SHUKRANI YA UKOO WA SHAIDI VUDEE – 26/9/2021
Tunamshukuru Mungu aliyetupa kibali kumtolea sadaka ya shukrani ya ukoo wa Shaidi. Hili linatokana na patano letu la ukoo kuwa tutamtolea BWANA shukrani zertu kila baada ya miaka miwili. Sadaka hiyo tunaitolea madhabahuni mwa Bwana,Chome au Vudee. Mwaka huu tulipatana kuwa sadaka ya kila mmoja wetu itatolewa kwa siri haitaandikwa kwenye mitandao ya kijamii wala kusomwa katika vikao. Tulipatana kuwa watakaokusanya ndio watakaojua fulani kamtolea BWANA kiasi gani na hawa ndio wazee wetu wa kanisa au watumishi wa Mungu. Katika somo linalofuata tafadhali soma kwa makini maana ya kutoa sadaka kwa siri. Maandalizi yalitanguliwa na vikao mbalimbali vya ukoo na somo la kumtolea BWANA sadaka inayompendeza. Vikao viliongozwa na Mwenyekiti Yofikah Shaidi. Katika vikao hivyo tulikubaliana na kupatana kumwomba Mungu atubariki na kutupa uzao wa Watoto wa kiume na kike wacha Mungu wenye hekima,maarifa na ujuzi. Tulisimama na Neno Kutoka 31:3 “Nami nimemjaza Roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa na ujuzi,na mambo ya kazi ya kila aina.”katika vikao hivyo tulikubaliana na kupatana kuwa wimbo wetu wa shukrani uwe Namba 196 katika kitabu cha nyimbo cha Tumwabudu Mungu wetu unaosema .”Upendo wa Mungu wetu ndio jua latu……”Neno la shukrani lilitoka Zaburi 50:23 “Atoaye dhabibu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.” Wana ukoo wa Shaidi walisafiri kutoka Dar es Salaam na sehemu zingine mbalimbali hadi Vudee ili kumtolea BWANA dhabihu za shukrani na kumtukuza. Tunamwomba Mungu kwa neema yake kuu atengeneze mienendo yetu na atuonyeshe wokovu wake. E-Mungu uturehemu, sawasawa na fadhila zake. Kiasi cha wingi wa rehema zako,uyafute makosa yetu. Siku ya Jumamosi tarehe 25/9/2021 wana ukoo kwa pamoja walifanya maombi na sala kwa ajili ya kujiandaa mioyo yao kumtolea Mungu sadaka ya shukrani. Waliimba wimbo wa chaguo lao No 196 na kusoma maneno ya Mungu waliyoyachagua; Kutoka 31:3 na Zaburi 50:23. Mchungaji Rosani Mmbwambo aliongoza ibada hiyo iliyofanyika nyumbani. Katika ibada ya Jumapili, tarehe 26/9/2021 wana ukoo walisimama mbele ya madhabahu ya BWANA na kutoa shukrani zao. Pamoja na shukrani ya patano kila mwanaukoo alitoa sadaka yake akijua kwamba si vyema kwenda madhabahuni mwa BWANA mikono mitupu. Neno la maombi pamoja na neno la shukrani lisomwa na Mchungaji Rosani Mbwambo wa Usharika wa Vudee. Mchungaji alitafakari maneno hayo ya Mung una baadaye alifanya maombi kwa ajili ya ukoo wa Shaidi na watu wote. Ilikuwa ibada njema iliyojaa utukufu wa Mungu. Tunamshukuru Mungu kwa kuwa pamoja nasi.