Yohana Mtakatifu 20:9 “Kwa maana hawalifahamu bado andiko, ya kwamba imempasa kufufuka”.
Tuanze kutafakari neno hili kwa kuangalia maandiko machahe yanayoonyesha kuwa imempasa Masihi au Kristo kufufuka.Katika Agano la Kale kuna unabii mwingi uliotabiri kufa na kufufuka kwa Masihi au Kristo.Zaburi 16:10 “ Maana hatakuachia kuzimu nafsi yangu, wala hatamtoa mtakatifu wako aone uharibifu” Zaburi 49:15 “ Bali Mungu atanikomboa nafsi yangu, atanitoa mikononi mwa kuzimu, maana atanikaribisha”. Isaya 54:7-8 “Kwa kitambo kidogo nimekuacha ; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya. Kwa ghadhabu ifurikayo nalikuficha uso wangu dakika moja, lakini kwa fadhali za milele nitakurehemu , asema BWANA Mkombozi wako.Isaya 25:8-9 “ Amemeza mauti hata milele; na BWANA na Mungu atafuta machozi katika nyuso zote na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote maana BWANA amenena hayo.Katika siku hiyo watasema, tazama huyu ndiye Mungu wetu, ndiye tuliyemngoja atusaidie; huyu ndiye BWANA tuliyemngoja na tushangilie na kuufurahia wokovu wake” .Pamoja na unabii wote huo Yesu Kristo mwenyewe kabla ya kifo chake alielezea wazi wazi kuwa atafufuka.Yesu alitabiri juu ya kufa na kufufuka kwake. “Marko 8:31-32 “Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi ; na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandisho, na kuuawa , na baada ya siku tatu kufufuka..Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. “ Yesu alitwaa tena wale Thenashara, akaanza kuwaambia habari za mambo yatakayompata . Marko 9:31-32 “Kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamjua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka. Lakini hawakufahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza . “Marko 10:32-34 akisema, Angalieni tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi , nao watamhukumu afe, watamtia mikononi mwa Mataifa , nao watamdhihaki, na kumtemea mate , na kumpiga mijeledi na kumuua; na baada ya siku tatu atafufuka” .Pamoja na maandiko yote yanayoelezea kwamba imempasa Bwana wetu Yesu Kristo kufa na kufufuka wako wanafunzi wake pamoja na watu wengine ambao hawakulifahamu bado andiko hili kuwa atafufuka siku ya tatu.Luka 18:34 “Walakini (wale Thenashara) hawakuelewa maneno hayo hata kidogo , na jambo hili lilikuwa limefichwa kwao, wala hawakufahamu yaliyonenwa”. Lakini hawakufahamu neno hilo nao wakaogopa kumwuliza”. Yesu aliwaambia wanafunzi wake katika Luka 9:44-45 “Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa mikononi mwa watu.Lakini hawakulifahamu neno lile. Likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile.” Mioyo yao ilikuwa mizito kuamini yote waliyoyasema manabii na yale yote aliyoyasema Bwana wetu Yesu Kristo kuwa imempasa kupata mateso, kufa na kufufuka siku ya tatu.Tuangalie maandiko machache yanayoonyesha kuwa Yesu Kristo Bwana wetu amefufuka katika wafu.Malaika wa Bwana walishuhudia kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Yohana 20:11-12 “Lakini Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi , nje yake analia .Basi akilia hivi , aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi .Akaona Malaika wawili , wenye mavazi meupe, wameketi; mmoja kichwani, na mmoja miguuni hapo ulipolazwa mwili wake Yesu” Mathayo 28:5-6 “ Malaika akajibu akawaambia wale wanawake , msiogope ninyi kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa .Hayupo hapa kwani amefufuka kama alivyosema.Njoni , mpatazame mahali alipolazwa .Bwana wetu Yesu Kristo baada ya kufufuka alijidhihirisha kwa wanafunzi wake na watu mbalimbali. Kwa mara ya kwanza alijidhihirisha kwa Mariamu Magdalene .Marko 16:9 “ Naye alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma , alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba” Yesu akamwambia usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa baba. Mariamu Magdalene akaenda , akawapasha wanafunzi habari ya kwamba amemwona Bwana na yote Bwana aliyomwambia (Yohana 20:14 -18). Yesu aliendelea kujidhihirisha kwa wanafunzi wake na watu wengine kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na