TUKAOKOLEWA NA WATU WASIO HAKI, WABAYA, MAANA SI WOTE WALIO NA IMANI. (Wathesalonike 3:2)
Tunamshukuru Mungu kwa matendo yake makuu na ya ajabu aliyotutendea wakati wote wa maisha yetu hata leo hii. Watu wasio haki, wabaya waliinuka na kusema maneno mabaya kuhusu wewe mtu wa Mungu wakisukumwa na chuki, hasira na dharau. Lengo lao likiwa ni kukuabisha, kukubeza na kukuchafua ili kukuvunja moyo katika kumtumikia Mungu. Katika somo hili ninataka tutafakari neno la Mungu kuhusu mambo hayo.
Zab 1:1 “Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki, wala hakusimama katika njia ya wakosaji; wala hakuketi barazani pa wenye mizaha”. Huyu atamzalia BWANA matunda mema na mengi na kila alitendalo litafanikiwa. Kwa kuwa BWANA anaijua njia ya wenye haki, bali ya wasio haki itapotea.
ROHO YA CHUKI
Yeye asemaye, kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa. Yeye ampendaye ndugu yake akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo. Bali yeye amchukuiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho (1 Yohana 2:9-11). Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji; nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndan yake. Mtu akisema nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo, kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake (1 Yohana 4: 20-21). Kumbuka kuwa chuki zao hazibadilishi kusudi la Mungu kwenye maisha yako. Mungu akikubariki hakuna mtu anayeweza kuondoa baraka zako. Mungu atakuinua viwango vya juu kulingana na kusudi Lake. Watashuhudia ukuu wa Mungu wako nao watamtafuta ikiwa utakuwa kielezo chema kwao. Acha wakuchafue Mungu wako anakazana kukuinua. Usiache kuwaombea wanao kuchukia ili waache uovu wao. Luka 6:27 “Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi. Wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi,waombeeni wale ambao wawaonea ninyi”.Tunamshukuru Mungu kwa kutuokoa na watu wasio haki tena wabaya wenye roho za chuki juu yetu.
HASIRA YA MWANADAMU
Chuki ya wasio haki huzaa hasira. Neno la Mungu linatutaka tusiwe wepesi wa kukasirika kwa maana hasira ya mwanaadamu haitendi haki ya Mungu. Hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu. Zab 37:8 “Ukomeshe hasira, uache ghadhabu, usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya”. Mhubiri 7:9 “usifanye haraka kukasirika rohoni mwako,maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu” Mtu asiye na wepesi wa hasira ni mwema kuliko shujaa (Mithali 16:32). Bwana wetu Yesu Kristo anafundisha juu ya hasira katika mahubiri yake ya mlimani.
Mathayo 5:22 “Lakini nawaambieni yeyote anaemkasirikia ndugu yake atakuwa chini ya hukumu”.
Tumwombe Mungu atusaidie kwa njia ya Roho Mtakatifu wake uchungu wote na ghadhabu na hasira jua lisichwe na uchungu bado haujatutoka. Hasira na kelele na matukano yaondoke kwetu pamoja na kila namna ya ubaya.
Tuwe na huruma, tusameheane kama na Mungu katika Kristo Yesu alivyotusamehe sisi, kwa kuwa BWANA si mwepesi wa hasira.
Zab. 145:8 "BWANA ana fadhili, ni mwingi wa huruma si mwepesi wa kukasirika, ni mwingi wa rehema”
KUDHARAULIWA NA KUBEZWA
Watu wasio haki wanadharau ndugu zao na kuwabeza kwa sababu wanajiona kuwa wao ni bora zaidi ya wengine, wanajiona kuwa wana elimu zaidi, fedha zaidi na wanajiona kuwa ni maarufu zaidi.
Lengo la watu wa aina hii ni kukuaibisha, kukutia unyonge na udhaifu. Neno la Mungu linatutia nguvu katika 1 Wakorintho 15:43 "Hupandwa katika aibu, hufufuliwa katika fahari, hupandwa katika udhaifu, hufufuliwa katika nguvu". Neno la Mungu linatutaka tusidharauliane kwa kuwa sisi sote ni watoto wa Mungu, warithi wa mapenzi yake. Wala usijidharau wewe mwenyewe hata kama watu wote watachagua kukudharau na kukupuuza. Ukijipa heshima mwenyewe na ukujiamini inatosha kabisa. Kumbuka Mungu huwaheshimu wale wanaomtumikia kwa uaminifu. Usijidharau kwa kuwa Mungu atakutia nguvu kama alivyofanya kwa Gideoni. Waamuzi 6:12 “Malaika wa BWANA akamtokea, akamwambia BWANA yu pamoja nawe, Ee shujaa”. Hawataweza kukuaibisha kwa sababu utapainulia patakatifu mikono yako na kumwita BWANA akusaidie usiaibike milele wala kutahayarika. Zaburi 25:2 “ Ee Mungu wangu, nimekutumaini wewe, nisiaibike, adui zangu wasifurahi kwa kunishinda”.
Mithali 11:12 "Asiye na akili humdharau mwenziwe, bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza." Hata Bwana wetu Yesu Kristo katika njia ya msalaba alidharauliwa, alidhihakiwa, alidhalilishwa, alitukanwa na kubezwa.
Luka 23:11 "Basi Herode akamfanya duni, pamoja na askari zake, akamdhihaki." Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakapiga magoti mbele yake wakamdhihaki, wakisema, salamu, mfalme wa Wayahudi kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi jiokoe mwenyewe. Luka 23:39 "Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi". Lakini yeye alinyamaza hakujibu neno. Mwishowe aliwasamehe na kuwaombea msamaha kwa Mungu. Luka 23: 34 "Yesu akasema, Baba uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo". Na sisi pia tunaamriwa tuwasamehe na kuwaombea adui zetu.
Kwa njia hii ya msalaba sisi tukaokolewa na watu wasio haki, wabaya, maana si wote walio na imani. Ukimwamini na kumfuata Bwana wetu Yesu Kristo hakika Mungu atakuokoa katika mitego yote ya wasio haki, atakukingia mabaya yote. Atakufunika kwa mabawa yake, utapata usalama kwake, mkono wake utakulinda na kukukinga. BWANA awe kimbilio lako na ngome yako, na umtumainie yeye tu. Mabaya hayatakupata wewe kwa kuwa atakuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Kwa Jina lake lenye nguvu, uweza na mamlaka tutawaangusha na kuwashinda. Tutawashinda kwa damu ya Mwanakondoo, na kwa Neno la ushuhuda. Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zetu, Amen