Katika sehemu hii ya pili ya somo letu tutatafakari juu ya nguvu ya uponyaji inayopatikana katika Yesu Kristo Bwana wetu.
Nguvu hizi za uponyaji zinapatikana katika; neno lake, mwili wake, jina lake na damu yake. Tuanza kwa kuangalia nguvu zilizoko kwenye neno lake. Yesu Kristo ni Neno naye Neno alikuwa Mungu.Yohana 1:1-3 “ Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo, wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. “Yesu Kristo ni Neno naye Neno alifanyika mwili akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba , amejaa neema na kweli (Yohana 1:14).Neema na kweli iliyojaa ndani yake ina nguvu ya uponyaji , kwa neno lake Yesu Kristo wagonjwa wakaponywa , viwete wakatembea, wakoma wakatakasika, vipofu wakaona, viziwi wakasikia, vilema wakatiwa nguvu, pepo wakatolewa na bahari ikanyamazishwa kwa ajili ya utukufu wa jina lake. Tutafakari matukio machache ya watu walioponywa na Bwana Yesu kwa kutumia Neno tu bila hata ya kuwagusa. Akida aliyekuwa na mtumishi wake mgonjwa alimwambia Bwana Yesu sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Naye Yesu akamwambia yule Akida.Nenda zako na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona saa ile ile (Mathayo 8:5-13).Katika kisa cha mama aliyekuwa na binti yake mgonjwa Yesu akamwambia yule mama na iwe kama utakavyo na binti yake akapona tangu saa ile. Kwa neno lake lenye nguvu ya uponyaji aliwatoa pepo, na kuwaponya wote waliokuwa hawawezi. Katika nchi ya Wagerasi watu wawili wenye pepo walikutana naye, wakatoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia ile njia. Yesu aliwatoa pepo hawa kwa neno mmoja tu, Nendeni nao wakatoka wakaingia nguruwe (Mathayo 8:28-32). Wakoma nao walipata nafasi ya kukutana na Bwana Yesu wakatakasika Luka 17:11-15 Yesu alipokuwa akipita katika kijiji kimoja katikati ya Samaria na Galilaya alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa uturehemu. Alipowaona aliwaambia Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika.Vipofu nao walimwendea Yesu ili wapate kuona , kwa neno lake tu walipata kuona Marko 10:46-52 .Huko Yeriko kulikuwa na kipofu mmoja alikuwa ameketi kando ya njia, aliposikia Yesu anapita akapaza sauti yake na kusema, Mwana wa Daudi Yesu unirehemu.Yesu akamjibu akamwambia wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia Mwalimu wangu, nataka nipate kuona .Yesu akamwambia , enenda zako, imani yako imekuponya mara akapata kuona , akamfuata njiani .Sehemu nyingine inayotuonyesha nguvu ya uponyaji iliyoko katika neno lake ni pale alipokutana na watu waliopooza. Mathayo 9:1-8. Wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu alipoona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Ondoka ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako. Akaondoka akaenda zake nyumbani kwake. Marko 3:1-5. Akaingia tena katika sinagogi, na palikuwepo mtu mwenye mkono uliopooza na ilikuwa siku ya sabato.Akamwambia yule mtu nyosha mkono wako, naye akaunyosha, mkono wake ukawa mzima tena .Neno la Yesu lina nguvu sana hata upepo wa bahari humtii. Mathayo 8:23-27 na Marko 4:35-41 wanaelezea kisa cha Bwana Yesu na wanafunzi wake wakiwa chomboni baharini. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo , mawimbi yakapiga chombo hata kikaanza kujaa maji wakati huo Yesu amelala wanafunzi wake wakamwendea wakamwamsha, wakisema, Bwana tuokoe, tunaangamia.Akawaambia mbona mmekuwa waoga , enyi wa imani haba hamna imani bado. Akaamka akaukemea upepo, akaiambia bahari, nyamaza utulie.Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Huyu ndiye Yesu Kristo ambaye hata pepo na bahari zamtii.Katika somo hili tumeona jinsi Bwana Yesu kwa kutumia neno lake tu alivyoweza kuwaponya vilema, viwete, vipofu na wakoma.Kwa njia hii ya miujiza watu waliuona utukufu wa Mungu na Mwanae hata wengine wakamtukuza Mungu wakisema hakika huyu ni Mwana wa Mungu.
