• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 24 Nov, 2024
  • Admin

SADAKA YA MZALIWA WA KWANZA KWA WANADAMU NA WANYAMA.

Neno la Mungu linatufundisha kuwa mtoto wa kwanza wa kiume kuzaliwa ni malimbuko kwa BWANA. Na sio watoto tu bali hata wanyama wa kwanza na mazao ya nchi yote hayo ni malimbuko kwa BWANA. Tunatakiwa tumtolee BWANA sadaka ya malimbuko bila kukawia. Kutoka 22:29 “ Usikawie kuleta malimbuko ya matunda yako ya vinywaji vyako. Mzaliwa wa kwanza katika wanao wanaume utanipa mimi. Nawe utafanya hivyo katika ng’ombe zako na kondoo wako.’’ Mungu amewapa nafasi ya pekee wazaliwa wa kwanza, amewatenga kwa ajili yake. Wamepewa  nafasi ya kubeba baraka za familia au ukoo. Yakobo alijua juu ya jambo hili ndio maana akamdanganya ndugu yake Esau akamwuzia haki yake ya mzaliwa wa kwanza ( Mwanzo 25:29-34). Haki yake Esau ya baraka ikahamia kwa Yakobo na Mungu akambariki Yakobo kwa mambo mengi. Mwanzo 35:9-10 “ Mungu akamtokea Yakobo tena aliporudi kutoka Padan-aramu akambariki. Mungu akamwambia, jina lako ni Yakobo; hutaitwa tena Yakobo, lakini Israeli litakuwa jina lako. Akamwita jina lake, Israeli.’’ Hata leo hii tunasema Mungu wa Ibrahimu,Isaka na Yakobo tunapomwita Mungu ( Mathayo 22:32).

Mungu amewapa wazaliwa wa kwanza nguvu,uwezo,ukuu, mamlaka na uongozi. Mzee Yakobo alijua jambo hili akamwambia Reubeni, u mzaliwa wa kwanza, nguvu zangu na malimbuko ya uwezo wangu, umewapita wengine kwa ukuu na nguvu.   

Wazaliwa wa kwanza watakuwa sadaka kwa BWANA kwa kutii sauti ya BWANA na amri zake na maagizo yake yote. I Samweli 15:22 “ Naye Samweli akasema Je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu sawa sawa na kutii sauti ya BWANA? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, na kusikia kuliko mafuta ya beberu.’’

Wazaliwa wa kwanza na wengine wote watakuwa sadaka kwa BWANA kwa kuitoa miili yao kuwa dhabihu mbele za BWANA. Warumi 12:1 “ Basi ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai,takatifu ya kumpendeza Mungu ndiyo ibada yenu yenye maana.’’

Tukumbuke kuna kuzaliwa mara ya pili kiroho yaani kuokoka. Mzaliwa wa kwanza kiroho ni yeyote aliyempokea Bwana wetu Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yake. Amehesabiwa haki bure, naye hupewa nafasi ya mzaliwa wa kwanza hata kama kimwili alizaliwa mwisho kwenye familia. Waebrania 12:23 “ Mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni na Mungu mwamuzi wa watu wote na roho za watu wenye haki waliokamilika.’’ Hawa ndio wamfuatao  Mwana- kondoo kila aendako. Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana – kondoo.

Je, sisi wakristo wa leo tumempa BWANA wazaliwa wetu wa kwanza? Sio kwa sheria kama kwenye Agano la kale bali kwa hiari yetu na kwa kupenda kwa kuwa tunajua ya kuwa jambo hilo linampendeza Mungu. Tuwahudhurishe wazaliwa wetu wa kwanza na kuwakabidhi madhubahuni kwa BWANA kwa njia ya maombi na sadaka. Tumwombe Mungu awabariki na awape nguvu, uwezo, ukuu, mamlaka na uongozi wa familia wazaliwa wetu wa kwanza sawa sawa na mapenzi yake. Jina la BWANA lihimidiwe.

Share This