WATEULE WA MUNGU NA MZAO MTEULE
WATEULE WA MUNGU.
Wateule wa Mungu ni watu ambao Mungu amewatenga wao na mataifa au amewatenga na uovu wote, dhambi na machukizo ya kila aina. Hawa ni watu walioteuliwa na Mungu mwenyewe kwa neema ya wokovu. Kwa maana nyingine wateule ni wale waliovua mwenendo wa kwanza na kuvaa utu mpya ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika hali na utakatifu wake wa kweli (Waefeso 4:22). Wamevua utu wa kale pamoja na matendo yake, hawa ndio wale walioonekana kumkiri Yesu Kristo kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yao. Hawa wamekuwa tunu kwa Mungu kwa maana wametii sauti ya Mungu na kulishika neno lake. Hawa ni wale wapendwao na Mungu walioitwa kuwa watakatifu wake. Zaburi 16:3 “Watakatifu waliopo duniani ndio walio bora, hao ndio niliopendezwa nao”. Wakolosai 3:12 “Basi kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana na kusameheana”. Zaidi ya hayo yoye jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. Iweni na imani ya Kristo Yesu mioyoni mwenu na tena iweni watu wa shukrani kwa Mungu. Marko 13: 27 “Ndipo atakapowatuma malaika na kuwakusanya wateule wake toka pepo nne, toka upande wa mwisho wa nchi hata upande wa mwisho wa mbingu”. Mungu amewahesabia haki na akawatukuza kwa hiyo hakuna anayeweza kuwashitaki wateule wa Mungu.
Warumi 3:33 “Ni nani atakaye washitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki”. Na sisi ndugu zangu tuombe neema hii ya Mungu ili tuwe wateule wake tutakaokuwa pamoja na Mwanakondoo, Bwana wa Mabwana na Mfalme wa Wafalme atakapokuja kulichukua kanisa lake.
MZAO MTEULE
Tunajifunza katika neno la Mungu kuwa uzao wa baba yetu wa imani Ibrahimu ni mzao teule kwa BWANA. Mungu alimbariki kwa kumfanya awe na uzao mwingi sana, akamzidisha na kumwongeza. Mungu akafanya agano na Ibrahimu kuwa atakuwa baba wa mataifa mengi na wafalme watatoka kwake. Mwanzo 17:7 “Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako na vizazi vyao kuwa agano la milele”. Hata sisi tumerithi baraka za Ibrahimu, katika Mwanzo 22:18 “Na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watabarikiwa, kwa sababu umetii sauti yangu”. Bwana wetu Yesu Kristo ni uzao wa Ibrahimu. Waebrania 2:16 “maana ni hakika hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu”. Wagalatia 3:16 “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa uzao wake. Hasemi, kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, kwa mzao wako, yaani Kristo”.
Kwa kuwa tunamwamini Yesu Kristo na sisi ni mzao mteule kwa Bwana. Warumi 8:17 “na kama tu watoto basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja nae ili tupate kutukuzwa pamoja nae”. 1 Petro 2:9 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu”. Je wewe na mimi tuko tayari kuzitangaza fadhili za Mungu.
Mfalme Daudi katika Zaburi 89:1 anasema, “Fadhili za BWANA nitaziimba milele, kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako”. Mungu ni mwenye fadhili nyingi na fadhili zake hazikomi, huruma zake hazina mwisho kila kunapokucha ni mpya kabisa, uaminifu wake ni mkuu mno.
Ukimtii Bwana Mungu wako kwa bidii na ukifuata maagizo yake yote utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako yote, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng’ombe wako na wadogo wa kondoo zako (Kumbukumbu la Torati 28:4).
Tunamuomba Mungu uzao wetu na vizazi vyetu tuwe mzao mteule kwake.
KUMILIKI MLANGO WA ADUI
Adui yetu tunayeomba kumiliki mlango wake ni shetani kwani shetani ndiye adui yetu mkuu. 1 Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi (shetani), kama simba angurumaye,huzunguka– zunguka,akitafuta mtu ammeze.” Huyu shetani ndiye tunayetakiwa kumpinga na kufunga mlango wake. Mlango ni mahali pa kuingilia au kutokea. Ukiwa mmiliki wa mlango huo unaweza kuufungua au kuufunga unavyotaka. Mlango wa adui ukishaumiliki utaufunga milele ili adui shetani asiweze kutoka na kuja kunishambulia. Mlango wa shetani hutumika kuleta mashambulizi kwetu na mashambulizi hayo yanaweza kuwa magonjwa, pepo wachafu na machukizo ya kila aina. Mashambulizi hayo yanaweza kuwa ya kimwili na kiroho. Funguo za mlango unaofungua fursa za mashambulizi ni dhambi; uasherati, zinaa, ushirikina, ibada za sanamu, chuki, uuaji na machukizo ya kila aina. Tunawezaje kumiliki mlango wa adui na kuufunga ili usituletee mashambulizi? Hili litawezekana tu kama tutatii sauti ya Mungu. Mungu anasema nasi kwa njia mbali mbali, kupitia neno Lake Takatifu, kupitia ndoto, maono, amri zake, maagizo na maelekezo yake. Je, mimi na wewe tunasikia sauti ya Mungu na kuitii?
