NAHUMU 1:9-10 “Mnawaza nini juu ya BWANA? Yeye atakomesha kabisa, mateso hayatainuka mara ya pili. Kwa maana wangawa kama miiba iliyotatana, na kunywesha kana kwamba ni katika kunywa kwao, wataliwa kabisa kama mabua makavu”
Tunapozunguzia juu ya mawazo tunayo waza maana yake ni kuweka mipango/ mikakati, makusudi, kufikiri na kutafakari. Swali analoulizwa kila mmoja wetu leo ni hili, unawaza nini juu ya BWANA? Kabla hatujajibu swali hili hebu tuangalie Mungu anawaza nini juu yetu. Isaya 55:8–9 “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; aseme BWANA. Kwa maaana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.” Maana BWANA asema hivi nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza (Yeremia 29:11-12). Ikiwa Mungu anatuwazia mambo mema ya kutupa amani na tumaini, je wewe umafikiria nini juu ya Bwana? .Hapa tuna watu wa aina mbili; wale wanaofikiria juu ya ulimwengu huu na wale wanafikiria juu ya ufalme wa Mungu. Wanaofikiria juu ya ulimwengu huu na tamaa zake wanawaza juu ya mali, fedha, kazi, biashara, familia na mengi yanayofanana na hayo bila ya kumtanguliza Mungu kwanza. Wanasumbuka wale nini na wavae nini hawajui kwamba vitu hivi Mungu atawapa ikiwa watamtumaini yeye. Msisumbukie mambo ya ulimwengu huu kwa kuwa Mungu anajua mahitaji yenu. Mathayo 6:33-34 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake, na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe.” Wale wanaowaza juu ya ufalme wa Mungu wameweka tumaini lao kwa BWANA, wanatafuta chakula chenye uzima wa milele. Yohana 6:51. “Mimi (Yesu Kristo) ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” Watu wengine wanawaza juu ya shetani na majaribu anayowajaribu kuliko kuwaza juu ya Mungu na uweza wake na kumtafakari Kristo usiku na mchana. Tunatakiwa tuwaze na kutafakari Neno la Mungu. Wafilipi 4:8. “Hatimaye ndugu zangu, mambo yoyote yaliyo kweli,yoyote yaliyo ya staha, yoyote yaliyo haki, yoyote yaliyo safi yoyote yenye sifa njema, ukiwepo wema wowote, ikiwepo sifa nzuri yeyote yatafakarini hayo. “ Neno la Mungu lisiondoke machoni pako ulihifadhi ndani ya moyo wako maana ni uhai na afya ya mwili wako. Zaburi 119:11” “Moyoni mwangu naliweka neno lako, nisije nikakutenda dhambi.” unapoumwa usiwaze na kutafakari ugonjwa wala kuwaza maumivu yake bali tafakari neno la Mungu juu ya uponyaji na ulihifadhi ndani ya moyo wako kwa matumaini huku ukiamini. Wakolosai 3:16 “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, nyimbo, na tenzi za rohoni, huku mkimwamini Mungu kwa neema mioyoni mwenu.” “Mungu anasema kama hivi ndivyo tunavyowaza juu yake yeye atakomesha kabisa, mateso hayatainuka mara ya pili . Kwa maana nyingine Mungu atatuokoa na dhiki kwa kutusamehe dhambi zetu na kutupa furaha na uzima wa milele, atakomesha mateso yote yanayotokana na utumwa wa shetani na kutuweka huru katika Yesu Kristo, Bwana wetu. Zaburi 50:15 “Ukaniite siku ya mateso; nitakuokoa, na wewe utanitukuza, Ee BWANA, uturuhemu, tumekungoja wewe; uwe wewe mkono wetu kila asubuhi na wokovu wetu pia wakati wa taabu. 