• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 28 Aug, 2023
  • Admin

NGUVU YA MAOMBI

UTANGULIZI

Maombi ni mawasiliano baina ya binadamu na Mungu au ni njia ambayo tunaweza kuwasiliana na Mungu. Maombi yanaongeza uhusiano wa mtu na Mungu. Maombi ni lazima yafanyike katika jina moja tu lipitalo majina mengine yote Jina lenye nguvu, uweza na mamlaka, Jina la Yesu Kristo (Yohana 14:13-14) Maombi yetu yatakuwa na nguvu ya Mungu iwapo yatafanyika kulingana na mapenzi ya Mungu. Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atasikia (Yohana 5:14) mapenzi yake yanapatikana katika Neno lake Takatifu; “Mapenzi yako yatimizwe hapa Duniani kama yanavyotimizwa huko Mbinguni (Mt6:10).” Maombi yetu yawe sawa sawa na ahadi za Mungu kwetu. Mungu anatualika na kutukaribisha ili tumwombe Mathayo 7:7-8,11 “Ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtaona, bisheni nanyi mtafunguliwa. Kwa maana kila aombaye hupokea, naye atafutaye huona, naye abishaye atafunguliwa “Basi ikiwa ninyi mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, Je, Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao? Katika somo letu hili tutatafakari juu ya Nguvu ya Maombi.


0.1       1.0 Maombi ya ujazo wa Roho Mtakatifu yana nguvu kubwa sana.


Warumi 8:26-28 “Kadhalika Roho naye hutasaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa”. Maombi ya roho mtakatifu yanatupa nguvu ya kunena Neno la Mungu kwa ujasiri mkubwa. Matendo ya Mitume 4:31 “Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neon la Mungu kwa ujasiri. Mpe nafasi Roho Mtakatifu akuongoze katika kuomba kwako. Huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa tukiomba kitu sawasawa na Mapenzi yake atasikia.


2.0 Maombi yanatupa nguvu ya kutoingia majaribuni.

Mathayo 26:41 “Kesheni mwombe msije mkaingia majaribuni; roho i radhi lakini mwili ni dhaifu”. Hili ni agizo la Bwana wetu Yesu Kristo na ni wito wake kwetu. Tunashinda majaribu ya mwovu shetani kwa maombi yenye nguvu na uwezo wa Roho Mtakatifu. Kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia tunapojaribiwa. Yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote bila kufanya dhambi. Paulo na Sila walipojaribiwa na kuwekwa gerezani walikua wakimuomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na mara milango ikafunguka, vifungo vyote vikalegezwa. Tumwombe Mungu siku zote asitutie majaribuni lakini atuokoe na yule mwovu shetani / ibilisi, utakaposhinda majaribu ibilisi atakuacha na tazama watakuja malaika wakutumikie (Mathayo 4:11). Kisha ibilisi akamwacha (Yesu); na tazama wakaja malaika wakamtumikia.


3.0 Maombi ya toba yana nguvu kubwa na uwezo wakubadilisha maamuzi ya Mungu juu yako, familia yako,ukoo wako na hata nchi yako.

Katika Bibilia iko mifano mingi ya wana wa Israeli walipofanya toba ya kweli Mungu aliwasamehe na kughairi adhabu yake juu yao. Hasira ya BWANA iliwaka juu ya Waisraeli walipomnung’unikia Mungu. Baadae watu wakamwendea Musa wakasema tumefanya dhambi, utuombee kwa BWANA atuondolee nyoka hawa. Wale wote waliokubali kumtazama yule nyoka wa shaba wakaishi. Mfano mwingine ni wa mfalme Hezekia Mungu alipomtaka atengeneze mambo ya nyumba yake maana atakufa. Isaya 38:2 Basi Hezekia akamwomba BWANA kwa machozi mengi. Bwana Mungu akayasikia maombi yake na kuyaona machozi yake akamwongezea kiasi cha miaka kumi na mitano ya kuishi. Zaidi ya hayo Mungu akamwambia (Isaya 38:6) Nami nitakuokoa wewe na mji huu na mkono wa mfalme Ashuru, nami nitaulinda mji huu BWANA akalitimiza jambo hilo alilolisema. Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na kutusafisha na udhalimu wote.