KUTII SAUTI YA MUNGU
Baba yetu wa Imani Abrahamu alitii sauti ya Mungu alipotakiwa kumtoa sadaka mwanawe Isaka na Mungu akamkirimia baraka nyingi na uwezo wa uzao wake kumiliki mlango wa adui. Mungu anapendezwa na kufurahishwa na utii. 1 Samweli 15:22 “Naye Samweli akasema,Je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu sawa sawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia kutii ni bora kuliko dhabihu, na kusikia kuliko mafuta ya beberu.” Bwana wetu Yesu Kristo alikuwa mtii hata mauti. Wafilip 2:8-11 “Tena alipooneka anaumbo kama mwanadamu,alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti,naam, mauti ya msalaba.”Mungu akapendezwa naye, kwahiyo tena Mungu alimuadhimisha mno,akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina, ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe la vitu vya mbinguni na vya chini ya nchi na kila ulimi ukiri YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba .Mimi na wewe tunao toa sadaka za shukrani tunatakiwa tuwe watii na wanyeyekevu mbele za Mungu kwa kuwa kipimo kizuri cha utoaji matoleo si wingi tu wa sadaka au ukubwa wa sadaka bali ni utii kwa Mungu unaye mtolea sadaka ya shukrani. Basi ndugu zangu twendeni mbele ya madhabahu ya BWANA siku zote za maisha yetu kwa utii na kwa kuogopa na kutetemeka.Njia nyingine ya kumiliki mlango wa adui ni kwa maombi.
MLANGO WA KONDOO
Bwana wetu Yesu Kristo anasema yeye ndiye mlango wa kondoo. Yohana 10:7, 9, 11,
“Mimi ndimi mlango, mtu akiingia kwa mimi,ataokoka, ataingia na kutoka,naye atapata malisho. Yesu alikufa ili tuwe na uzima kisha tuwenao tele. “Mimi ndimi Mchungaji mwema. Mchungaji mwema hutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.
Yesu Kristo anao kondoo,na kondoo wake waisikia sauti yake naye anawajua nao wanamfuata. Kondoo wa Yesu ni wale wanao mkubali na kukiri kuwa ni Bwana na Mwokozi wao na kumfuata. Kondoo ni wafuasi wa Kristo na Yesu Kristo ndiye Mchungaji mwema wa kondoo na ameutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Yesu anasema Yeye ndio mlango wa kondoo.
Watakaoingia kupitia mlango wa kondoo watapata uzima wa milele. Mlango wa kondoo ni mwembamba Mathayo 7:13 -14 “Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba,maana mlango ni mpana na njia ni pana iendayo upotevuni,nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba,na njia imesonga iendayo uzimani,nao waingiao ni wachache. “Tunamwomba Mungu tuwe kati ya hao wachache watakaoingia kupitia mlango wa kondoo ambao umesonga ili tupate uzima wa milele katika Yesu Kristo Bwana wetu. Yeye aliye naye Mwana anao huo uzima wa milele,asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima (1 Yohana 5:12).
Utapata malisho
Je,ukiingia kwa Bwana Yesu utapata malisho gani? Tutalishwa chakula cha uzima na Yesu Kristo anacho chakula hicho cha kiroho kiletacho uzima wa milele.Yesu Kristo anasema wazi kwenye Yohana 6:48-58 “Mimi ndimi chakula cha uzima hiki ni chakula kilichoshuka toka mbinguni, mtu akila hiki ataishi milele. Na chakula hicho ni mwili wake alioutoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu”.Usipoula mwili wake Mwana wa Adam na kuinywa damu yake,hakuna uzima ndani yako, Kula mwili wa Yesu na kunywa damu yake ni tendo la kiimani la kiroho linaloonesha kumkubali kuwa ni Mtakatifu wa Mungu,Mwana wa mungu,Bwana na Mwokozi wa maisha yetu.Tunakiri juu ya nguvu na uweza wa kifo chake pale msalabani. Tuko tayari kusikia maneno yako,kuyaamini na kuyaishi.Tunapoula mwili wake na kuinywa damu yani neno lake ndipo tunapata afya ya kiroho.
