SHUKRANI ZETU KWA BWANA PASAKA 2024
Neno la Mungu linatutaka kuwa watu wa shukrani, kwa Bwana Mungu wetu siku zote za maisha yetu. Imetupasa kuwa kila ifikapo majira ya Pasaka wote tutoe shukrani zetu kwa Mungu tukimshukuru Mungu kwa ndimi za kelele za furaha zilizojaa kicheko kwa kuwa Bwana ametutendea mambo makuu.Kila mtu katika familia yake kuna mambo makuu Mungu aliyomtendea.Kama familia moja ya Mungu tumshukuru Mungu kwa mafanikio makubwa yaliopatikana katika elimu.Neno la Mungu katika Mithali 4:13 linatutaka tumkamate sana elimu,tusimwache aende zake ,tumshike,maana yeye ni uzima wetu.Elimu ni ufunguo wa maisha.
Mafanikio haya ni ushuhuda wetu kuwa Mungu ametutendea mambo makuu. Kila mtu aandae sadaka yake kwa BWANA na aitoe katika madhabahu ya BWANA. Neno la kusimamia sadaka zetu Zab 9:1-2 “Nitamshukuru BWANA kwa moyo wangu wote.Nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.Nitafurahi na kukushangilia WEWE .Nitaliimbia jina lako wewe uliye juu”.Shukran zinatupa ukaribu na Mungu kila siku. Wimbo: 309 Karibu na wewe Mungu wangu.
Elimu ya Ufalme wa Mungu.
Pamoja na elimu hii ya ulimwengu huu tunatakiwa kuwa na elimu ya ufalme wa mbinguni.Bwana Yesu akawaambia kwa sababu hiyo,Kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale (Mathayo 13:52).Elimu ya ufalme wa mbinguni ipitayo elimu zote tunaipata katika neno lake takatifu.Bwana wetu Yesu Kristo anataka tujifunze kwake .Mathayo 11:29 “Jitieni nira yangu mjifunze kwangu ,kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo,nanyi mtapata raha nafsini mwenu.” Mtume Paulo akamwambia Timotheo afanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha(Timotheo 4:13) Ndugu zangu tusiwe wavivu wa kusoma na kujifunza neno la Mungu ili tusije kutupwa huko na huko na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu za udanganyifu.Mungu atubariki sisi sote na zaidi sana alibariki neno lake.