SURA YA KWANZA
CHIMBUKO LA SADAKA YA UKOO WA SHAIDI
Na Neli Msuya Lyaruu
Angalao mara moja kwa mwaka ukoo wa Shaidi popote pale walipo hukusanyika ili kukutana na kutoa shukrani kwa Mwenyenzi Mungu. Shughuli hiyo ya shukrani pamoja na mambo mengine huambatana na kufanya maombi, kushiriki ibada kanisani, kutoa mkono wa msaada kwa wahitaji, kupata chakula cha pamoja na kufanya kikao cha ukoo.
Utaratibu huu umekuwa ukifanyika kwa zaidi ya karne moja sasa na inatarajiwa kuwa vizazi vijavyo vitaendelea kuudumisha na kuuenzi ikiwa ni njia ya kuendeleza umoja, kuleta upatanishi na kujenga jeshi imara ambalo lilikuwa ndiyo ndoto ya mababu zetu.
Utoaji wa sadaka ya kumshukuru Mungu ni mpango ulioasisiwa na Mzee Mkaza ambaye alikuwa ni kizazi cha nne kutoka kwa muanzilishi wa ukoo aliyetambulika kwa jina la Mntuwedi yaani mtu mwema.
Kwa mujibu wa maandiko yaliyotokana na simulizi za mdomo, ninanukuu….. “Mzee Mkaza alitambua kuwa anahitaji nguvu za Mungu katika maisha hayo ya vita na ghasia naye akaweka nadhiri yake kwa Mungu kuwa Mungu akimjalia ukoo wake kupata watoto wa kiume wenye akili na afya nzuri atamtolea dume kubwa la ng’ombe la KIRURUMO kama shukrani yake kwa Mungu”, anaeleza Vincent Shaidi katika kitabu cha Ukoo wa Shaidi. Kwa tafsiri, dume la Kirurumo ni ng’ombe dume kubwa kuliko yote katika zizi.
Katika kitabu hicho, Vincent Shaidi ambaye ni kizazi cha sita anasimulia hali ya kivita iliyotawala kati ya koo na makabila tofauti. Itoshe kusema kuwa aliyekuwa familia na ukoo wenye vijana jasiri, nguvu na wenye maarifa ndiye aliyeweza kuwa na uhakika wa maisha, chakula, ardhi na mifugo.
Simulizi hizi zinazopatikana katika kitabu cha ukoo wa Shaidi, zinatupa mfano halisi wa umuhimu wa kuwa na vijana hodari, werevu, jasiri na wakakamavu. Tunaelezwa kuwa siku moja iliyoanza vizuri, kukiwa na upepo mwanana, kabaridi kwa mbali huku vigelegele vya kina mama vikisikika, palitokea jambo la kustusha. Furaha iliyokuwepo ikageuka majonzi na eneo la sherehe likageuka uwanja wa vita. Siku hiyo isiyo na jina Mzee Mkaza na wenziwe wa ukoo na majirani zake waliondoka nyumbani kupisha wake zao ili waweze kufanya sherehe ya kueka (unyago). Shughuli hii ya akina mama waweza kuilinganisha na Kitchen party hivi sasa kwani endapo sherehe kama hiyo inafanyika nyumbani, basi kina baba hulazimika kuwapisha wake zao ili waweze kuwa huru na kuzungumza na mabinti zao.
Tunasoma katika kitabu hicho kuwa wazee walipoondoka, huku nyuma, kundi la maadui walivamia kinamama na bahati mbaya Mwali wa Mkaza, ambaye ni mke wa Nziamwe yaani bibi Nakusighe alitekwa na kupelekwa huko Mhezi ili kuuzwa. Waweza kufikiri taharuki ambayo iliwakuta wazee hawa siku hiyo!! Nziamwe ambaye alikuwa jasiri alipata habari kuwa mkewe amepelekwa Mweteni hivyo akamwaga baba yake na akaondoka kwenda kumkomboa mkewe. Aliporejea tu Mzee Mkaza, akiwa na Gobole lake alilonunua kutoka kwa Waarabu wafanyabiashara utumwa, akaitisha vijana wake hodari na wakajipanga kwenda kupigana na kulipiza kisasi. Kilichofuata ilikuwa ni fedheha kwa watu wa Mweteni ambao walilazimishwa kuswaga ng’ombe wao waliotekwa hadi Vudee tena huku wakilazimishwa kuimba. Baada ya kufika nyumbani jeshi zima likiwa salama ilikuwa ni furaha kwa wote na hasa bibi Nakusighe. Hapa moja kwa moja tunajifunza kuwa ombi la Mkaza lilijibiwa kwani yeye na vijana wake walishinda vita hii.
