Pamoja na unabii wote waliopewa alipokuja masihi au Kristo kwao, Wayahudi walio wake hawakumpokea. Matendo ya Mitume 2:36 “Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulubisha kuwa Bwana na Kristo.” Yesu alitimiza unabii huo na kuuthibitishia ulimwengu kwamba yeye ndiye Masihi aliyeahidiwa. Yeye ndiye atakayewaokoa watu na dhambi zao, Mwana- kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu. Hebu tuangalie kwa namna gani Wayahudi walivyomkataa Bwana Yesu kuwa yeye sio Masihi. Yohana 3:12 “Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni? Yesu ndiye nuru ya uzima inayoangaza gizani wala giza halikuiweza. Nuru hii imekuja ulimwenguni lakini watu wakapenda giza. Yohana 19:21 “Na hii ndiyo hukumu, ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi yakuwa yametendwa katika Mungu.” Wako Wayahudi, mafarisayo, waandishi na wazee ambao hawakumkubali wala kumwamini Yesu kuwa ndiye Masihi aliyetabiriwa katika Agano la Kale. Yohana 4:25-26 “Yule mwanamke akamwambia, najua ya kuwa yuaja Masihi (aitwaye Kristo), naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote. Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye.” Yohana 10:24-26 “Basi Wayahudi walimzunguka, wakamwambia, Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu. Kama wewe ndiwe Kristo, utwambie waziwazi. Yesu akajibu, naliwaambia lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia. Lakini ninyi hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo wangu.” Baba aliyemtuma Bwana Yesu alimshuhudia mara nyingi hata wakati wa kubatizwa kwake lakini hawakutaka kuja kwake kupata uzima badala yake walinung’unika na kutafuta kumuuwa. Yohana 6:41:42 “Basi Wayahudi wakamnung’unikia, kwa sababu alisema, mimi ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni. Wakasema, Je huyu siye Yesu,mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, nimeshuka kutoka Mbinguni.” Kukawa na manung’uniko mengi baadhi ya mafarisayo wakasema, mtu huyo yaani Yesu hakutoka kwa Mungu, kwa sababu haishiki sabato, wengine wakasema ana pepo huyu, tena ana wazimu, mbona mnamsikiliza. Wayahudi wakatafuita kumwua wakatuma watumishi ili wamkamate. Yohana 7:32 “Mafarisayo wakawasikia mkutano wakinung’unika hivi juu yake; basi wakuu wa makuhani na mafarisayo wakatuma watumishi ili wamkamate.”Basi tangu siku ile walifanya shauri la kumwua. Basi wale askari na yule jemedari na wale watumishi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga (Yohana 18:12). Wakamchukua hadi Gorgotha wakamsulubisha huko. Hawakumtambua, hawakumpokea wala kumsadiki au kumwamini kwa sababu macho yao ya rohoni yalifichwa mambo hayo. Yohana 12:39 “Ndiyo sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena; amewapofusha macho, ameifanya mizito mioyo yao, wakafahamu kwa mioyo yao, wakaongoka, nikawaponya.” Hata hivyo wapo Wayahudi na watu wa mataifa mengine waliompokea na kumwamini.” Yohana 12:42-43 “Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini lakini kwa sababu ya mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu.” Wengi walimwamini baadaye kama neno linavyosema katika Yohana 7:39-41 na neno hilo linasema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watapokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa. Basi wengine katika mkutano walipoyasikia maneno hayo, walisema, hakika huyu ndiye nabii Yule. Wengine walisema, huyu ndiye Kristo.” Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, ninyi mkikaa katika neno la langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru (Yohana 8:31-32) Je, sisi wa kizazi hiki tunakubali kumpokea na kumkiri Bwana Yesu Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yetu? Yohana 13:20 “Amin,Amin, nawaambieni, yeye ampokeaye mtu yeyote nimpelekaye, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenipeleka.” Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. tuanze kwa kuangalia maana ya kuitwa watoto wa Mungu. Mungu anatukumbusha tu watoto wake 1 Yohana 3:1 “Tazameni ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.” Bwana wetu Yesu Kristo anasisitiza jambo hili alipoletewa watoto wachanga ili awaguse. Luka 18:15:17 “Wakamletea na watoto wachanga ili awaguse, lakini wanafunzi walipoona waliwakemea. Bali Yesu akawaita waje kwake, akasema, waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa kuwa watu kama hao ufalme wa Mungu ni wao. Amini nawaambia, mtu ye yote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hauingii kamwe.” Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha kuwa tusipoongoka na kuwa kama vitoto hatutaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Tena ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. Na ye yote atakaye mpokea mtoto mmoja kwa jina la Yesu atakuwa amempokea Bwana Yesu (Mathayo 18:1-5). Warumi 8:14-17 “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu Kwa kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea Roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.” Neno la Mungu linasema watoto wa Mungu ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Tito 3:5-7 “si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi, bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu, ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.” Zipo ahadi nyingi za Mungu kwa wale waliaminio jina lake; wale wanaoamini kuwa Yesu ni Kristo Mwana wa Mungu na ndiye Mwokozi wa ulimwengu na kuwa jina lake ni kuu lipitalo majina yote mbinguni na duniani. Ahadi hizo ni nyingi lakini hapa tutaorodhesha chache tu kama ifuatavyo;
Tuhitimishe somo hili kwa kukiri kuwa jina hili ni kuu lipitalo majina yote. Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina, ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.” Kwa sababu ikimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu utaokoka (Warumi 10:9). Tena katika Yohana 5:24 neno linasema, “Amii, Amin nawambia yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele, wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Tumwombe Mungu kupitia jina hili lenye nguvu na mamlaka na tuamini kwamba kwa kupitia jina hili nasi tutauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli. Mungu atubariki tutakaosoma neno hili na kuliamini jina la Yesu. Amina.