· Achilieni nanyi mtaachiliwa.
Neno la Mungu linatufundisha kuwa tusihukumu wala kulaumu watu wengine bali tuwasamehe na kuachilia mioyoni mwetu na kutokumbuka tena. Tusiwe sawa na wale wanaosema nimekusamehe lakini sitasahau. Kusamehe na kuachilia ni tabia tunayojifunza kutoka kwa Mungu wetu. Zaburi 86:5 “Kwa maana wewe Bwana, u mwema, umekuwa tayari kusamehe, na ni mwingi wa fadhili kwa watu wote wakuitao.” Katika Yeremia 31:34 anasema BWANA; “Maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.”Anatuhakikishia kuwa akishasamehe watenda dhambi wenye kutubu hatawaadhibu wakati ujao kwa sababu ya dhambi hizo. Inatufariji sana kujua kwamba Mungu wetu anatusamehe na kusahau. Tuangalie ni mambo gani tunayotakiwa kusamehe na kuachilia ili na sisi tuachiliwe. Katika maisha haya kuna watu wanaotukwaza, wanaotuudhi, wanaotufedhehesha, wanaotuabisha, wanaotuonea na wanaotukosea kinyume na neno la Mungu kwa njia mbalimbali. Watu wa namna hii wanaweza kukukasirisha, kukuhuzunisha na kukuvunja moyo ili usifikie ndoto zako au kusudi la Mungu kwako. Hawa ndio neno la Mungu linatufundisha kwamba tuwasamehe na kuachilia. Mkristo aliyejaa neno la Mungu husamehe na kuachilia bila kuombwa wala kulazimishwa wala kubembelezwa. Kwa maana anajua kuwa kusamehe na kuachilia ni kwa ajili ya faida yake mwenyewe ili Mungu aweze kumsamehe na kusahau uovu wake. Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao na Baba wa mbinguni atawasamehe ninyi. Mathayo 6:12 “ Utusamehe makosa yetu, kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea. “Mathayo 6:14-15 “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu. Matokeo ya kushindwa kusamehe ni huzuni, uchungu, hasira, visasi, na kuinama na kuvunjika moyo. Neno la Mungu linatuonya tusitende mambo ya namna hiyo. Moyo wenye huzuni, uchungu na uliovunjika una hatari kubwa ya kuzaa manung’uniko ambayo ni machukizo mbele ya Mungu. Unapoona dhiki, huzuni na uchungu moyoni mwako usikubali kushidwa wala kukata tamaa bali achilia moyo wako kwa Bwana kwa kuwa unatambua ya kuwa yupo mfariji mwema naye ni Yesu Kristo pekee. Kwa njia hii utapata uponyaji wa roho yako iliyoinama . Mzigo wako huo uachilie kwa Bwana naye atakusaidia na kukujibu kwa wakati na kwa usahihi wote. Mathayo 11:28 “ Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha. Mtwike Bwana fadhaa zako zote. 1 Petro 5:6-7 “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili uwakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.” Zaburi 55:22 “Umtwike BWANA mzigo wako naye atakutegemeza, hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.” Usiwabebe moyoni mwako watu waliokukosea bali wasamehe na waachilie tena waondoe moyoni mwako na hapo ndipo utakapopokea neema ya Mungu, furaha na amani yake. Wakolosai 3:15 “Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja, tena iweni watu wa shukrani. “ Amani yako haipatikani kwa kumkasirikia ndugu yako, haijalishi umesalitiwa kiasi gani au umeudhiwa kiasi gani au kuaibishwa kiasi gani, wewe samehe na achilia utapata amani moyoni mwako. Ukishidwa kusamehe na kuachilia hasira na roho ya kisasi inaweza kukuingia na shetani akivitumia vitu hivyo viwili kukufarakanisha na Mungu. Matokeo ya hasira ni ugomvi na neno liumizalo huchochea ghadhabu. Mhubiri 7:9 “ usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, maana hasira hukaa kifuani mwa mpumbavu. “ Ukiwa na hasira kiasi cha kushidwa kuachilia utakuwa mpumbavu kama neno la Mungu linavyosema. Mathayo 5:22-23 “Bali mimi nawaambieni, kila amwoneaye ndugu yake, hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza, na mtu akimwapiza, itampasa jehanamu ya moto .” Basi ukileta sadaka yako madhabahuni na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neon juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.” Mtu wa hasira huchochea ugomvi, bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano (Mithali 15:18). Hasira na ghadhabu huleta mauaji kama yale ya Kaini na Habili. Tumwombe Mungu atuondolee hasira mioyoni mwetu. Waefeso 4:26, 31-34 “ Muwe na hasira ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala usimpe Ibilisi nafasi. Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasemeheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.” Hasira pamoja na kupoteza amani moyoni mwako inaleta magonjwa mbalimbali mwilini mwako inaleta magonjwa mbalimbali mwilini mwako kama vile; shinikizo la damu (presha),vidonda vya tumbo, kuchanganyikiwa na shida ya kupumua. Tumwombe Mungu atuepushe na hasira na ghadhabu atupe moyo wa kusamehe na kuachilia kwa ajili ya afya njema ya miili yetu na roho zetu. Upatano wetu na ndugu zetu ndio amani yetu na uponyaji wetu. Hasira inaweza kukupeleka katika hatari nyingi na kubwa ya kutaka kulipa kisasi. Usimlipe mtu ovu kwa ovu, angalieni yaliyo mema machoni pa Bwana na machoni pa watu wote. Kaeni katika amani na watu wote, achilia utapata amani moyoni mwako. Msije ukalipa kisasi kwa kuwa hicho unatakiwa kumkabidhi Bwana, Mungu