NGUVU YA NENO LA USHUHUDA
Utangulizi
Mtu anatoa ushuhuda au taarifa au tangazo la jambo aliloshuhudia au aliloshuhudiwa na mtu mwingine, aliloliona au kulisikia au alilotendewa. Swali kubwa la kujiuliza ni kuwa unashuhudia nini?
1 Yohana 1:1-3 “lile lililokuwepo tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima. Na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona tena twashuhudia na kuwahubiri ninyi ule uzima uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu. Hilo tuliloliona na kusikia twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi; na ushirika wetu ni pamoja na Baba na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo”. Bwana wetu Yesu Kristo alishuhudiwa na Mungu kupitia Neno lake, akashuhudiwa na malaika, manabii, mitume na watumishi wa Mungu. 1 Yohana 5:9(b),11 “Tukiupokea ushuhuda wa mwanadamu, ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi, kwa maana ushuhuda wa Mungu ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe. Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe”. Wakati Yesu Kristo alipobatizwa sauti ilitoka Mbinguni ikisema; Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Wakati mwingine ni ule alipokwenda kusali mlimani akiwa na Petro, Yakobo na Yohana. Sauti ikatoka katika lile wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye, msikieni yeye (Mathayo 17:5). Yesu Kristo alimshuhudia Mungu alipowashuhudia watu wa mataifa kuhusu ufalme wa Mungu au ufalme wa mbinguni. Mathayo 4:17 “Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia”. Yesu alienda hadi Galilaya akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni na kuamini Injili (Marko 1:14-15). Baada ya utangulizi huu sasa tutafakari nguvu iliyopo katika kushuhudia.
01 Neno la ushuhuda lina nguvu ya wokovu au lina nguvu ya kuokoa.
Neno la Mungu linataka tumshuhudie Yesu Kristo bila aibu yoyote ile watu waokoke. Warumi 1:16 "Kwa mana siionei haya Injili; kwa sababu ni uwezo wa Mungu uuletoa uwokovu kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza na kwa Myunani pia”. Mfalme Daudi katika Zaburi 119:46 anasema “Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, wala sitaona aibu”. Bwana wetu Yesu Kristo katika Marko 8:38 anasema “Maana kila mtu atakayenionea haya mimi na maneno yangu, katika kizazi hiki cha unzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.” Twendeni tukawaambie watu habari njema ya Injili ya Yesu Kristo, wala tusinyamaze ili watu waokoke. Mathayo 28:19-20 “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi, na tazama mimi nipo pamoja nanyi siku zote hata ukamilifu wa dahari.” Tuwe mashahidi na mashuhuda wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa uwezo wa Roho Mtakatifu Injili yake Kristo, ienee pote. Kwa ushuhuda wetu watu waokoke. Swali la kujiuliza ni Je, matendo yetu yana ushuhuda gani? Mathayo 5:16 “Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.” Wafilipi 4:9 “Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea na kuyasikia na kuyaona kwangu yatendeni hayo, na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.” Tuwashuhudie watu kuwa uzima wa milele unapatikana kwa Yesu Kristo na kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yao wote wanaomwamini.
0.2 Neno la shuhuda lina nguvu ya kumshinda shetani
Kulikuwa na vita mbinguni, Mikaeli na Malaika zake wakipigana na yule joka (aitwaye ibilisi na shetani) yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao (Ufunuo 12:7-11). Ibilisi/ Shetani pamoja na malaika zake walitupwa hata nchi nao wanaendeleza vita yao kwa watu wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu Kristo. Hatutakiwi kuwa na uwoga wowote juu ya vita hii kwa sababu tutashinda. Warumi 8:37 “Lakini katika mambo haya yote tunashinda na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.” Ulimwenguni kuna dhiki nyingi lakini Bwana wetu Yesu Kristo anasema tujipe moyo kwa kuwa yeye ameushinda Ulimwengu. Swali la kujiuliza hapa ni hili, Je, tuna Neno gani la ushuhuda lenye nguvu ya kumshinda shetani? Neno letu la ushuhuda nalitokane na mambo mengi makuu Mungu anayotutendea na kazi za Bwana wetu Yesu Kristo hapa duniani. Tutoe ushuhuda wa mambo hayo ili tumwabishe shetani na malaika zake. Yohana 10:25 “Yesu akawajibu Naliwaambia lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia.” Kazi za Bwana Yesu ambazo alizifanya na anaendelea kuzifanya ni nyingi mno Yohana 5:17 “Akawajibu, Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi.” Kazi zinazomshuhudia Bwana Yesu Kristo ni nyingi sana lakini hapa nitaeleza chache tu; aliwaponywa wagonjwa, akawapa vipofu kuona, viziwi kusikia wenye ukoma wenye kifafa, vilema, viwete na wasiojiweza aliwaweka huru. Miujiza yote hii ni matendo makuu ya Bwana wetu Yesu Kristo yanayoshuhudia kuwa ana nguvu kuliko adui yake shetani. Baada ya Yesu Kristo kuondoka humu duniani kazi hizi na nguvu hizi za kumshinda shetani amewaachia wafuasi wake wale wanaomwamini. Yohana 14:12 “Amin, amin, nawaambieni, yeye aniaminiye mimi kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba”. Kazi hizi zinafanyika hata leo hii zikishuhudia ukuu wa Mungu na neema zake kwetu. Shetani naye anaendelea kuzipiga kazi hizi vita au kuzipinga hivyo ili tuweze kumshinda tunatakiwa tuvae silaha zote za Mungu. Waefeso 6:11-12 “Vaeni silaha zote za Mungu mpate kuweza kuzipinga hila za shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote kusimama.” Silaha tunazotakiwa kuvaa ni dirii ya haki, Injili ya amani,ngao ya imani, chepeo ya wokovu na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu . Kwa kuwa tumeshajua mambo yote haya tunatakiwa tuyashuhudie ili kumshinda shetani. Watu wamjue Mungu wa pekee na wa kweli na Yesu Kristo Mungu aliyemtuma kwetu. Shuhuda zetu ziwatie moyo watu waliokata tamaa chini ya ufalme wa giza, wapate kuokoka na hatimaye uzima wa milele. Shuhuda zetu zote zimpe Mungu utukufu kwa kuwa utukufu ni wake
Peke yake, hata milele na milele. Amina