4.0 Maombi ya rehema yana nguvu yakiambatana na toba ya kweli.

Katika maombi yako mwombe Mungu akurehemu kwa kuwa maombi ya rehema yana nguvu ya kuharibu kila nguvu ya uovu inayokuzunguka. Kupitia maombi ya toba na rehema tumepewa mamlaka juu ya mataifa na juu ya falme ili kung’oa na kubomoa na kuharibu na kuangamiza, ili kujenga na kupanda kwa jina na damu ya Yesu Kristo. Kipofu Bartimayo aliomba rehema na macho yake yakafunguliwa Marko 10:47-52, “Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi Yesu unirehemu. “Yesu akamwambia, Enenda zako Imani yako imekuponya, mara akapata kuona, akamfuata njiani. Luka 17:12-14 “na alipoingia kwenye kijiji kimoja alikutana na watu 10 wenye ukoma wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema Ee Yesu Bwana mkubwa uturehemu. Alipowaona aliwaambia Enendeni mkajionyeshe kwa Makuhani ikawa walipokuwa wakienda walitakasika. “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza, kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba Yeye yupo na huwapa thawabu wale wamfuatao.

4.1 Maombi ya rehema na toba yakifanyika kwa Imani yana nguvu ya kuvunja maagano ya kichawi na kiganga yaliyofanywa na wewe mwenyewe, familia yako, au ukoo wako.

Kumbuka kutumia jina na damu ya Yesu katika maombi yako. Luka10:19 “Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga Ng’e na Nyoka na nguvu zote za yule adui Shetani. Maombi ya aina hii yana nguvu ya kuvunja vifungo vya utasa.        Mwanzo 25:21 “Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake maana alikuwa tasa naye BWANA akamwitikia na Rebeka mkewe akachukua mimba”. Rebeka akajifungua mapacha, Esau na Yakobo (1 Samweli 1:5).   

5.0 Maombi ya kufunga yana nguvu na uwezo wa kukusaidia katika mambo magumu ambayo hayawezekani isipokuwa kwa kufunga, hapo ndipo utapata mafunuo (Revelation) kutoka kwa Mungu.

Wanafunzi wa Bwana Yesu waliposhindwa kumtoa pepo akawaambia haiwezekani ila kwa sala na kufunga (Mathayo 17:21). Katika Yeremia 33:3 Mungu anasema “niite nami nitakuitikia nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu, (Mafunuo) usiyoyajua”. Esta na watu wake walifunga na kumwomba Mungu akamwonyesha Esta mambo makubwa, magumu asiyoyajua. Adui yao na mshitaki wao aitwae Hamani Mfalme aliagiza atundikwe juu ya mti “basi wakamtundika Hamani juu ya mti waliomwekea tayari Mordekai. Ili tukue kiroho tunatakiwa kufunga na kuomba wakati tumeweka mbali uovu wote na hila yote na unafki na husuda na masingizio yote (1 Petro 2:1)

6.0 Maombi ya kunena kwa lugha yana nguvu ya kumsadia Mkristo kunena mambo ya siri katika roho yake na Mungu wake.

1 Wakorintho14:2 “Maana yeye anenaye kwa lugha hasemi na watu kwa bali husema na Mungu maana hakuna asikiaye lakini ananena mambo ya siri katika roho yake; yeye ananae kwa lugha hujijenga nafsi yake. Maombi ya kunena kwa lugha yana nguvu pekee yenye uwezo wa kuleta majibu ya mambo ya sirini na yaliyojificha Mathayo 6:6 “Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi”. Wakati wa Pentekoste Mitume wakiwa ndani ya nyumba walipokea Roho Mtakatifu wakiaanza kunena kwa lugha.

Kwa maana hiyo kunena kwa lugha kuna uwezo wa Roho Mtakatifu (Matendo ya Mitume 2:1-44). Matokeo yake watu wapatao elfu tatu walilipokea neno wakabatizwa. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.

7.0 Maomb yana nguvu ya kukupatia hekima, akili na mali.

Mfalme Suleimani alipewa nafasi na Mungu kuomba kitu chochote atakacho, naye akaomba hekima (1 Wafalme 3:12) Mungu akampa moyo wa hekima na wa akili. Katika 2 Mambo ya Nyakati 1:12 “Basi hekima na maarifa umepewa, nami nitakupa mali, na utajiri na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala badala yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo”. Ukiomba sawasawa na mapenzi ya Mungu kuna nguvu ya baraka hata kwa yale ambayo hukuyaomba, Waefeso 3:20-21 “Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawezayo kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu, naam atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina.

