• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 22 Aug, 2023
  • Admin

·       Kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu

Neno la Mungu linatutaka  tuombe  kwa  unyenyekevu sawasawa  na  mapenzi ya Mungu. Tuombe kuwa mapenzi yake yatimizwe katika maisha  yetu  hapa duniani kama yanavyotimizwa  huko mbinguni. Mapenzi ya Mungu yanapatikana katika neno lake. Mapenzi ya Mungu ni mengi sana kwa hiyo  katika somo hili tutatafakari  mistari michache ya neno  la Mungu  itakayo tusaidia kufahamu namna  inavyompendeza Mungu  tukiomba sawasawa  na mapenzi yake. Tutajifunza pia mapenzi ya Mungu ni yapi ambayo tunatakiwa  kuzingatia  wakati wa  kuomba. Bwana wetu  Yesu Kristo  alipokuwa akiomba  katika bustani ya Gethsemane  wakati ule moyo wake ukiwa umejaa huzuni nyingi aliomba kuwa mapenzi ya Mungu  ya timizwe . Mathayo 26:39,42 “Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli akaomba  akisema, Baba yangu ikiwa haiwezekani  kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama  nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.Akaenda  tena mara ya pili, akaomba akisema, Baba yangu ikiwa yawezekana  kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, mapenzi yako yatimizwe”. Tunatakiwa tufahamu ya kwamba  Mungu anaweza  kukuacha upitie mateso kwa sababu  ni mapenzi yake  ili mateso hayo  yamzalie  Mungu ushindi na kumpa utukufu.

1.   Petro 3:17 “Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kutenda mabaya.

 Ukishafahamu  kuwa mateso unayopitia  ni mapenzi ya Mungu, maombi yako yawe ni kumuomba  Mungu  kwa neema yake  iliyo kuu akupe nguvu na amani yake uweze kustahamili mateso hayo bila ya kuingia majaribuni  na kumkosea Mungu wako. Bwana Yesu alipoomba maombi hayo malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu (Luka 22:43). Hata wewe uliyepo  kwenye mateso ukiomba sawasawa na mapenzi yake Mungu  atakuonyesha  milango wa kutokea, atamtuma malaika wake akushike mkono na kukutoa  kwenye mateso hayo. Unapoomba sawasawa  na mapenzi ya Mungu  unampa Mungu nafasi ya kutenda yaliyo mapenzi yake katika maisha yako kwa kuwa yeye anajua mahitaji yako yote hata kabla wewe hujamuomba. Mathayo 6:7-8 “Nanyi mkiwa katika kusali msipayuke – payuke kama watu wa mataifa, maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao mengi. Basi msifanane na hao, maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamuomba”Zaburi 40:8 Mwimba zaburi Daudi anasema, “Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;naam, sheria yako imo moyoni mwangu.”

Nabii Yeremia katika Yeremia 15:16 anasema, “Maneno yako yalionekana nami nikayala, na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu, maana nimeitwa kwa jina lako, Ee BWANA, Mungu wa majeshi”.

Ni mapenzi ya Mungu  kuwa tumuamini yeye na kuzaliwa mara ya pili ili tuwe viumbe wapya wanaoitwa kwa jina lake .Yohana 1:12-13 “Bali wote waliompokea. aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa  si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu bali kwa mapenzi ya Mungu”. Hawa ndio wale Bwana Yesu anaosema wakikaa ndani  yake na maneno yake  yakikaa ndani yao, waombe lolote watakalo naye atawatendea au atawapa, nao watakuwa wanafunzi wake. Sisi tuliozaliwa mara ya pili tunatakiwa tutambue kuwa maamuzi  ya kukupa au kutokupa na kwa wakati gani na kwa kiasi gani yako mikononi mwa Mungu. Yakobo 4:13-15 “Haya basi ninyi msemao leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi”. Mtume Petro alipoagana na watu wa Efeso aliwaambia nitarejea  kwenu tena Mungu akinijalia, kwa kuwa alijua kuwa Mungu ndiye muweza na muamuzi wa mambo yote tunayomuomba.Neno la Mungu linatufundisha kuwa tusipoomba sawasawa na mapenzi ya Mungu hatuwezi kupokea tunayoyaomba lakini tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atatusikia. Yakobo 4:3 “Hata mwaomba, wala hampati  kwa sababu mwaomba vibaya ili mvitumie kwa tamaa zenu”. Hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia  ni kuwa adui wa Mungu.