wako maana kisasi si juu yako, kisasi ni cha Mungu. Warumi 12:19 “Wapenzi, msijilipize kisasi, basi ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa, kisasi ni juu yangu mimi, mimi nitalipa, anena Bwana.” Atawahukumu watu wake kwa kweli na haki . Hasara nyingine au madhara mengine ya kutosamehe na kuachilia ni kuvunjika au kuinama moyo, jambo ambalo linaweza kufanya ujione kuwa huwezi na uhisi kushidwa na hivyo kukata tamaa. Kuvunjika moyo kunaweza kuchochewa na matendo mabaya/maovu, maneno ya kuvunja moyo, au kinywa cha ukaidi. Zaburi 69:20 “ Laumu imenivunja moyo, nami ninaugua sana. Nikangoja aje wa kunihurumia wala hakuna, na wa kunifariji wala sikumwona mtu.” Ulimi safi ni mti wa uzima, bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo, bali Bwana huwaokoa. Zaburi 34:18 “ BWANA yu karibu nao waliovunjika moyo, na waliopondeka roho huwaokoa.” Inakupasa kulinda moyo wako kuliko vitu vyote uvilindavyo kwa kuwa una thamani kubwa mbele za Mungu. Mithali 4:23-24 “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo, maana ndiko zitokako chemichemi za uzma. Kinywa cha ukaidi ukitenge nawe, na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe.” Moyoni mwako usiweke kumbukumbu mbaya zinazotokana na midomo michafu au vinywa venye hila, usibebe majeraha au watu walikujeruhi usiye ukamtenda Bwana dhambi. Moyoni mwako uweke nini? Zaburi 119:11 “Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, nisije nikakutenda dhambi.” Midomo yangu izisimulie sifa zako, amri zako, hukumu zote za kinywa chako, shuhuda zako, mausia yako na njia zako Sitalisahau neno lako la uzima, likaalo kwa wingi ndani yangu. Wakolosai 3:16 “ Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa Zaburi na nyimbo, na tenzi za rohoni.” Vinywa vyetu vimwimbie Mungu kwa neema mioyoni mwetu na kutangaza siku ya Bwana iliyokubalika. Tumwombe Mungu atuvike utu mpya tuachane na ule wa zamani, atuvike moyo wa rehema, moyo safi utakaotuletea furaha na amani maishani mwetu tutakaposamehe na kuwaachilia waliotukosea. Kipekee kabisa tuwasamehe na kuwaachilia adui zetu. Neno la Mungu linatuagiza tuwapende adui zetu. Adui yako akiwa ana njaa mpe chakula,tena akiwa na kiu , mpe maji ya kunywa. Maana utatia makaa ya moto kinywani pake na BWANA atakupa dhawabu (Mithali 25:21-22). Wabarikini wanaowaudhi, barikini wala msilaani. Luka 6:27-36 “Lakini nawaambieni ninyi mnaosikia, wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi. Wabarikini wale ambao wawalaani ninyi, waombeni wale ambao wawaonea ninyi.” Mithali 24:17-18 “ Usifurahi adui yako aangukapo, wala moyo wako usishangilie ajikwaapo. Bwana asije akaliona hilo likamkasirisha, akageuzia mbali naye hasira yake.” Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo. Kama unataka Mungu akusamehe na kusahau dhambi zako fanya hivyo hivyo kwa adui zako na wale wote waliokukosea. Achilieni nanyi mtaachiliwa kwa maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Neno la Mungu linatufundisha kuwa adui yako akikupiga shavu moja mgeuzie la pili, naye akikunyang’anya joho lako usimzuilie na kanzu. Mpe kila akuombaye, na akunyang’anyaye vitu vyako, usitake akurudishie. Ukifanya hivi utakuwa umemwonyesha adui yako upendo na fadhili na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru na waovu. Basi iweni na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma. Basi fanyeni hivyo nanyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Achilia jikung’ute mavumbi, inuka na songa mbele; moyo wako usiiname na kufadhaika kwa kuwa BWANA huwaponya waliopondeka moyo na kuziganga jeraha zao. Zaburi 42:11 “Nafasi yangu kwa nini kuinama, na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; kwa maana nitakuja kumsifu, aliye afya ya uso wangu, na Mungu wangu.” Tuwe na huruma inayoleta msamaha wa dhambi hata saba mara sabini atakapotukosea mtu yoyote yule. Huruma na msamaha ni kiini cha habari njema ya wokovu inayopatikana katika Kristo Yesu Bwana wetu. Jikung’ute mavumbi inuka ukaifanye kazi ya Bwana ya kuhubiri Injili kwa watu wote. Ezra 10:4 “Inuka, maana shughuli hii yakuhusu wewe, na sisi tu pamoja nawe, uwe na moyo mkuu, ukaitende.“
Hatuwezi kukamilisha simo hili la kusamehe na kuachilia bila kujifunza kutoka kwa Bwana wetu Yesu kristo. Bwana wetu Yesu kristo pamoja na Pilato kumwona kuwa hana hatia wala hakutenda neon lolote lisolofaa wali mshutumu wakimfunga, wakambebebsha msalaba mzito, wakampiga mijeledi, wakamdhihaki na kisha wakamsulubisha kifo cha aibu. Lakini Bwana Yesu kwa uoendo wake na huruma yake kuu aliwasamehe watesi wake. Luka 23:24 “ Yesu akasema Baba, uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo.” Hapo ndipo Bwana wetu Yesu kristo alipoonyesha kuwa upendo huvumilia, hufadhili, upendo hauhusudu, upendo hautakabari, haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake, hauoni uchungu, hauhesabu mabaya, haufurahi udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote(1 Wakorintho 13: 4-8). Jina la Bwana lihimidiwe.