Katika sehemu hii inayofuata tutatafakari nguvu za uponyaji zilizoko ndani ya mwili wake na kwenye mkono wake. Mathayo 26:26 “Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake akasema twaeni mle huu ndio mwili wangu.” Mwili wa Yesu ni chakula cha uzima cha kiroho na kimwili. Waulao mwili wa Kristo kwa imani wana uzima ule wa milele na hao ni wale wanaotambua kwamba mkono wa kuume wa BWANA hutenda makuu na tena mkono wa kuume wa BWANA umetukuzwa .Tuangalie matukio machache yanayoonyesha nguvu ya uponyaji iliyoko katika mwili wa Yesu na katika mikono yake. Marko 5:25-32. Habari hii ni ya mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili aliyegusa vazi la Yesu, maana alisema nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona.Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule.Mara Yesu , hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka akasema, ni nani aliyenigusa mavazi yangu.Wanafunzi wake kwa kutokujua kuwa mguso ule ulikuwa na imani ndani yake wakafikiri ameguswa kutokana na msongamano wa watu, lakini Bwana Yesu anayetambua roho na nafsi zetu aliiona imani ya yule mwanamke.Akatazama pande zote ili amwone yule aliyetenda neno hilo. Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote. Akamwambia, binti , imani yako imekuponya enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena.Hapa tunaona mguso uliotoa nguvu za uponyaji ndani ya mwili wa Bwana Yesu.Je, wewe, uko tayari kumgusa Bwana Yesu upate amani na uponyaji wa kimwili na kiroho? Mtu mwingine ambaye Yesu alimgusa akapona ni mkwe wa mtume Petro.Mathayo 8:14-15 .” Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro , akamwona mkwe wa Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa. Akamgusa mkono, homa ikamwacha, naye akaondoka akawatumikia.Katika nchi ya Genesareti walipomtambua walituma watu kwenda nchi zile zilizo kando kando wakamletea wote waliokuwa hawawezi ; nao wakamsihi waguse hata pindo la vazi lake tu, na wote waliogusa wakaponywa kabisa (Mathayo 14:34-36). Mathayo 9:27-29 “Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti wakisema, uturehemu Mwana wa Daudi. Naye alipofika nyumbani wale vipofu walimwendea Yesu akawaambia; Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia Naam, Bwana. Ndipo alipowagusa macho, akasema kwa kadiri ya imani yenu mpate. Macho yao yakafumbuka”.Marko 3:10 “ Maana aliponya wengi hata wote waliokuwa na msiba wakamrukia wapate kumgusa.” Nguvu zingine za uponyaji tunazishuhudia katika mkono wake. Kila mwenye imani Bwana Yesu alipomgusa kwa mkono wake au kumshika mkono alipata uzima au uponyaji.
Jina la Yesu Kristo wa Nazareti ya Galilaya lina mamlaka, uweza na nguvu kubwa ya uponyaji, hili ni jina lipitalo majina yote hapa duniani , kule mbinguni na hata kule kuzimu. Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno,akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe , la vitu vya mbinguni na vya duniani, na vya chini ya nchi, na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.” Yesu Kristo ametupa jina hili lenye nguvu ili na sisi watumishi wake tuweze kuendeleza ufalme wa Mungu.Kwa njia hii Mungu anafanya miujiza hata leo kupitia watumishi wake wapakwa mafuta wa Bwana. Matendo ya miujiza na uponyaji ni karama ambazo anatoa Roho Mtakatifu kwa wote wamwaminio. Wakolosai 3:17 “ Na kila mfanyalo kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.” Tumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Kristo, hali tukinyenyekea katika kicho cha Kristo.
Ni jambo la kweli na hakika kwamba Jina la Yesu linayo nguvu ya kumsaidia mtu aaminiye kufanya jambo lolote hapa duniani, mradi tu liwe ni jambo jema la kumpendeza Mungu.