mazungumzo , kumega mkate, mafundisho na kula pamoja nao. Yesu aliwatokea njiani watu wawili waliokuwa wakienda Emau na kuzungumza nao.Luka 24:15 “Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao” Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani , alitwaa mkate , akaubariki, akaumega akawapa.Yakafumbuliwa macho yao. Wakaambiana, je mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko? Wakaondoka saa ile ile , wakarejea Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na moja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao wakisema, Bwana amefufuka, kweli kweli naye amemtokea Simoni. Nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani na jinsi alivyotambulikana nao katika kumega mkate (Luka 24:30-35). Kuwaondoa mashaka wanafunzi wake Yesu aliwadhihirishia wanafunzi wake kuwa yeye alikuwa na mwili halisi sio roho kama wengine walivyofikiria ..Hata alikula chakula pamoja nao na kuwaonyesha mwili wake .Luka 24:36-43 “ Na walipokuwa katika kusema habari hiyo , yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu.Wakashituka wakaogopa sana wakidhani ya kwamba wanaona roho.Akawaambia mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu.Tazameni mikono yangu na miguu yangu ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo.Na baada ya kusema aliwaonyesha mikono yake na miguu yake. Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha , huku wakistaajabu , aliwaambia mna chakula chochote hapa? Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa.Akakitwaa akala mbele yao” . Tunatakiwa na sisi wakristo wa leo tujiulize swali hili, je tuna mashaka yoyote kuhusu kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo .Kama hatuna mashaka natukiri kuwa Yesu Kristo Bwana wetu amefufuka kweli kweli Haleluya.Tutafakari kwa kifupi tutapata nini kukiri na kuamini hivyo.Neno la Mungu katika 1 Wakorintho 15:17,20 , linasema “ Na kama Kristo hakufufuka, imani yetu ni bure, mngalimo katika dhambi zenu.Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea.Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala” Yesu Kristo anao uwezo wa kufufua alimfufua Lazaro hata sisi atatufufua. 1 Wakorintho 6:14 “ Naye Mungu alimfufua Bwana , na tena atatufufua sisi kwa uweza wake” Tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu , na kutuhudhurisha pamoja nanyi (2 Wakorintho 4;14) .Lakini ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu Katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yetu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu(Warumi 8:11) .Kufufuka kwa Yesu Kristo Bwana wetu kumetuhakikishia kuwa na sisi tutakapokufa tutafufuka.Kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo kumetuhakikishia sisi kuishi maisha ya ushindi ndani ya Kristo kwani Roho Mtakatifu wake anaishi ndani yetu naye atatupa kushinda dhidi ya nguvu za giza .Mwana wa Mungu alidhihirishwa ili azivunje kazi za shetani. Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo .Kwa kufufuka kwake tumepewa uwezo na mamlaka ya kuhubiri Injili na kufanya mambo makuu .Marko 16:14-18 “ Baadaye akaonekana na wale kumi na moja walipokuwa wakila akawakemea kwa kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakusadiki wale waliomwona alipofufuka katika wafu. Akawaambia, enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.Aaminiye na kubatizwa ataokoka ; asiyeamini atahukumiwa.Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo, watasema kwa lugha mpya , watashika nyoka, hata wakinywa kitu cha kufisha hakitawadhuru kabisa, wataweka mikono yao juu ya wagonjwa nao watapata afya.” Kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo kunatuhakikishia uzima wa milele. Yohana 6:39-40 “ Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja , bali nimfufue siku ya mwisho.Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.” Tumwombe Mungu atupe macho ya rohoni ili tuweze kumtazama Bwana wetu Yesu Kristo na kuamini kuwa Mungu alimfufua katika wafu na kuwa atatufufua na sisi tunaomwamini na kutupa uzima wa milele. Tumeokolewa kwa neema.