1 Petro 5: 6–7 “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.” Yesu Kristo akishatukomboa kwa njia ya msalaba anatuweka huru na kutupa furaha yake. Yohana 8:36 “Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.” Tena mtaifahamu kweli nayo hiyo kweli itawaweka huru. Kristo amekuja kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari njema za kufunguliwa kwao, vipofu kupata kuona tena na kuwaacha huru waliosetwa. Uhuru tunaopata kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo unatuletea furaha kubwa mno. Wafilipi 4:4-7 “ Furahini katika Bwana siku zote tena nasema furahini upole wenu na ujulikane na watu wote.Bwana yu karibu, msijisumbue kwa neno lolote, bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.” Tukiisha kuwekwa huru na kupewa furaha tutapewa pia furaha ile ya uzima wa milele.Warumi 6: 22- 23 “Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru na kuwa mbali na dhambi na kufanywa watumwa wa Mungu, mnayofaida yenu ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele. Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Wakati Bwana akitukomboa na yule mwovu shetani atatulinda kwa kuweka mazingira magumu kwa mwovu shetani kuweza kutufikia. Katika Biblia ya kiingereza ule mstari wa kumi (Nahumu 1:10) Bwana anasema,” They will be entangled among thorns and drunk from their wine, they will be consumed like dry stubble. “Neno la Mungu linasema maadui hawa watazungushiwa miiba na ulevi na tena waliwa kabisa kama mabua makavu. Mungu anatupa ulinzi adui wanapoinuka juu yetu na shetani anapotaka kutuangamiza. Mungu anatupa ulinzi wa kimwili na kiroho. Tangu enzi za wana wa Israel Mungu amewalinda wafalme mbalimbali kama Daudi na watumishi wake pia. Tunayo mifano mingi katika Agano la Kale la watumishi wa Mungu waliopewa ulinzi wa Mungu kama vile Daniel alivyoweza kupona katika tundu la simba na maadui zake kuangamizwa na vijana akina Shedrack, Meshack na Abednego waliokataa kuabudu sanamu ya mfalme. Mungu akawalinda katika tanuru la moto lakini akawaangamiza maadui zake wakateketea kabisa katika moto ule kama mabua makavu. Mfalme Daudi kwa kutambua ulinzi aliopewa na Mungu dhidi ya maadui zake alitambua pia ya kuwa Mungu ni ngome na ngao na kimbilio lake kwa sababu hiyo alimwimbia Mungu nyimbo za sifa na utukufu.
Ulinzi wa kiroho kutoka kwa Mungu ni hitaji letu kubwa sana kwa kuwa mshitaki wetu ibilisi/shetani anayeunguruma kama simba yuko tayari kuchinja, kuiba na kuharibu roho zetu. Habari njema ni kuwa vita hivi hatuwezi kuvishinda kwa nguvu zetu wenyewe bali tunaye jemadari mkuu Yesu Kristo atupaye kushinda. Nasi tumpinge ibilisi tukiwa dhabiti katika imani naye atakimbia.
1 Wakorintho 15:57-58 “Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.” Kwa kuwa Bwana ni mwaminifu atakayetufanya imara na kutulinda na yule mwovu. Na amani ya Mungu ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu. Katika vita hii ni lazima tuwe na silaha na vitendea kazi. Waefeso 6:10-14 neno la Mungu linatutaka kuwa hodari katika Bwana, tuvae silaha za Mungu na dirii ya haki na utayari tupatao kwa Injili ya amani ili tuweze kuzipinga hila za shetani. Kushinda kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili,juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Ili tuweze kusimama tunatakiwa kupokea chepeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu, kwa sala na maombi. Inatupasa kukaa ndani ya zizi la Bwana Yesu kwa kuwa yeye ni mchungaji wetu mwema anayetoa uhai wake kwa ajili ya kondoo (yaani sisi wanadamu).
Yohana 10:1,14 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema hutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mimi ndimi mchungaji mwema, nao walio wangu nawajua, na walio wangu wanijua mimi. “Je wewe ndugu yangu upo kwenye zizi lipi? Mimi nitakaa nyumbani mwa Bwana milele, kama Daudi nitaliimbia na kulisiifu jina lake daima. Zaburi 22:22 “Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu, katikati ya kusanyiko nitalisifu.” Amina.