguzi huko Kiomboi Singida. Baadaye alihamishiwa katika hopitali ya Nkoaranga iliyo chini ya kanisa la KKKT iliyopo Makumira, Arusha.
Kati ya mwaka 1974 â 1977 Alipata nafasi ya kuwa Mwakilishi wa Taifa wa kampuni ya madawa ya Kimarekani ya ER Squibb and Sons.
Mwaka 1979 na 1984 Aliajiriwa na Wizara ya Afya, kwanza kama Makamu Mkuu wa chuo cha Madakatari na Mkuu wa Idara ya Afya ya Jamii na baadaye akateuliwa kuwa Mkuu wa Vyuo vya Afya vilivyokuwa katika hospitali ya KCMC.
Mwaka 1984 hadi 1990 alipata fursa ya kufanya kazi AMREF katika vituo mbalimbali Tanzania na Kenya akiwa kama mshauri wa masuala ya afya na usimamizi wa program mbalimbali ikiwemo HESAWA. Katika kipindi hiki aliweza kuandaa mtaala wa Taifa kwa ajili ya mafunzo ya maofisa wa afya katika ngazi ya vijiji na miongozo mbalimbali kwa ajili ya usimamizi wa afya katika ngazi hiyo. Mtaala huo ulikuwa ni moja ya matokeo ya program hiyo ya HESAWA kwa ajili ya Wizara ya Afya.
Kati ya mwaka 1990 na 1995 alipata nafasi ya kuajiriwa katika Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na kuwa Regional Health Delegate for Southern Africa (Msimamzi wa Masuala ya Afya wa chama cha msalaba mwekundu Kusini mwa Afrika). Katika nafasi hiyo alikuwa mshauri wa masuala ya Afya wa nchi 10 zilizo kusini mwa Afrika ikiwemo Angola, Botswana, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Namibia, Afrika kusini Swaziland, Zambia na Zimbabwe. Katika kipindi hicho, pamoja na kuchangia katika kuunda idara za Usimamizi wa Afya ya Jamii katika nchi hizo aliongoza timu ya wataalamu iliyofanya tathimini ya mauwaji ya kimbari ya Rwanda na ndiye aliyeandaa andiko la usimamizi wa wimbi la wakimbizi hao na kuandaa michoro kwa ajili ya kambi za wakimbizi hao.
Mwaka 1995 na 1998 aliomba kusogea karibu na nyumbani ili ajiandae kustaafu hivyo akahamia Nairobi na kusimamia nchi za Afrika Mashariki. Katika kipindi hicho, kwa nafasi hiyo alikuwa mkuu wa kikosi cha uokoaji wa ajali mbaya ya boti ya MV Bukoba. Pia alisimamia timu ya Madaktari chini ya Red Cross katika uokoaji wa shambulio la kigaidi la Ubalozi wa Marekani Jijini Nairobi. Kwa kazi hizi alitunukiwa tuzo maalum za uokoaji ambazo familia itaendelea kuzienzi kama alama ya ushujaa na kujitoa kwa ajili ya wengine.
Kati ya mwaka 1967 na 1998 aliweza kuandika machapisho yapatayo 17 aidha aliweza kutafsiri vitabu kadhaa vya afya. Aidha aliweza kuandaa miongozo kadhaa ya kimataifa yaliyolenga katika kujadili masuala muhimu ya kuzuia magonjwa ya milipuko, kupambana na njaa na ukame katika nchi zilizo Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Miongoni mwa kazi ngumu alizowahi kusimulia zilihusu utoaji wa huduma za kiafya katika maeneo yaliyokuwa na vita wakati huo ikiwemo Msumbiji, Liberia, Somalia nk
Mahusiano
Kwa majiarani, Baba - Cleopas (wakiitamka Kiliopa) alikuwa ni mwanakijiji mwenzao aliyependa sana kujichanganya na jamii na kuthamini kila mmoja, wakubwa na wadogo. Alipenda kufundisha vijana na kuwapa ushauri. Atakumbukwa kwa Upendo, kujitoa katika kusaidia wanajamii katika changamoto zao za kiafya. Alijitoa hata kwa kadri ya uwezo wake kifedha pale wahitaji walipojitokeza. Amekuwa ni msahauri na msuluhishi katika familia. Jambo moja alilosisitiza sana ni kutosahau watu waliomsaidia katika maisha yake. Aliwakumbuka na kila mara alituhadithia yale mema aliyotendewa wakati alipokuwa kijana mdogo. Na kubwa Zaidi alituusia kutopenda kujikweza.