Ulinzi wa kondoo
Kazi nyingine ya mchungaji wa kondoo kando ya kuwalisha anatakiwa kuwalinda ili wasishambuliwe na mbwa mwitu.Mchungaji wa mshahara ambae kondoo sio mali yake akimuona mbwa mwitu hukimbia, na mbwa mwitu huwakamata na kuwatawanya.Mchungaji
mwema (Yesu Kristo) ameutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.Yohana 10:15 “Kama vile Baba anijuavyo nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.”Yupo mlinzi
waroho zetu, Yeye aliye tukomboa kwa damu yake ya thamani pale msalabani.Shetani hataweza kutushambulia nasi tutaishi kwa Amani ndio maana anaitwa mfalme wa amani Bwana mwenye nguvu Je, Ndugu yangu uko kwenye zizi la Bwana wetu Yesu Kristo au uko nje ya zizi ambako yuko adui shetani ambaye kazi yake ni kuchinja,kuharibu na kuua? Tumrudie Mchungaji na Mwangalizi war oho zetu
1Petro 2:25 “Kwa maana mlikuwa mnapotea kama Kondoo, lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu”Kondoo wanaoiskia sauti yake huwaita kwa majina yao na kuwapeleka nje, kisha kutakuwepo kundi moja na Mchungaji mmoja tu ambae ni Yesu Kristo Bwana wetu. Bwana alibariki neno lake.Amen
NAMI NITAWAJALIA MAISHA MAREFU
Mungu anawaahidi wateule wake wamchao, wenye kumtumikia kwa moyo wa ukamilifu na wenye kutenda haki ya kuwa atawajalia maisha marefu. Hesabu ya siku zao ataitimiza kwani anazijua siku za wakamilifu. Imetupasa kumwogopa Mungu na kumpenda, kumheshimu na kumtumikia na kumtii kwa moyo wote. Mithali 10:27 “Kumcha BWANA kwaongeza siku za mtu; bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.” BWANA anasema mtu mwenye haki hakika ataishi. Midomo ya mwenye haki hulisha watu wengi; bali wapumbafu hufa kwa kuwa hawana ufahamu. Mtumishi wa Mungu Nehemia kwa kujua ukweli huo anasema, “Unikumbukie,Ee Mungu wangu, kwa mema yote niliyowafanyia watu hawa(Nehemiah 5:19). Heri mtu yule amkumbukaye mnyonge BWANA atamwokoa siku ya taabu. BWANA atamlinda na kumhifadhi hai. Mungu anaweza kukujalia maisha marefu kama utaenenda kwa ukamilifu na kuomba kama mfalme Hezekia ambaye Mungu alimwambia atakufa. Isaya 38:2-5 “Basi Hezekia akajigeuza akaelekeza uso wake ukutani akamwomba BWANA, akasema, Ee, BWANA kumbuka haya, nakusihi,kwamba nimekwenda mbele zako katika kwelii na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa neno la BWANA likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia BWANA Mungu wa Daudi baba yako asema hivi,Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama nitaziongeza siku zako kiasi cha miaka kumi na tano.” Hata wewe na mimi tukienenda sawa sawa na mapenzi ya Mungu tukimwomba atatuongezea siku za kuishi hapa duniani.
Amri ya nne ina ahadi ya kupata maisha marefu nayo yasema; Waheshimu baba yako na mama yako,siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na BWANA Mungu wako. Imetupasa tusiwakasirishe, wazazi wetu ila tuwaheshimu, tuwatumikie, tuwatii na tuwapende kwa moyo . Mithali 1:8 Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, wala usiiache sheria ya mama yako,kwa maana hayo yatakuwa kilemba cha neema kichwani pako na mikufu shingoni mwako.” Mithali 30:17 “Jicho la mtu amdhihakiye; babaye, na kudharau kumtii mamaye; kunguru wa bondeni wataling’oa, na vifaranga wa tai watalila.”
Imetupasa tuzingatie maonyo haya kwa kuwa kushindwa kuyafuata ni dhambi mbele za Mungu na mshahara wa dhambi ni mauti. Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe bali haki huokoa na mauti. Ukiziacha dhambi zako kwa kutenda haki, ukaacha maovu yako kwa kuhurumia maskini utazidishiwa siku zako za kuishi hapa duniani tena utaishi kwa raha. Wapendwa tusiombe tu maisha marefu hapa duniani bali tuombe karama ya Mungu ambayo ni uzima wa milele katika Yesu Kristo Bwana wetu. Pamoja na kuomba maisha marefu tumwombe Mungu tuwe uzao mteule wenye baraka tele sawa sawa na ahadi zake kwa wateule wake; na sawa sawa na Neno lake. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele Amina.
