• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 25 Nov, 2023
  • Admin


Katika somo hili tutaangalia mambo muhimu tunayopaswa kuzingatia tunapoamua kumfuata Bwana wetu Yesu Kristo na hatimaye kuwa wanafunzi wake. Mambo ya muhimu ya kuzingatia ni mengi lakini katika somo hili tutaangalia mambo muhimu matatu chini ya vichwa vidogo vifuatavyo:-

·       Kujikana mwenyewe

·       Kujitwika msalaba wako

·       Kuacha vyote ulivyo navyo

Neno la Mungu katika Luka 9:23 “Akawaambia wote,mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe ajitwike msalaba wake kila siku anifuate .Unatakiwa ujikane mwenyewe kwanza ndipo uchukue hatua nyingine ya kujitwika msalaba wako.

Kujikana maana yake ni kuachana na dhambi na furaha za dunia hii ambazo ni machukizo mbele za BWANA.Tuache mapenzi yetu, furaha zetu na matakwa ya miili yetu yaliyo kinyume na Mungu. Kwa maana mwisho wa mambo hayo ni mauti. Kwa kuwa mshahara wa dhambi ni mauti.Lakini ukijikana mwenyewe ukiisha kuwekwa huru na kuwa mbali na dhambi na kufanywa mtumwa wa Mungu unayo faida kubwa maana utatakaswa na mwisho wake utapata uzima wa milele. Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.Basi kama ni hivyo ndugu, tu wadeni si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili, kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho mtaishi (Warumi 8:12-13).

Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi na mambo yanayofanana na hayo nawaambia mapema kama nilivyokwisha kuwaambia ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa mbinguni. Na hao waliojikana wenyewe wamekuwa wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake (Wagalatia 5:19-21, 24). Tukiishi kwaRoho natuenende kwa Roho na hapo ndipo tutakapopata uzima wa milele.Maana tu kazi yake tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.Mungu atusaidie tuokoke na kuacha dhambi na kumkiri na kumwamini Bwana Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yetu.Tumfuate na kuwa wafuasi wake waaminifu.

Kujitwika msalaba wako au kuchukua msalaba wako na kumfuata Yesu Kristo Bwana wetu. Msalaba ni alama ya aibu, kudharauliwa, kudhihakiwa, kulaumiwa, kutukanwa na kupata maudhi na mateso.Lakini jambo kubwa zaidi msalaba ni alama ya ushindi baada ya mateso.Neno la Mungu katika 2 Timotheo 3:12 linasema, “Naam na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa.“Tunaomfuata Bwana wetu Yesu Kristo hatuna budi kujua kwamba tunaweza kukutana na mateso mbalimbali ili tumkane Bwana wetu Yesu Kristoau turudi nyuma katika kumfuata na kumtumikia.Neno la Mungu linatufundisha ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.Mtu asifadhaishwe na dhiki hizi, maana ninyi wenyewe mnajua ya kuwa twawekewa hizo. Njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.Mateso ya mwenye haki ni mengi, lakini BWANA humponya nayo yote. Wanafunzi waliojitwika msalaba na kuuchukua na kumfuata Bwana wetu Yesu Kristo walipata mateso mengi, ndio maana Bwana Yesu aliwaambia,

“Watawatenga na masinagogi, naam saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa amtolea Mungu ibada” (Yohana 16:2). Bwana Yesu anawatahadharisha wafuasi wake. Mathayo 10:17 “Jihadharini na wanadamu, kwa maana watawapeleka mabarazani na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa”. Atakayejitwika msalaba wake kwa uaminifu atashinda na yule ashindaye atapewa taji ya uzima wa milele.Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao.Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu.Furahini na kushangilia kwa kuwa dhawabu yenu ni kubwa mbinguni, Kwa Maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu” (Mathayo 5:11-12).

Neno la Mungu linatufundisha kuwa ni heri watu watuchukie, watutenge, watushutumu kwa ajili ya Mwana wa Adamu kwa kuwa thawabu yetu ni kubwa mbinguni. Mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Tunatakiwa kila mtu kujitwika msalaba wake kila siku na kila mahali .Luka 9:23-24 “Akawaambia wote, mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu  atakaye  kuiponya nafsi yake ataiangamiza na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha”. Ili uweze kumweka Yesu kwanza kwa kila jambo ni lazima umpende kuliko vitu vyote na uijue sauti yake na kuitii.Luka 10:27 “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho  yako yote na kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote na jirani yako kama nafsi yako.” Sauti ya Bwana wetu Yesu Kristo tunaijua kwakupitia katika neno lake. Yohana 8:31-32 “Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini ,ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli, tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” Yesu Kristo anasema kwamba kondoo wake waisikia sauti yake naye anawajua nao wanamfuata naye anawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wake (Yohana 10:27-28). Kutii sauti ya Bwana ni bora kuliko sadaka.

