SHUKRANI YA PEKEE YA EDNA M.SHAIDI NA VINCENT M.SHAIDI KWA
KUFIKISHA UMRI WA MIAKA 70
Edna na Vincent ni watoto mapacha waliozaliwa na Mwl.Marko Shaidi na mkewe Merina Karani. Mapacha hawa walizaliwa tarehe 27/28 mwezi wa January 1952 katika kijiji cha Vudee, Wilaya ya Same, mkoa wa Kilimanjaro. Mtoto wa kwanza kuzaliwa ni Edna, walibatizwa tarehe 11 April 1952 katika kanisa la KKKT – Usharika wa Vudee. Mapacha hawa katika ubatizo walidhaminiwa na Ratera Paulo Mtae na Christina Shangweli. Mapacha hawa wangezaliwa kabla ya Ukristo kufika Vudee mwaka 1909 kulingana na mila na desturi za Kipare za wakati huo wangeuawa kwa kuwekwa kando pembeni ya jiwe la Kisesa lililoko Kwanamburi. Mtoto hunyonyeshwa hadi ameshiba na kupata usingizi. Akiwa usingizini huachwa peke yake hapo na wazazi na watu wengine huondoka mara atakapoamka usingizini akijaribu kujigeuza tu huanguka chini ya jiwe hilo na kufariki. Jiwe hilo lilikuwa maalumu kwa ajili ya kuuwa watoto mapacha ambao walionekana kuwa ni laana katika jamii ya wakati huo.
Wapare wa wakati huo waliona mapacha kuwa ni laana kwa kuwa haikuwa kawaida kwa mama mjamzito kuzaa watoto wawili kwa mara moja.
Tunamshukuru Mungu aliyetuumba na kutuleta duniani kwa nyakati na majira ya habari njema za Bwana wetu Yesu Kristo. Tutashukuru na kwimba milele, wote wajue jinsi wewe ulivyo mkuu. Mapacha hawa wenye umri wa miaka sabini waliamua kutoa shukrani ya pekee kwa Mungu wakati wa Pasaka tarehe 17 April 2022 katika usharika wa Vudee. Ndugu na marafiki walipanda nao kwenda Vudee ili wapate kushirikiana nao kwa kuwa ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo ili furaha yetu itimizwe. Jumamosi tarehe 16/04/2022 asubuhi ndugu na marafiki waliokuwa Vudee walienda hadi nyumbani kwa mama Christina Shangweli mdhamini wa ubatizo wa mapacha hawa kwa ajili ya ibada ya shukrani. Katika ibada hiyo tuliimba na kusikia neno la Mungu lililotolewa na mtumishi Jennifer Mareale na tulitoa sadaka kwa BWANA.
Pamoja na sadaka tulimpatia mama Christina Shangweli zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyakula, kitenge na blanketi. Mama Christina Shangweli alipokea zawadi hizo kwa furaha iliyojaa machozi na shkrani kwa Mungu. Siku hiyo hiyo ya jumamosi jioni wakati tunasubiri kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo tukiwa Vudee Holiday Home tulifanya ibada ya kujiweka wakfu kwa Bwana kwa ajili ya ibada ya shukrani kesho yake jumapili ya pasaka. Katika ibada hii tulimsifu Mungu kwa kumwimbia nyimbo za sifa pamoja na za kuabudu.Tuliimba wimbo uliokuwa umechaguliwa maalumu kwa ajili ya sadaka ya shukrani wimbo namba 262 katika kitabu cha Tumwabudu Mungu wetu. Wimbo unaosema “Tumshukuru Mungu kwa kunywa na kwa moyo, atendaye makuu popote hata kwetu. Tangu kuzaliwa mpaka leo hivi na siku zijazo hutuhurumia. Baba mwenye nguvu atupe siku zote mioyoni mwetu furaha na Amani .Baraka yake kuu itusaidie, tushinde huzuni na shida zozote. Tumsifu Mwenyezi aliye Baba yetu. Tumsifu na Mwana aliyetuokoa. Tumsifu na Roho atutakasaye. Tumsifuni Mungu sasa na milele. Tulitafakari neno la Mungu lililochaguliwa maalumu kwa siku hiyo ya shukrani ya pekee, neno kutoka Zaburi 92:13-15. Neno la Mungu linasema hivi “waliopandwa katika nyumba ya BWANA watasitawi katika nyua za Mungu wetu. Watazaa matunda hadi wakati wa uzee. Watajaa utomvu watakuwa na ubichi. Watangaze ya kuwa BWANA ni mwenye adili, mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu”.
Hakika Mungu alituhurumia akatuokoa na laana ya kifo kile cha kwenye jiwe la Kisea, tu kashinda huzuni na shida zile akatupa Amani na furaha. Tumsifu Mungu sasa na milele.
Katika kutafakari neno hilo la Mungu tuliongozwa na mtumishi Anna kutoka Hedaru. Baada ya neno tulitoa sadaka ili kukamilisha ibada hiyo. Ibada iliongozwa na Mch. Rosani Mbwambo wa usharika wa Vudee.
Jumapili tarehe 17/04/2022
Jumapili ya Pasaka, siku ya kukumbuka kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo ambaye ameshinda kifo; Kristo amefufuka Haleluya, amefufuka kweli kweli Haleluya, tulisimama mbele ya madhabahu ya BWANA kumtolea dhabihu zetu za shukrani .Washarika wa Vusee walitusindikiza kwa kuimba wimbo na. 262 na Zaburi ya 92:13-15. Ulikuwa wakati wa furaha na shangwe mbele ya madhabahu ya BWANA. Tulimshukuru Mungu kwa ajili ya maisha ya Edna na Vincent kufikisha miaka sabini. Kila mmoja wetu alimshukuru Mungu pia kwa ajili ya maisha yake hata kufikisha umri alionao sasa. Tulimwomba Mungu aushibishe siku uzee wa kila mmoja wetu. Tulimshukuru Mungu kwa mambo mengi mema na makuu ambayo ametutendea katika maisha yetu. Ibada ilifuatiliwa na chakula cha mchana kwa waalikwa wote ikiwapo kwaya ya Tarumbeta ya usharika wa Vudee. Baada ya chakula cha mchana mapacha walikata keki na kupewa zawadi mbalimbali .Ulikuwa wakati wa furaha na shangwe. Pacha wa kiume Vincent alipigiwa vigelegele mara nne na pacha wa kike Edna mara tatu. Wapare walifanya hivyo ili kuwajulisha wana jamii ni mtoto wa kiume au wa kike aliyezaliwa. Wakati huo wa zama hizo wanaume hawakuruhusiwa kukaribia eneo la kujifungulia wamama wakati kuna mama mzazi wa kujifungua. Wao walisikiliza kwa matumaini vigelegele vitakapopigwa. Sherehe hii ilikuwa njema sana kwa kuwa kila tulilolifanya tulilifanya kwa neno na tendo katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, tukimshukuru Mungu Baba kwa kuwa yote yalifanyika kwa ajili ya utukufu wake. Jina la BWANA lihimidiwe. Mungu atubariki sisi sote tunaomtumainia na kumtegemea.
Picha mbalimbali zilizopigwa wakati wa tukio hili zipo kwenye link hapo chini.