ULINZI WA MUNGU KWETU
Tunamshukuru Mungu kwa kuzidisha uzao wetu na kuulinda. Katika maisha yetu yote tumeshuhudia ulinzi wa Mungu kwetu. Mungu ndiye alindaye hakuna mwingine awezaye kulinda isipokuwa Yeye peke yake. 1 Petro 1:5 “Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho”. Wala hakuna mtu awezaye kutupokonya katika mkono wa BWANA. Hakika mkono wa BWANA si mfupi hata ushindwe kuokoa. Tunaomba ulinzi wa Mungu kwetu na kwa vizazi vyetu kwa kuwa BWANA ni mwaminifu na wa haki. 2 Wathesalonike 3:3 “lakini BWANA ni mwaminifu atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu”. Tunamwomba Mungu awe mlinzi wetu, atulinde na mabaya yote, azilinde nafsi zetu. BWANA atulinde tutokapo na tuingiapo. BWANA atutie nguvu, atusaidie na atushike kwa mkono wa kuume wa haki yake. Tunamwomba Mungu ulinzi wa nyumba zetu, familia zetu na miji yetu. Zaburi 127:1 “BWANA asipojenga nyumba waijengao wafanya kazi bure, sisi hatutakesha bure kwa kuwa tutakukimbilia wewe. Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Hatutaogopa kwa sababu BWANA wa majeshi yu pamoja nasi Mungu wa Yakobo ni ngome yetu. BWANA anatuambia wana wa Marko’s tusiogope tusonge mbele. Tusiogope kwa sababu BWANA wa majeshi yupo pamoja nasi, atatulinda, atatupigania. Zaburi 121: 3-5, 7 “Asiuache mguu wako usogezwe, asisinzie akulindaye, Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi. Yeye aliye mlinzi wa Israel. BWANA ndiye mlinzi wako, BWANA ni uvuli mkono wako wa kuume. BWANA atakulinda na mabaya yote, atakulinda nafsi yako. BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, tangu sasa na hata milele.
Zaburi 27:1, 4 “BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? BWANA ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani? Neno moja nimelitaka kwa BWANA, nalo ndilo nitakalolitafuta, nikae nyumbani mwa BWANA siku zote za maisha yangu. Niutazame uzuri wa BWANA, na kutafakari hekaluni mwake”.
BWANA sikia kuomba kwetu AMEN.
KUMILIKI MLANGO WA ADUI KWA MAOMBI
Tukiomba kulingana na Neno la Mungu sawa sawa na mapenzi yake tunapata nguvu ya kumiliki mlango wa adui na kuufunga. Kuomba kunatusaidia tusiingie majaribuni au kuufunga mlango wa majaribu. Mathayo 26:40 (a) “Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni.” Yakobo 4:3 (b) “Mwafanya vitu na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi.” Maombi yanauwezo wa kuzuia jambo la kishetani ambalo lilipangwa likupate, lakini kwa maombi yako ya kulizuilia hakika jambo hilo halitakupata. Kwa kuwa Neno la Mungu linatupa mamlaka hayo. Mathayo 18:18 “Amin, nawaambieni, yoyote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni;na yoyote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.” Nguvu na mamlaka hiyo utaipata kwa kumwamini na kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Kumbuka kuwa ukiokoka unakuwa uzao wa Ibrahimu na uzao wa Yesu Kristo. Wagalatia 3:29 “Na kama ninyi ni wa Kristo, basi mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawa sawa na ahadi.” Ahadi mmoja wapo ya uzao wa Ibrahimu ni kumiliki mlango wa adui. Hivyo sifa moja kuu ya uzao wa Yesu Kristo ni uwezo wa kumiliki mlango wa adui. Nje ya uzao huo huwezi kwa namna yoyote ile kufunga mlango wa shetani wala kumkwepa na hila zake. Tunawezeshwa na Yesu Kristo Bwana wetu kumiliki mlango wa adui (shetani) kwa njia ya Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anaingia ndani yetu kisha anatuongoza katika kweli yote ambayo ni Neno la Mungu. Katika vita ya kuufunga mlango wa adui neno la Mungu linatutaka tuvae silaha zote za Mungu kuweza kuzipinga hila za shetani au kwa maana nyingine kuweza kumiliki mlango wa adui. Tusimame na kuvaa dirii ya haki vifuani mwetu. Waefeso 6:16-7 “Zaidi ya yote mkitwaa ngao ya imani ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu,na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu. “Ndugu zangu wapendwa tuufunge mlango wa adui shetani na tubishe hadi mlangoni pa Bwana wetu Yesu Kristo,kwa kuwa ametukaribisha na ameahidi kutufungulia. Mathayo 7:7-8 “Ombeni,nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtaona; bisheni nanyi mtafunguliwa. Kwa maana kila aombaye hupokea,naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.” Katika Ufunuo 3:8 Neno la Mungu linasema, “Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu,wala hukulikana jina langu.” Tujitahidi kuingia katika mlango ulio mwembamba kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze (Luka 13:24).
Tunamwomba Mungu kwa neema yake kuu aturehemu tuingie kupitia mlango mwembamba unaoenda wokovuni, mlango wa kondoo.