· Msilaumu nanyi hamtalaumiwa.
Neno la Mungu linatuonya kuwa tusilaumu wala kumnung’unikia Mungu wala watumishi wake wala ndugu tunaoshi nao kwa kuwa hayo ni machukizo mbele yake. Waraka wa Yuda 1:16 “Watu hawa ni wenye kunung’unika, wenye kulalamika, waendao kwa tama zao, na vinywa vyao vya nena maneno makuu mno ya kiburi, wakipendelea watu wenye cheo kwa ajili ya faida.” Hawa ni wale wafuatao mwili katika tamaa ya mambo machafu, na kudharau, mamlaka. Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana matakatifu, ijapo kuwa malaika ambao ni wakuu zaidi kwa uwezo na nguvu, hawaleti mashitaka mabaya juu yao mbele za Bwana (2 Petro 2:10-11). Na wengi watafuata ufisadi wao, na kwa hao njia ya kweli itakanwa. Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno ya kutugwa, ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii (1Petro 2:2-3). Wana wa Israeli mara kadhaa walimlaumu Musa na kumnung’unikia Mungu walipopata dhiki ya vita, njaa na kiu ya maji. Wakadai ni heri wangeachwa Misri kuliko kuja kufia jagwani. Hesabu 14:1-3 “Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia, watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung’unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona BWANA anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga. Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; Je! si afadhali turudi Misri. “Mungu alichukizwa na manung’uniko yao akawaadhibu kutoiona nchi ya ahadi na akawaangamiza makutano wote waliomdharau Mungu kwa tauni na wengi wakafia jangwani . Hesabu 21:5- “Watu wakamnung’unikia Mungu na Musa, mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani. Maana hapana chakula wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. BWANA akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma ,watu wengi wakafa.” Walipotubu Mungu aliwawekea nyoka wa shaba ambaye wakimtazama wanaishi. Kutoka 16:2-3 “Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung’unikia Musa na Haruni huko barani. Wana wa Israeli, wakawaabia, laiti tungelikufa kwa mkono wa BWANA katika nchi ya Misri, hapo tulipo keti karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba, kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote.” Kutoka 17:3 “Watu wakawa na kiu huko, na wakamnung’unikia Musa, wakasema, mbona umtupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?” Mungu aliwapa mana pamoja na maji lakini matokeo ya wana wa Israeli ya kumjaribu Mungu yalimkasirisha Mungu. BWANA akamwambia Musa, mtakataa kuyashika maagizo yangu na sheria zangu hata lini? Hata sisi leo hii Mungu anatuonya tuyachunge maneno ya midomo yetu yasiwe ya kulaumu. Tujifunze kupitia kwa Bwana wetu Yesu Kristo aliposhutumiwa na kuhukumiwa kifo cha msalaba. Isaya 53:7 “ Alionewa lakini alinyenyekea, wala hakufunua kinywa chake, kama mwana kondoo apelekwaye machinjoni, na kama vile kondoo anyamazavyo mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.” Yeye alipotukanwa hakurudisha matukano, alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo tunajifunza kuwa watakaolaumiwa na kushutumiwa kwa ajili ya Mungu wana dhawabu nyingi. Mathayo 5:10-12 “Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na wakuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia, kwa kuwa dhawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.” Neno la Mungu linasema, mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu, kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia. Ikiwa Roho wa utukufu wa Mungu anakaa ndani yetu tunatakiwa kuchunga vinywa vyetu ili tusilaumu tusije nasi kulaumiwa. Hatuna budi kutambua kuwa lawama na shutuma humvunja mtu moyo, hufedhehesha, huhuzunisha na kuaibisha. Zaburi 69:7, 19-20 “Maana kwa ajili yako nimestahili laumu, fedheha imenifunika uso wangu. Wewe umejua kulaumiwa kwangu, na kuabika na kufedheheka kwangu, mbele zako Wewe wako watesi wangu wote. Laumu imenivunja moyo, nami ninaugua sana. Nikangoja awe wa kunihurumia, wala hakuna, na wakunifariji, wala sikumwona mtu. Mwimba zaburi hizi mfalme Daudi alitambua kuwa kimbilio na tumaini lake ni Mungu peke yake wala hakuwategemea wanadamu. Zaburi 70:1-2, 71:1-2,7 “Ee Mungu uniokoe, Ee BWANA unisaidie hima. Waabike, wafedheheshe, wanaotafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, wapendezwao na shari yangu. Ee Mungu unijilie kwa haraka. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu. Ee BWANA, usikawie. Nimekukimbilia Wewe Bwana, nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye, uniopoe, unitegee sikio lako, uniokoe,. Nami nitatumaini daima, nitazidi kuongeza sifa zake zote.” Badala ya vinywa vyetu kutumika kwa ajili ya kulaumu wengine, vitumike kumsifu Mungu na vinywa vyetu kutangaza wokovu wake na haki yake. Zaburi 71:8, 15, 23-24 “Kinywa changu kitajazwa sifa zako, na heshima yako mchana kutwa. Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako mchana kutwa, maana sijui hesabu yake. Midomo yangu itafurahi sana nikuimbiapo, na nafasi yangu uliyoikomboa. Ulimi wangu nao utasimulia haki yako mchana kutwa. Kwa maana wameaibishwa, wametahayarika, wanaonitakia mabaya.” Tujifunze kwa mfalme Daudi kuisafisha midomo na vinywa vyetu ili kila tunalolisema liwe na kibali cha Mungu. Zaburi 19:14 “Maneno ya kinywa changu, yapate kibali mbele zako. Ee BWANA, mwamba wangu na mwokozi wangu. “Mithali 15,2,4,7 “Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri, bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu Ulimi safi ni mti wa uzima, bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo. Midomo ya wenye haki hueneza maarifa, bali moyo wa mpumbavu haufanyi hivyo.”Tunapolaumiwa na tunaposimagwa masimango mengi tuwe wavumilivu na tena tuwe tayari kuwasamehe watesi wetu. Wakolosai 3:12-24 “Basi kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole,uvumilivu, mkichukiliana na kusamehana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu.”mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.” Usikubali kushidwa na ubaya bali uushinde ubaya kwa wema. Usimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote na mbele ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mkae siku zote katika amani na watu wote hata ukamilifu wa dahari usilaumu ili nawe usije laumiwa kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. Bwana alibariki Neno Lake. Amina.