Na hao Mungu aliwaacha, Warumi 1:28 “Na kama walivokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa”. Lakini wale wote wanaoliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo anawapa ujasiri na lolote waombalo walipokea kwake, kwa kuwa wamezishika amri zake na kuyatenda yapendezayo machoni pake.       

1Yohana 5:13-15 “Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mnauzima wa milele, ninyi mnaoliamini jina la Mwana wa Mungu. Na huu ndio ujasiri tulianao kwake, yakuwa tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake,atusikia.Na kama tukijua kwamba atusikia tuombacho chote twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba” Inatubidi tusubiri wakati sahihi wa Mungu kutujibu maombi yetu kwa kuwa Yeye hawahi wala hachelewi ni Mungu mwaminifu anayehukumu kwa haki.Kumbuka siku zote kuwa Mungu huliangalia neno lake na kulitimiza sawasawa na mapenzi yake. Mapenzi ya Mungu yanapatikana katika ahadi zake kwetu. Kwa hiyo ni vyema kuzijua ahadi za Mungu. 

·       Mungu ametuahidi ulinzi wa miili yetu na  roho zetu.

Tusisahahu kuwa katika somo hili tunajifunza juu ya ahadi za Mungu ambazo tunaweza kuzitumia  kuomba sawasawa na mapenzi yake.Mungu analinda miili yetu kwa kutuepusha na hatari, ajali na magonjwa.Mungu analinda watoto wetu pamoja na mali zetu ; mali zile zinazotumika katika kutukuza jina lake yaani kwa utukufu wake. Tukimtumaini BWANA , yeye ni mwaminifu atakayetufanya imara na kutulinda na yule mwovu pamoja na kufanya mlango wa kutokea.1 Korintho 10:13 “ Jaribu halikuwapata ninyi isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu , ila Mungu ni mwaminifu, ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea ili mweze kustahimili”. Basi Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu. Malaika wa BWANA hufanya kituo akiwazungukia wamchao na kuwaokoa na yule mwovu .Tunalindwa na nguvu ya Mungu ambaye pia aweza kukilinda kile tulichokiweka amana kwake hata siku ile ya mwisho .Basi tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu , ni nani aliye juu yetu (Warumi 8:31) . Bwana wetu Yesu Kristo hutulinda na hutuombea ulinzi kwa Mungu.Yohana 17:11,12,15 “ Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini uwalinde hawa ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nami naja kwako Baba Mtakatifu kwa jina lako ulilonipa. Nilipokuwa pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza, wala hapana mmoja wapo wao aliyepotea, ile yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie .Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu , bali uwalinde na yule nwovu. “ Mungu pamoja na kulinda roho zetu anailinda miili yetu kutokana na maadui zetu, hatari na ajali mbalimbali. Isaya 354:15 “ Tazama, yamkini watakusanyana lakini si kwa shauri langu.Watu wowote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako “ Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba(kumb. Torati 28:7) .Yeye atalinda miguu ya watakatifu wake, bali waovu watanyamazishwa gizani, maana kwa nguvu hakuna atakayeshinda , washindanao na BWANA watapondwa kabisa.Yeremia 1:19 “ Nao watapigana nawe lakini hawatakushinda ; maana mimi nipo pamoja nawe aseme BWANA , ili nikuokoe”. Mungu anatuahidi kuwa tukimpenda na kuliinua jina lake tukamwita ataitikia na atakuwa pamoja nasi taabuni, atatuokoa na kutuweka palipo juu.Mabaya hayatakupata wewe, kwa kuwa atakuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote .Mikononi mwako watakuchukua, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe (Zaburi 91:10-15) .Kwa siku nyingi nitamshibisha , nami nitamwonyesha wokovu wangu. Isaya 49:10