Kuacha vyote na kumfuata Bwana Yesu.Bwana Yesu anataka tumtangulize yeye kwanza zaidi ya vitu vyote tulivyonavyo; YESU KWANZA na vingine tutaongezewa. Luka 14:33 “Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.” Yesu Kristo Bwana wetu anasema katika Injili ya Luka Mtakatifu 14:26-27 “Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake na mama yake na mke wake na wanawe na ndugu zake waume na wake; naam hata nafsi yake mwenyewe hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu.” Katika watu wote hawa tunaowapenda tumtangulize Yesu Kristo Mwokozi wetu awe wa kwanza. (Mathayo 10:37-39).

“Apendaye baba au mama kuliko mimi hanistahili; wala apendaye mwana na binti kuliko mimi hanistahili. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata hanistahili.Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza, naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona”.Tunayo mifano mbalimbali katika Biblia ya watu walioitwa na Bwana Yesu wakaacha vyote wakamfuata.Luka 5:27-28

“Baada ya hayo akatoka, akaona mtoza ushuru jina lake Lawi ameketi forodhani akamwambia nifuate.Akaacha vyote akaondoka akamfuata.” Kadhalika Simoni Petro, Yakobo na Yohana  wana wa Zebedayo waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni usiogope tangu sasa utakuwa ukivua watu.Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata (Luka5:10-11). Mtu mwingine aliyeitwa na Bwana Yesu akaacha vyote akamfuata ni Mathayo. Mathayo 9:9 “Naye Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani aitwaye Mathayo akamwambia nifuate.Akaondoka akamfuata.” Hata hivyo katika Biblia Takatifu tunayo mifano ya watu waliotaka kumfuata Yesu lakini baada ya kufanya mambo waliyoyaona kuwa nimuhimu zaidi kwao. Mmoja ni yule aliyemwomba Bwana Yesu ampe ruhusa kwanza aende kumzika baba yake. Lakini Yesu akamwambia, nifuate, waache wafu wazike  wafu wao. Mtu mwingine akamwambia Bwana nitakufuata, lakini nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia  mtu aliyetia mkono wake kulima kisha akaangalia nyuma hafai kwa ufalme wa Mungu (Luka 9:57-61).

Ikiwa tutaamua kuacha vyote tulivyonavyo na kumfuata Bwana wetu Yesu Kristo, Je, tutapata nini? Mathayo 19:27-29 “Ndipo Petro akajibu akamwambia, tazama sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi? Yesu akamwambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti chake cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. Na kila mtu aliyeacha nyumba au ndugu wa kiume au wa kike, au baba au mama au watoto au mashamba kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele. Tumwombe Mungu atusaidie tuwe wafuasi na wanafunzi wazuri wa Yesu.

 Yesu anataka wafuasi wake wahakikishe kuwa wanashika kwa dhati wito mkuu wa Kristo kwa maisha yao yote na wajibu wao ni kuendeleza kazi ya Kristo duniani.TunamwombaMungu wetu atusaidie tumweke Bwana wetu Yesu Kristo KWANZA katika kila jambo, ili tuweze kumzalia matunda mema. Yohana 15:8. “Hivyo hutukuzwa Baba yangu kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.” Yesu Kristo anajifananisha na mti wa mzabibu unaozaa matunda yake.Yohana 15:5 “Mimi ni mzabibu ninyi ni matawi akaaye ndani yangu nami ndani yake huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamuwezi kufanya neno lolote.” Mwanafunzi wa Yesu anatakiwa kuzaa matunda yaitwayo matendo mema. Mathayo 5:16 “Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli.Basi zaeni matunda yapasayo toba.Bwana wetu Yesu Kristo ametuchagua na kutuweka na kututuma twende tukazae matunda na matunda yetu yapate kukaa. Tunda moja tunalotakiwa kulizaa ni tunda la Roho. Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi, juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.” Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia neno la Mungu na kulitendea kazi.Iweni watendaji wa neno wala si wasikilizaji tu. Enendeni uliwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini atahukumiwa.

Katika somo hili tumetafakari kuhusu kujikana mwenyewe, kujitwisha msalaba na kuacha vyote na kumfuata na hatimaye kuwa mwanafunzi wa Bwana wetu Yesu Kristo. Jambo hili sio jambo rahisi isipokuwa kwa neema ya Mungu na msaada wa Roho Mtakatifu.Yohana 6:65 “Akasema,kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.” Hakuna mtu awezaye kumfuata Bwana Yesu kama hakuvutwa na Baba aliyempeleka. Tumwombe Mungu atuvute kwa Bwana wetu Yesu Kristo.

Share This