• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 13 Oct, 2023
  • Admin

YEREMIA 29:11-14 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala sio ya mabaya , kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho .Nanyi mtaniita , mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza .Nanyi mtanitafuta na kuniona mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote .Nami nitaonekana kwenu asema BWANA nami nitawarudisha watu wenu waliofungwa, nami nitawakusanya ninyi, nikiwatoa katika mataifa yote na katika mahali pote nilikowafukuza , asema BWANA, nami nitawaleta tena, hata mahali ambapo kutoka hapo naliwafanya mchukuliwe mateka.

Utangulizi:Kuna mafundisho mengi katika unabii wa Yeremia ambayo tutaanza kuyaangalia kabla ya kutafakari mistari hii ya Yeremia 29:11-14 .Unabii wa Yeremia ulihusu mambo mengi lakini jambo tutakaloangalia hapa ni kuhusu dhambi .Mungu anachukizwa na kukasirishwa na dhambi zetu naye hutuonya kwa njia ya Neno lake na mafundisho ya manabii, mitume, wachungaji na watumishi wake. Ikiwa tutazitambua dhambi zetu , na tukizijutia na tukitubu yeye ni mwingi wa rehema .Hutusamehe uovu wetu na dhambi zetu zote hivyo hatuna budi kumfuata na kumtumainia yeye katika maisha yetu yote ya hapa duniani

Mungu anasema tukitenda dhambi atatutupa mbali na macho yake, ataikomesha sauti ya kicheko na sauti ya furaha , sauti ya Bwana arusi na sauti ya bibi harusi, kwa maana nchi itakuwa ukiwa watu waovu wanaokataa kusikiliza maneno ya Mungu , wanaokwenda kwa ushupavu wa mioyo yao na kufuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu atawaharibu.Yeremia 17:5 “Bwana asema hivi amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu , amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake na moyoni mwake amemwacha BWANA. Ataleta juu yake aibu ya milele, na fedheha ya daima ambayo haitasahauliwa .Dhambi ni aibu kwa watu wote.Mwenye kiburi atajikwaa na kuanguka wala hapana atakayemwinua .Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti

Mungu anatuonya katika Neno lake kuwa tuachane na dhambi tumsikilize yeye anavyotufundisha .Mungu anatufundisha kama watoto wake kwa njia za ndoto na maono ,kwa zaburi na nyimbo na tenzi za rohoni .Roho Mtakatifu ni mwalimu mwema ambaye hutufundisha na kutuonyesha mapenzi ya Mungu .Yeremia 7:23 “ Lakini naliwaamuru neno hili, nikisema , sikilizeni sauti yangu nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru mpate kufanikiwa”. BWANA asema hivi tazama naweka mbele yenu njia ya uzima na njia ya mauti .Ole wake aijengaye nyumba yake kwa uovu na nyumba yake kwa udhalimu.Atumiaye utumishi wa mwenzake bila ujira, wala hampi mshahara wake.Ole wao wachungaji wanaoharibu kondoo za malisho yangu na kuwatawanya, angalieni nitawapatiliza uovu wa matendo yenu, asema BWANA. Kwa wale wanaomtumain BWANA , BWANA anasema, nami nitaweka juu yao wachungaji watakaowalisha ; wala hawataona hofu tena, wala kufadhaika , wala hatapotea hata mmoja wao , asema BWANA .Mathayo 24:24-25 “ Kwa maana watatokea wakristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu , wapate kuwapoteza kama yamkini, hata walio wateule.Tazama nimekwisha kuwaonya mbele” .Jiepusheni na jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi. 2Timotheo 2:14-16. “ Uwakumbushe mambo hayo ukiwaonya machoni pa Mungu , wasiwe na mashindano ya maneno ambayo hayana faida , bali huwaharibu wasikiao. Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtende kazi asiye nasababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno lakweli”.Vijana nao wanaonywa wawe na kiasi katika mambo yote. asikudharau mtu awaye yote. 1 Petro 1:11 “Wakatafuta ni wakati upi na tunatakiwa kuonya na kukaripia kwa mamlaka yote, wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo. BWANA amewatuma watumishi wake kwetu ili watufundishe kuziacha njia zetu mbaya tuache uovu wa matendo yetu na kumrudia BWANA 2Timotheo 3:16 “Kila andiko lenye pumzi ya Mungu , lafaa kwa mafundisho na kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza na kwa kuwaadabisha katika haki”Tukitengeneza njia zetu na matendo yetu yakawa ya haki na tukasikiliza sauti ya BWANA, Mungu wetu naye BWANA atayaghairi mabaya aliyonena juu yetu wala hatatudhuru kwa dhara lolote badala yake atatubariki.Tukizijutia dhambi zetu na kutubu na tukiomba rehema ya Mungu , Mungu ataturehemu kwa kuwa yeye ni Mungu mwenye rehema nyingi.Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA , ni mawazo ya amani wala si ya mabaya kuwapa niyi tumaini siku zenu za mwisho” Mungu anasema mwenye kuasi akimrudia hatamtazama kwa hasira maana Mungu ni mwenye rehema.Ukiungama uovu wako wote ya kwamba umemwasi BWANA, Mungu wako na njia zako zimekuwa mbaya, wala hukutii sauti ya BWANA ndipo BWANA atakupa wachungaji wanaompendeza moyo wake, watakaokulisha kwa maarifa na fahamu. Yeremia 4:22 “Kwa maana watu wangu ni wapumbavu, hawanijui, ni watoto waliopungukiwa na akili wala hawana ufahamu, ni wenye akili katika kutenda mabaya bali katika kutenda mema hawana maarifa”. Hawatetei madai ya yatima ili wapate kufanikiwa, wala hawaamui haki ya mhitaji. Yeremia 10:23-24 “Ee BWANA ,najua ya kuwanjia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake, kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu Ee BWANA, unirudi kwa haki, si kwa hasira yako, usije ukaniangamiza’’.