8.0 Maombi ya kuweka watu au vitu wakfu yana nguvu katika utendaji wa kazi ya BWANA.

Maombi haya hufanyika kumtenga mtu au kitu kwa kusudi takatifu la BWANA. Matendo ya Mitume 13:2-3” Basi hawa walipokuwa wakimfanyia BWANA ibada  na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.” Wakiongozwa na Roho Mtakatifu  wakahubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Wayahudi, Ndipo liwali , Sergio Paulo , mtu mwenye akili nyingi alipoyaona yaliyotendeka akaamini akistajabia mafundisho ya BWANA, Luka 2: 22” Kisha zilipotimia siku za kutakasika kwao , kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye (Yesu) hata Yerusalemu wakamweka kwa bwana katika maandiko utaona kuwa watu walikuwa wanaweka vitu vipya wakfu au watoto wao wa kwanza kwa BWANA. Katika kumbukumbu la Torati 20:5 “Na maakida na waseme na watu na kuwaambia ni mtu gani aliye hapa aliye jenga nyumba mpya wala hajaiweka wakfu? Aende akarudi nyumbani kwake asije akafa mapiganoni isije ikawekwa wakfu na mtu mwingine. Nehemia 12:27 “Basi walipouweka wakfu ukuta wa Yerusalemu wakawaleta Walawi ili waweze kufanya wakfu pamoja na furaha, na kwa shukrani, na kwa kuimba, kwa matoazi, vinanda na vinubi.” Tusipoweka vitu vyetu wakfu shetani anaweza kututangulia na kuviweka wakfu kwake. Tukumbuke kujitenga wenyewe kwa ajili ya kazi ya BWANA kwa kuwa miili yetu ni hekalu la BWANA, ili Mungu aweze kututumia kwa ajili ya kazi yake. Mungu akubariki.

9.0 Maombi ya kusamehe wale waliotukosea yana nguvu ya kukupatia msamaha wa dhambi zako.

Mathayo 6: 14 “kwa maana mkisamehe watu makosa yao na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi.” Kwa sababu hiyo nawaambia kila msimamapo na kusali, sameheni mkiwa na neno juu ya mtu ili na Baba yenu aliye mbinguni naye awasamehe makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehi hata Baba yenu wa mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu (Marko11: 25-26). Basi ukileta sadaka yako madhabahuni na huku ukikumbuka ndugu yako ana neno juu yako , iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako kwanza  upatane na ndugu zako kisha urudi uitoe sadaka yako ( Mathayo 5 : 23 – 24 ).

 

10. Maombi yana nguvu ya kukupatia ushindi na kukuondolea aibu.

Eliya aliposhindana na Makuhani wa Baali aliomba hivi, “Ee BWANA Mungu, wa Ibrahimu, na wa Isaka na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya haya kwa neno lako. Unisikie, Ee BWANA, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, BWANA ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa BWANA ukashuka ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwepo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema BWANA ndiye Mungu, BWANA ndiye Mungu (1Wafalme 18:36-39). Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii. Yakobo 5:17-18 “Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi akaomba kwa bidii mvua isinyeshe na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, Mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikaaza matunda yake” Maobi ya mwenye haki kujibiwa akiomba sawasawa na mapenzi ya Mungu. Maombi ya mtu mnyoofu yana nguvu ya kuleta furaha.

Nihitimishe

Nihitimishe somo hili kwa kusisitiza kuwa maombi yana nguvu kubwa yanapofanywa kwa imani. Tuombe kwa imani na hatupashwi kuwa na mashaka yoyote, kwa kuwa ahadi ya Mungu ipo wazi mbele yetu kuwa, ombeni nanyi mtapata. Yohana Mtakatifu 16:23-24 “Amini, amini nawaambia mkimwomba Baba neno lolote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu, ombeni nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.” Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule na BWANA atamwinua hata ikiwa amefanya dhambi atasamehewa (Yakobo 5:15). Neno la Mungu linatuhakikishia kuwa tusimamapo na kusali tuamini ya kwamba tutayapokea nayo yatakayokuwa yetu. Mungu alibaliki Neno lake.

 

 

  

  

 

 

Share This