Yapo mambo ambayo hakuyapenda. Hakupenda watu wavivu, walevi wa kupindukia, wenye majivuno na walipenda kujikweza. Alisisitiza sana kuwa na kiasi katika kila jambo na kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kutimiza malengo binafsi na malengo ya kitaifa. Alisisitiza sana umuhimu wa elimu katika ukombozi na aliamini katika umuhimu wa kusomesha mtoto wa kike.
Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana familia ilidhani somo katika Timotheo wa 2: 4;7 lisemalo Nimevipiga Vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza Imani nimeilinda, unaweza kutoa taswira halisi ya maisha ya baba yetu mpendwa.
Ugonjwa
Dr Cleopas Msuya alikuwa akisumbliwa na magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu tangu mwaka 1991. Magonjwa haya yalipelekea kupata maradhi mengine yanayoambatana na magonjwa haya. Hii ilipelekea afya yake kudorora hasa ilipofika miaka ya 2015. Pamoja na matibabu mbalimbali aliyopataiwa ndani nan je ya nchi, afya yake iliendelea kuzorota hadi mauti yalipomkuta.
Shukrani
Familia inapenda kuwashukuru sana Madaktari wa Hospitali za KCMC, Mawenzi, Hindu Mandal, Jafarry nk ambao wamekuwa nasi bega kwa bega wakati wa kumuuguza baba.
Tutakuwa wachoyo wa fadhila kama hatutawashukuru Madaktari ndani ya familia yetu akiwemo mama mdogo Esther Temu pamoja na mumewe, Mjomba wetu Estomihi Mduma, kaka yetu David Msuya, Lucy Senyagwa pamoja na daktari mwanafunzi Dorry Mduma ambao walitushauri na kumpa baba uangalizi wa karibu.
Tuchukue fursa hii pia Wachungaji na viongozi wa dini waliokuwa wanamtembelea na kumlea kiroho ikiwa ni pamoja na kumpa chakula cha bwana.
Tunawashukuru majirani wote ambao kwa miaka yote walikuwa wanamtembelea na kumjulia hali ikiwa ni pamoja na kumuombea.
Tunasema asante kwa Wanafamilia ambao walitukimbilia kipindi chote ambacho baba yetu amekuwa akiumwa. Tulishuhudia upendo wa ajabu kutoka kwao katika kipindi hicho.
Kwa namma ya pekee tunamshukuru ndugu yetu wa karibu, dada na mdogo wetu Anna Ludani Tarimo (Mama Gilo). Yeye amekuwa ni sehemu ya familia yetu. Kwake tunasema asante sana kwa kumtunza baba.
Mwisho lakini si kwa umuhimu tunapenda kumshukuru sana mama yetu mzazi kwa moyo wa upendo aliouonyesha wakati wote wa kumtunza baba wakati wa uzima na katika hali ya ugonjwa wake. Ni wajibu wake lakini tumeona ni vizuri kusema kwani hata baba alikuwa anatuambia kwamba umuhimu wa mama katika maisha yake.
Mwisho kama watoto wake, tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa maisha ya baba yetu. Alisimama kama baba wakati wote na kutuhimiza kufanya vizuri katika hatua zote za maisha yetu ikiwemo kujitafutia ujuzi na elimu kila wakati. Alitimiza wajibu wake kama Baba. Alitufundisha kwa vitendo na ilipobidi kupata karipio kali basi tulipata. Matendo yake kwa ndugu jamaa na marafiki ilikuwa ni elimu tosha kwetu na tunaamini kuwa mafanikio makubwa na madogo ndani ya maisha yetu ni kwa sababu ya wazazi wetu.
Sisi tulimpenda lakini Mungu amempenda Zaidi. Yeye ndiye aliyetoa na yeye amemtwaa hatuna Zaidi ya kusema â¦.jina lake lihimidiwe.
Baba ameacha Mke, watoto watatu na wajukuu 10.
2Wakorintho 13;11
Hatimaye, ndugu, kwaherini; mtimilike, mfarijike, nieni mamoja, mkae katika Amani; na Mungu wa upendo na Amani atakuwa pamoja nanyi.