“ Hawataona njaa wala hawataona kiu; hari haitawapiga wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemichemi za maji atawaongoza”. Hatutaona njaa wala kiu kamwe kwa kuwa Yesu Kristo Bwana wetu anacho chakula cha uzima Yohana 6:35 “ Yesu akawaambia , mimi ndimi chakula cha uzima , yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe”. Mungu anatuahidi kutulinda na hatari za wanyama na wadudu wakali tukimwamini na kumtegemea yeye. Zaburi 91:13 “ Utawakanyaga simba na nyoka , mwana samba na joka utawaseta kwa miguu”. Hutaogopa hofu ya usiku wala mshale urukao mchana .Luka 10:19 “ Tazama , nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za yule adui , wala hakuna kitu kitakachowadhuru” Amri hii inatupa uwezo na mamlaka ya kumpinga na kumkanyaga shetani pamoja na mapando yake yote.Jambo lolote linalofunga na kuzuia baraka na mafanikio yako unayo mamlaka ya kulikanyaga chini ya miguu yako nalo lisiibuke na kudhuru maisha yako iwe ugonjwa , umaskini, utasa na kila aina ya pando ambalo shetani amelipanda katika maisha yako.Wakati mwingine pando la shetani linakuwa juu ya mali zako kama alivyofanya kwa mtumishi wa Mungu Ayubu .Ayubu alipoteza watoto na mali zake nyingi lakini hakumkufuru BWANA na BWANA akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza Kumbukumbu la Torati 28:4 “ Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wan chi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo , maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo zako”. Ukimcha Mungu kwa moyo wako wote atalinda nyumba yako na mashamba yako. Zaburi 127:1 “ Bwana asipoienga nyumba wajengao wafanya kazi bure. BWANA asipoulinda mji yeye aulindaye akesha bure”. Shamba lako BWANA atalilinda na kulitia maji kila dakika asiye mtu akaliharibu ; usiku na mchana atalilinda (Isaya 27:3). Yoeli 2:23-27 “ Furahini basi , enyi wana Sayuni mkamfurahie BWANA, Mungu wenu kwa kuwa yeye huwapa ninyi mvua ya masika kwa kipimo cha haki, naye huwanyeshea mvua, mvua ya masika na mvua ya vuli, kama kwanza na sakafu za kupepeta zitajaa ngano na mashinikizo yatafurika kwa divai na mafuta.Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu , na tunutu, jeshi langu kubwa nililolituma kati yenu.Nanyi mtakula chakula tele na kushiba , na kulihimidi jina la BWANA , Mungu wenu” Na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA , Mungu wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani . Litabarikiwa kapu lako na chombo chako cha kukandia unga. Utabarikiwa uingiapo na utokapo (Kumb la Torati 28:2,3,5,6).Mungu katika neno lake takatifu ametuahidi utajiri na mafanikio ikiwa tutaenenda katika uchaji wa neno lake ,tukizishika amri , maagizo na mausia yake.Kumbukumbu la Torati 15:4-5. “ Lakini hawatakuwepo masikini kwenu; (kwa kuwa BWANA atawabarikia kweli katika nchi akupayo BWANA , Mungu wako, uimiliki, iwe urithi wako) kwamba utaisikiliza tu kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako , uyatunze maagizo haya yote  nikuagizayo leo kufanya”. Mungu katika Yoshua 1:7-8 alimwahidi mtumishi wake Yoshua mwana wa Nuni kuwa akitenda sawa sawa na sheria ya Mungu atafanikiwa sana kila aendapo maana ndipo atakapofanikisha njia yake, kisha ndipo atakapostawi sana kwa kuwa BWANA , Mungu wake atakuwa pamoja naye kila aendako .Neno la Mungu linasema kuwa heri mtu yule ambaye hakusimama katika njia ya wakosaji bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo .Zaburi 1:3 “ Naye atakuwa kama mti uliopandwa kando kando ya vijito vya maji , uzao wa matunda yake kwa majira yake, wala jani lake halinyauki na kila alitendalo litafanikiwa”. Bwana wetu Yesu Kristo anasema kuwa yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao . 2 Wakorintho 8:9 “ Maana mmejua neema ya Bwana wetu YESU Kristo , jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu , Ingawa alikuwa tajiri ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umasikini wake”. Mungu atatujaza kila kitu tunachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu , ndani ya Kristo Yesu .Tukumbuke kuwa vitu vyote yeye ndiye aliyeviumba na ni mali yake naye humpa mtu atakavyo kwa ajili ya utukufu wake. Bwana wa majeshi anatuahidi  ya kuwa tutakuwa nchi ya kupendeza sana na yenye heri na baraka tele ikiwa tutamtolea zaka kamili.Malaki 3:10-11 “ Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwepo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu  kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye , wala hataharibu mazao ya ardhi yenu, wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wala katika mashamba , asema BWANA wa majeshi” . Mungu anapokubariki hivi shetani anaweza kuleta pando la ugonjwa au maradhi ili usiweze kufurahia baraka hizi za Mungu.Tuangalie ahadi za Mungu kuhusu afya njema , ugonjwa na tiba ili tuweze kumwomba  Mungu sawaswa na mapenzi yake tukimkumbusha ahadi hizo.Na itakuwa utakapozisikiliza amri na sheria za Mungu na kuzishika na kuzitenda , basi BWANA Mungu wako atakurehemu na kukupa afya njema.Kumbukumbu la Torati 7:15 “ Na BWANA atakuondolea ugonjwa wote, wala hatatia juu yako maradhi yoyote mabaya uyajuayo ya Misri, Lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao”. Mungu anasema hatatia juu yako maradhi yoyote aliyowatia Wamisiri, kwa kuwa yeye ndiye BWANA akuponyaye.Mabaya hayatakupata wewe wala tauni iharibuyo haitaikaribia hema yako, kwa kuwa atakuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako. Zaburi 103:3 “ Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote, aukomboa uhai wako na kaburi, akutia taji ya fadhili na rehema”. Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako , asema BWANA, kwa sababu wamekuita , mwenye kutupwa, wakisema ni Sayuni ambao hapana mtu autakaye (Yeremia 30:17). Katika Agano Jipya kuna ahadi nyingi za Bwana wetu Yesu Kristo kuhusu afya njema, uponyaji wa maradhi au magonjwa na uponyaji wa hayo yote kwa kuwa mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu .Mathayo 9:35 “ Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao , na kuihubiri habari njema ya ufalme , na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali , akatoa pepo wengi hakuwaacha pepo kunena kwa sababu walimjua (Marko 1:34) .Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao na misiba na pepo wabaya na vipofu wengi aliwakirimia kuona, viwete wakatembea wenye ukoma wakatakasika , viziwi wakasikia, wafu wakafufuliwa, masikini wakahubiriwa habari njema (Luka 7:21-22) .Bwana Yesu ametutuma kwenda kwenye miji na vijiji kuwaponya wagonjwa waliomo na kuwahubiria juu ya ufalme wa Mungu kuwa umewakaribia .Bwana wetu Yesu Kristo ametuahidi kuwa wale wamwaminio wataweka mikono yao juu ya wagonjwa nao watapata afya (Marko 16;18 ). Mtu wa kwenu amekuwa hawezi ? na awaite wazee wa kanisa, nao wamwombee na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule , na Bwana atamwinua hata ikiwa amefanya dhambi , atasamehewa (Yakobo 5:14-15).  Katika Yohana Mtakatifu 14:12 Bwana wetu Yesu Kristo anasema “ Amini amini nawaambieni, yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi yeye naye atazifanya, naam na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba” Mungu Baba wa Mbinguni atakuwa pamoja na wateule wake nao watakuwa watu wake. Ufuno. 21:4 “ Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwepo tena , wala maombolezo , wala kilio wala maumivu hayatakuwepo tena, kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita “ Tazama atayafanya yote  kuwa mapya. Ili mambo yote yawe mapya tunatakiwa kuomba kwa bidii na juhudi nyingi ; tukidumu katika maombi na sala bila kuchoka wala kukata tamaa.

Share This