Mengi yameelezwa kuhusu ukakamavu na ujasiri wa wazee amabo ni chimbuko la ukoo wa Shaidi. Pia tumesikia kuhusu hekima la upendo wa mabibi zetu. Lakini ni mara chache husikia simulizi za uzuri aliokuwa nao Bibi Nakusighe. Tunaelezwa kuwa alikuwa ni mrembo mwenye rangi ya maji ya kunde, mrefu wa kadri, macho ya upole, aliyekuwa na nywele ndefu na laini za asili.
Wana ukoo wa rika langu watakumbuka wakati tunakua wazazi wetu waliitwa na baba zao kwenda Vudee au Chome kwa ajili ya kutoa sadaka, kufanya mikutano, sherehe ama hata misiba ambapo pamoja na mambo mengine, walihudhuria ibada na kukaa pamoja kula, kunywa na kujadiliana. Hafla hizi hazikurasimishwa sana lakini zilitosheleza lengo kwa wakati ule. Mababu zetu kwa nyakati tofauti walitafuta dume la Kiroromo na wakawaita vijana wao na kuwasimulia kuhusu ahadi ya waasisi wa ukoo kwa Mungu. Aidha kitendo cha Mzee Mkaza kudhamiria na kutimiza nia yake ya kutoa sadaka, imekuwa chanzo cha utaratibu wa kuuweka ukoo pamoja ili kutoa shukrani kwa Mungu na kuweza kujenga ukoo ulio imara, wenye upendo, mshikamano na shukrani.
Miaka mingi sasa imepita na ukoo wa Shaidi umeimarika, umepanuka na kutawanyika katika pembe mbalimbali za nchi na Dunia. Mnamo mwaka 2006, wazee wa ukoo wa kizazi hiki waliamua kurasimisha utaratibu wa ahadi ya shukrani ya babu Mkaza. Katika nyakati hizi za maendeleo ya kasi, ilionekana kuwa ni wakati muafaka wa kumshukuru Mungu kwa Baraka nyingi anazoendelea kututendea lakini kuomba msaada wake katika kuimarisha vijana kiakili na kiroho, ili kuweza kuwa na msimamo wa kimisha katika Ulimwengu wa leo. Ili kufanikisha ibada hii, vijana kwa wazee wa kizazi chote cha Shaidi walihamasishwa kukutana na kutoa michango ya sadaka ili kuweza kwenda Vudee au Chome, palipo chimbuko la Ukoo na kufanya ibada ya kutoa sadaka ya shukrani.
Mwaka huu 2017 kama ilivyo ada, Tarehe 13 hadi 15 Oktoba, shughuli hii ilifanyika huko Vudee. Jumla ya wanaukoo 63 walihudhuria. Shughuli ilianza kwa vikao vya maandalizi vilivyoweka mipango sawa na kugawa majukumu kwa kamati ndogo ndogo tano ambazo zilitakiwa kutoa mrejesho kwa Mwenyekiti, Mzee wa ukoo ambaye kwa sasa ni Mzee Wilfred Abraham Shaidi.
Ili kuweka kumbukumbu vizuri kwa ajili ya vizazi vijavyo, ukoo ulishauri safari hii pawepo kijarida ambacho kitakusanya kumbukumbu chache muhimu za shughuli hii. Lengo ni kuanzisha utamaduni wa kuweka kumbukumbu sahihi za suala hili katika maandishi kwa manufaa ya kizazi kilichopo na cha baadaye. Hii ndiyo ikawa chimbuko la jarida hili lisilo rasmi.
Hivyo kwa heshima na taadhima nawakaribisha ili msome, mfurahi na mtafakari jinsi ya kuendelea kuboresha utaratibu huu.
Bofya Hapa kupata jarida lililoandaliwa - https://drive.google.com/file/d/1MURdjQQZ8BrHwYop_UH6l4sPVnq6VXV_/view?usp=sharing