• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 05 Nov, 2023
  • Admin

·       Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa

Tuanze kutafakari neno hili kwa kutambua kuwa vitu vyote tulivyonavyo ni mali ya BWANA. Mungu ndiye ambaye ametukirimia vitu hivi, kupitia uumbaji wake, tena ametupa bure. Zaburi 24:1 “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA. Dunia na wote wakaao ndani yake. “Mungu ndiye muumba wa vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Mungu ametupa vitu hivyo vyote tuvimiliki  na tuvitumie kwa ajili ya utukukufu wake. Tuwe mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu. Mungu ndiye aliyeanza kutupa vitu kwanza, katika Mwanzo 1:29 “Mungu akasema, tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia,na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndiyo chakula chenu.” Tunamshukuru Mungu kwa ukarimu wake mkuu kwa kutukirimia ulimwengu wake na vyote viujazavyo. Hagai 2:9 "Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema BWANA wa majeshi. Je, Mungu anataka tuvitumie vitu vyote hivi kwa namna gani? Au kwa njia zipi, ili vimletee yeye utukufu? Mungu ametupa vitu hivi ili tuvitumie kwa matumizi yake binafsi, tuvitumie kutunza nyumba zetu, wageni, kanisa na watakatifu wake pamoja na wahitaji mbalimbali kama vile yatima, wajane, maskini na wanyonge. Neno lake linasema tuwape watu vitu nasi tutapewa, kwa hiyo kuwasaidia watu si jambo la hiari bali ni wajibu wa kila mkristo. Tuanze kutafakari makundi mbalimbali tunayotakiwa kuwapa vitu tukianza na wale wa nyumbani kwako. 1Timotheo 5:8 “Lakini mtu yoyote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani kwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini . “Ili imani yetu iwe timilifu mbele za Mungu tunawajibu wa kutunza vyema familia zetu na watu tunaoishi nao katika nyumba zetu. Jambo hili litaleta amani, furaha na upendo katika familia na nyumba zetu. Yakobo 2:15-17 “Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na risiki, na mtu wa kwenu akiwaambia, enendeni, zenu kwa amani mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani isipokuwa na matendo imekufa nafsini mwake.” Katika Waraka wa kwanza wa Yohana 2:17 neno la Mungu linasema, “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, Je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo? Tupendane na tuwape ndugu zetu vitu. 1Yohana4:20-21 “Mtu akisema, nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake ni mwongo, kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake. Kundi la pili ambalo tumeagizwa tuwape vitu na kuwatunza ni wageni, yatima na wajane. Neno la Mungu linasema kuwa Mungu wetu ni baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu katika kao lake takatifu (Zaburi 68:5). Kama watu hawa wana hadhi kubwa hivi mbele za Mungu wewe utaachaje kuwapa vitu. Zaburi 146:9 “BWANA huwahifadhi wageni, huwategemeza yatima na mjane; bali njia ya wasio haki huipotosha .” Sheria ya Mungu inasema usimtese mjane wala yatima. Kutoka 22:21-24 Usimwonee mgeni, wala kumtendea jeuri kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Usimtese mjane yeyote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima. Ukiwatesa watu hao katika neno lolote, nao wakinililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima.” Jifunzeni kutenda mema, takeni hukumu na haki, wasaidinieni walioonewa, mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. Mungu huwafanyia yatima na mjane hukumu ya haki, naye humpenda mgeni, akimpa chakula na mavazi. Basi mpendeni mgeni maana ninyi mwajua moyo wa wageni ulivyo, kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Neno la Mungu linatuonya kuwa tusipotoshe hukumu ya mgeni, wala yatima, wala tusitwae mavazi ya mjane, yawe rehani. Bali kumbuka uvunapo mavuno yako katika shamba lako, ukasahau mganda shambani, usirudi kuuchukua; na uwe wa mgeni, au yatima, au mjane; ili BWANA Mungu wako akubariki katika kazi yote ya mikono yako. Utakapochuma matunda ya mizeituni yako, usirudi kuchuma mara ya pili, yaliyobaki apewe mgeni, na yatima na mjane (Kumbukumbu la Torati 24:17-21). Na mgeni akikaa pamoja nawe katika nchi yako, usimdhulumu. Mgeni akaaye pamoja nawe atakuwa kama mzaliwa kwenu, mpende kama nafsi yako. Neno hili la kuwapa vitu wageni, yatima na wajane linasisitizwa katika Agano Jipya pale neno la Mungu linaposema kuwa dini iliyo safi ni kusaidia yatima na wajane. Yakobo 1:27 “Dini iliyo safi isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa." Wanaukula nyumba za wajane watapata hukumu iliyo kubwa. Tunatakiwa kuwatunza na kuwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli. Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake huyu amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku (1Timotheo 5:3,5). Mayatima na wajane wanatakiwa kumtumaini Mungu kwa kuwa Mungu anawapenda na kuwathamini sana. Kundi lingine tunalotakiwa tulitunze na kulipa vitu ni maskini, wanyonge na wenye uhitaji. Mungu anawaagiza matajiri watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikiane na wengine kwa moyo (1Timotheo 6:18) kwa kuwa Mungu humdhili huyu na kumwinua huyu. Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda. Usimwambie jirani yako nenda, urudi halafu, na kesho nitakupa, nawe unacho kitu kile karibu nawe (Mithali 3:27-28).Neno la Mungu linasema kuwa amdharauye mwenzake afanya dhambi, bali umhurumiaye maskini ana heri. Amhurumiaye maskini humkopesha BWANA; naye atamlipa kwa tendo lake jema. Mwenye jicho la ukarimu atabarikiwa, maana huwapa maskini chakula chake. Kwa maana atamkomboa mhitaji aliapo, na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi. Atamhurumiaaliye dhaifu na maskini, na nafsi za wahitaji ataziokoa .Atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimi na damu yao ina thamani machoni pake. Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha kuwapa vitu maskini, wanyonge na wenye uhitaji ili tuurithi ufalme wa milele. Marko 10:17, 22 “Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyonavyo vyote, uwape maskini , nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate.Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi”. Katika Luka 14:12-14 Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha kuwakarimu  maskini, vilema, viwete na vipofu; “Akamwambia na yule aliyemwalika, ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako,wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo .Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema , viwete , vipofu, nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki Neno la Mungu katika mambo yote linatuonyesha ya kuwa imetupasa kuwasaidia wanyonge na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu jinsi alivyosema, mwenyewe, ni heri kutoa kuliko kupokea .Akuombaye mpe naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini , yeye naye atalia lakini hatasikiwa. Ndugu zangu msikunje uso wala kuwa na huzuni mnapowapa watu vitu vyenu bali toeni kwa upendo na furaha. Yohana 13:34-35 “Amri mpya nawapa, mpendane, kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi”. Mkaribishane ninyi kwa ninyi pasipo kunung’unika. Mungu huwapenda na hufurahishwa na wale wanaotoa kwa moyo wa ukunjufu. 1Wakoritho 13:3 “ Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo hainifaidii kitu”.Kundi lingine  tunalotakiwa kulipa vitu na kulitunza ni kanisa na watakatifu wake. Mungu anapendezwa na watakatifu walioko duniani .Zaburi 16:3 “watakatifu waliopo duniani ndio walio bora, hao ndio niliopendezwa nao.Tunajifunza kutunza watakatifu katika mambo yao ya kimwili kama walivyofanya watu wa Makedonia na Akaya .Warumi 15:26 “Maana imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya watakatifu huko Jerusalemu walio maskini”. Watu wa Makedonia na Akaya walikuwa watu maskini wenye dhiki nyingi lakini kwa furaha na ukarimu wao walitoa vitu kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao yenyewe walitoa vitu vyao. Walitenda hivi kwanza kwa kujitoa nafsi zao kwa Bwana na kuyatenda mapenzi ya Mungu.Katika kanisa hili hakuna mtu aliyepungukiwa wakati wengine wanavyo vitu. Kama ilivyoandikwa, aliyekusanya vingi hakuzidi, wala yeye aliyekusanya vichache hakupungukiwa. Huu ndio moyo tunaotakiwa tuwe nao wakristo tuwahudumie watumishi wa Mungu na tuhudumiane sisi kwa sisi kwa upendo. Luka 12:48 “Na yule asiyejua, naye amefanya yasitahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vingi vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi.” Tukiwapa watu vitu neno la Mungu linasema nasi tutapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachotupa vifuani mwetu. Kwa kuwa kipimo kile kile tupimacho ndicho tutakachopimiwa. 2 Wakorintho 9:6 -11 “Lakini nasema neno hili, apandaye haba atavuna haba, apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu.Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kujaza  kila neema kwa wingi, ili ninyi mkiwa na  riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; kama ilivyoandikwa, ametapanya, amewapa maskini, haki yake yakaa milele. Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu; mkijitajirisha katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu. Maana utumishi wa huduma hii hauwatizimii watakatifu riziki walizopungukiwa tu, bali huzidi sana kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu”. Katika huduma hii mwenye kukirimu afanye kwa moyo mweupe, kwa hiari yake mwenyewe kwa furaha na pendo na unyofu wa moyo wake. Kwa maana mambo yote ni kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo, ili neema yake ikiongezwa sana kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe. Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote; atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo tunazofarijiwa na Mungu

(2 Wakorintho1:3 - 4). Kwa hiyo mkaribishane ninyi kwa ninyi, kama naye Kristo alivyotukaribisha, ili Mungu atukuzwe.          

Share This