Katika somo hili tutatafakari zaidi nguvu za jina la Yesu katika miujiza ya uponyaji wa kimwili na kiroho.Mathayo 10:1-8 “Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.” Katika Marko 16:15-17 Bwana Yesu anatoa amri kwa wanafunzi wake,”Akawaambia enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini atahukumiwa.Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio, kwa jina langu watatoa pepo, watasema kwa lugha mpya, watashika nyoka, hata wakinywa kitu cha kufisha hakitawadhuru kabisa, wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.” Hakika yote yanawezekana kwake yeye aaminiye.Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri (amri hii nawapa pendaneni). Yohana 3:18”Amwaminiye yeye hahukumiwi, asiyemwamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.” Yesu Kristo katika Yohana 14:12-14 anasema, “ Amini , amin, nawaambieni, yeye aniaminiye mimi,kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya, naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.” Yesu Kristo anasema tukimwomba baba neno lolote atatupa kwa jina lake.Hata sasa tukiomba neno kwa jina lake tutapata ili furaha yetu iwekamilifu kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.Wanafunzi wa Bwanaa Yesu walitoka wakahubiri kote kote. Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.Mungu akafanya miujiza ya kupita kawaida kwa mikono ya Paulo Mtume. Matendo 19:11-12.” Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida, hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka”. Paulo alimponya baba yake Publio aliyekuwa anaumwa homa na kuhara damu.Matendo 28:8-9 “Ikawa babaake Publio alikuwa hawezi homa na kuhara damu Paulo akaingia kwake akaomba, akaweka mikono yake juu yake, na kumpoza. Yalipokwisha kutendeka hayo wengine waliokuwa na wagonjwa katika kisiwa wakaja wakapozwa.” Kando ya magonjwa hata pepo wanatii jina la Yesu Kristo.Luka 10:17-20 2 Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha wakisema, Bwana hata pepo wanatutii kwa jina lako.” Yesu akawaambia msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni. Akatokea mtu mmoja ambaye hakuwa pamoja na wanafunzi lakini aliweza kutoa pepo. Marko Mtakatifu 9:38-40 “Yohana akajibu, akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi. Yesu akasema, msimkataza kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya muujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya, kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu.” Walitokea watu wengine ambao hawako upande wa Bwana Yesu nao wakajaribu kutoa pepo kwa jina la Yesu.Yule pepo akawaambia tunamjua Paulo na tunamjua Yesu ninyi ni nani? Kwa hasira wale pepo wakawarukia na kuwashinda nguvu nao wakakimbia kwa hofu.Jina hili linatumika kwa wale waaminio kuwa Yesu ni Bwana na mwokozi wa maisha yao (waliookoka). Paulo alimponya kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi. Matendo ya Mitume 16:16-18 “Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuhubiri njia ya wokovu .Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika , akageuka akamwambia yule pepo, nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.” Jina la Yesu lina nguvu nyingi linaponya viwete. Matendo 3:1-10 Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali saa tisa. Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu na kuwekwa kwenye mlango wa hekalu uitwao Mzuri.Alipowaona Petro na Yohana aliwaomba sadaka .Lakini Petro akasema , mimi sina fedha , wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti; simama uende. Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda akiruka-ruka kwa furaha na kumsifu Mungu.Katika Waraka wa Yakobo 5:14-16 neno la Mungu linatufundisha kuwa jina la Yesu linaweza kutumika pamoja na mafuta kumpaka mgonjwa naye akapona. “Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa Kanisa , nao wamwombea na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua, hata ikiwa amefanya dhambi atamsamehe .Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana mpate kuponywa”. Katika matendo haya makuu aliyoyafanya Bwana Yesu na wanafunzi wake yalifanyika ili Mungu asifiwe na kutukuzwa. Walioponywa walimtukuza Mungu na wale walioshuhudia matendo hayo walimsifu na kumtukuza Mungu .Matendo 19:17-18, 20 “Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa. Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama , wakidhihirisha matendo yao.Hivyo ndivyo neno la Bwana lilizidi na kushinda kwa nguvu .Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.
Sehemu hii ya mwisho ya somo hili tutatafakari nguvu iliyoko ndani ya damu ya Yesu.Ni damu yenye nguvu ipitayo damu ya mafahali. Katika Agano la Kale damu ya mafahalli (ng’ombe na kondoo) ilitumika kama sadaka ya ondoleo la dhambi . Waebrania 9:22 “Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.” Katika Agano Jipya Mungu Baba amemtoa mwanawe wa pekee Yesu Kristo kuwa Mwana –kondoo wa sadaka kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu sisi wanadamu . Huyu ndiye Yohana Mbatizaji alipomwona alisema, “ Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake.Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake akasema , Tazama, Mwana- kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu (Yohana 1:27,29).” Huyu ndiye Yesu Kristo aliyesulubiwa pale msalabani Golgota na damu yake ya agano jipya ikamwagika.
Hii ndiyo damu ambayo tutatafakari nguvu zake za uponyaji wa kimwili na kiroho. Damu ya Yesu ina nguvu ya kukuondolea shida zako zote ikiwa una imani, unapotamka damu ya Yesu katika maisha yako unatakiwa uwe na imani ya kutosha juu ya nguvu na uwezo wa hiyo damu hapo ndipo utaona matendo makuu ya Mungu kama vile uponyaji. Hakika ipo nguvu ya ajabu ndani ya damu ya Yesu. Kwa njia ya imani katika damu yake, damu ya Yesu inafanya mambo mengi sana; inatakasa ulimwengu, inaponya na kutulinda, inanena mema juu yetu, inamshinda shetani, inaleta ondoleo la dhambi, na kufanya upatanisho baina ya Mungu na wanadamu inatupa uzima wa milele, haina mwisho wala haipungui nguvu.