TAFAKARI “PRAYER ITEMS” ZAKO
Unapokwenda mbele za BWANA kuomba mahitaji yako au haja za moyo wako ni vyema utafakari kwa makini maombi yako au “prayer items” zako. Mambo atakayoomba yawe sawa sawa na neno la Mungu au sawa sawa na mapenzi ya Mungu. Ni vyema ukawa na mistaro ya neno la Mungu ya kusimamia maombi yako.
· Tuombe neema ya wokovu.
Tuombe neema ya wokovu ili kila mmoja wetu aokolewe kwa jina na damu ya Yesu Kristo. Kwa maana tunaokolewa kwa neema kwa njia ya imani, ambayo hiyo haikutokana na nafsi zetu ni kipawa cha Mungu wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akijisifu (Waefeso 2:8-9). Tunaokolewa kwa jina la Yesu.
Matendo ya Mitume 4:12 “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote kwa maana hapana jina lingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo”.
Tunakombolewa kwa damu ya thamani kama ya mwana – kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo (1 Petro 1:18 – 19).
Yanipasa nifanye nini nipate kuokolewa?
· Matendo ya Mitume 16:31 “Wakamwambia mwamini Bwana Yesu nawe utaokoka pamoja na nyumba yako”. Kwa kinywa chako ukiri kuwa Yesu ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Warumi 10: 9-10 “Kwa sababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu”.
· Fanya toba ya kweli utubu dhambi na kuziacha uishi maisha mapya yanayompendeza Mungu (1Yohana 1:8-10). Wakati wa kufanya hivyo ni sasa. 2 Wakorintho 6:2 “Kwa maana anasema wakati uliokubalika nalikusikia, siku ya wokovu nalikusaidia tazama, wakati uliokubalika ndio sasa, tazama siku ya wokovu ndio sasa”.
· Tutapataje kupona tusipojali wokovu. Waebrania 2:3 “Sisi je! Tutapataje kupona tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitishwa kwetu na wale waliosikia”. Tutapona ikiwa tutamwamini Yesu Kristo na kuokoka. Yohana 3:36 “Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia”. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu
Tuombe ndoa takatifu kwa vijana wetu
Tuombe ili vijana wetu wa kiume na wakike katika kizazi hiki na vizazi vijavyo wapate ndoa takatifu. Ndoa takatifu ni muungaano wa kudumu kati ya mume mmoja na mke mmoja. Muungano huu unaunganishwa na Mungu mwenyewe. Mathayo 19:4-6 “Akajibu (Bwana Yesu) akawaambia, hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Hata wamekuwa si wawili tena bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu,mwanadamu asiwatenganishe”. Kwa kuwa ndoa takatifu ni tendo la ki-Mungu halina budi kuheshimiwa na watu wote. Waebrania 13:4 “Na ndoa iheshimiwe na watu wote na malazi yawe safi, kwa maana waasherati na wanzinzi Mungu atawahukumia adhabu. Ili ndoa iheshimiwe na watu wote Mungu anamaagizo kwa wanandoa. Waefeso 5:22-25 “Enyi wake watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Enyi wanaume wapendeni wake zenu kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake”. Mke anayeweza kutii kwa kiasi hicho ni mke mwema kutoka kwa Mungu. Mithali 19:14, 18:21 “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA. Apataye mke mwemwa apata kitu chema; naye ajipatia kibali kwa BWANA. Mwanamume anayempenda mke wake kama Kristo alivyolipenda Kanisa atamwacha babaye na mamaye na kuambatana naye. Ataishi naye kwa akili, atamheshimu atakuwa mwaminifu wala hatamfanyia hiana au hila. Malaki 2:15 (b) “Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana”. Tena atawatunza waliowake yaani wale wa nyumbani kwake. 1 Timotheo 5:8. “Lakini mtu yoyote asiyewatunza walio wake, yaani wale wa nyumbani mwake hasa ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini”. Mume mwenye upendo kiasi hicho atakuwa kichwa cha mkewe. Waefaso 5:23 “Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa, naye ni Mwokozi wa mwili”. Twendeni mbele za Mungu wetu tuwaombee vijana wetu ndoa takatifu. Ndoa takatifu ina baraka za kipekee na neema kutoka kwa Mungu.