Tukitubu dhambi zetu Mungu ataturehemu na kutusamehe nasi tutauona wema wa BWANA na roho zetu zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji, wala hatutahuzunika tena, tutafurahi na kucheza , vijana na wazee pamoja .Ee Bwana, tunakiri uovu wetu na ubaya wa baba zetu , maana tumekutenda dhambi.Usituchukie bali utusamehe kwa ajili ya jina lako , jina lipitalo majina yote , jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliyekuja ulimwenguni kuzivu nja kazi za Ibilisi. Marko 2:10 “ Lakini mpate kujua ya kwamba Mwanawa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi’’.Kwa maana damu yake ya agano imemwagika kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Neno hili lawezekanaje kwetu? Neno hili ni kwa ajili ya wale waaminio na kumtumainia BWANA, naye atawasafisha na uovu wao wote, ambao kwa huo wamemtenda BWANA dhambi , naye atawasamehe maovu yao yote na kuyasahau.Nao watakuwa watu wake naye atakuwa Mungu wao atawapa moyo mmoja na njia moja wapate kumcha siku zote; kwa mema yao na watoto wao baada ya hao. Bwana atafanya agano la milele pamoja nao, kwamba hatageuka wala kuwaacha ili awatendee mema.Hawa watakula mema ya nchi na baadaye uzima ule wa milele.Hawa ni wale waliofua mavazi yao kwa damu ya Mwna kondoo .Hawa BWANA atawapa tumaini siku zao za mwisho.Zaburi 125;1-2 “ Wamtumainio BWANA ni kama mlima Sayuni, ambao hautatikisika, wakaa milele.Kamamilima inavyouzunguka Yerusalemu, ndivyo BWANA anavyozunguka watu wake, tangu sasa na hata milele. Wamtumainio BWANA ni wale wanaomtegemea na kumwamini Mungu.Tunatumaini kwa njia ya imani kwa kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo nani bayana ya mambo yasiyoonekana. Kwa maana nyingine kuwa na imani ni uwezo wa kutumaini kwamba jambo fulani litakuwa kwa uhakika kabisa bila mashaka yoyote.BWANA mwenye nguvu ndio ngome yao na kimbilio lao siku ya taabu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, ambaye BWANA ni tumaini lake hataona hofu.Yeremia 17:17 “Usiwe sababu ya hofu kuu kwangu mimi, wewe ndiwe uliyekimbilio langu siku ya uovu’’. Kwa sababu hiyo sitaogopa wala sitafadhaika kwa maana utaniokoa wakati wa shidayangu.Nitakuita nawe utaniitikia na kunionyesha mambo makubwa na magumu nisiyoyajua.Kwa kuwa wewe ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili, hakuna neno gumu lolote usiloliweza, wewe ni BWANA wa majeshi, mkombozi hodari unayetetea kwa bidii watu wanaokutumaini wewe.Waefeso 1:12-13.

“Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu.Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli ,habari njema za wokovu wenu, tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Rohoyule wa ahadi aliye Mtakatifu”.

Ni neno la kuaminiwa tena la stahili kukubalika kabisa, kwa maana twajitaabisha na kujitahidi kwa kusudi hili, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote hasa wa waaminio.Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu.Liko tumaini la uzima wa milele katika siku zetu za mwisho, asema BWANA, Mungu wa majeshi.

Share This