• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 05 Nov, 2023
  • Admin

MUNGU ANASEMA NINI KUHUSU NDUGU.

Bwana Yesu Kristo asifiwe!

Wapendwa ndugu zangu katika Kristo Yesu Bwana wetu, tumesikia kutoka kwa kaka yetu mkubwa ndugu Vincent Marko Shaidi, wengine baba mkubwa na wengine babu alivyotueleza wazee wetu walivyotuasa jinsi ya ndugu kuishi. Mimi nimepewa jukumu la kuangalia na kuchunguza maandiko matakatifu yaani Biblia ili kuona Mungu anasema nini kuhusu ndugu. Leo nimeangalia maeneo machache kama ifuatavyo:

1.       UPENDO

Marko 12:28 – 34

Ni amri ipi iliyo ya kwanza?

Yesu akamjibu ya kwanza ndiyo hii sikia Israel Bwana Mungu wetu ni mmoja, nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, mpende jirani yako kama nafsi yako.

Swali: Jirani yako ni nani?

Jibu:   Jirani yako ni mtu yeyote isipokuwa wewe. Hivyo hata ndugu yako ni jirani yako. Mfano wa msamaria mwema – Luka 10:25-37.

Warumi 12:9-10

Pendo lisiwe na unafiki

Kupendana ninyi kwa ninyi

Kuchukia lililo ovu na kutenda lililo jema kwa pendo la undugu mpendane ninyi kwa ninyi na kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu.

1Yohana 4:20-21

Mtu akisema nampenda Mungu naye anamchukia ndugu yake ni mwongo, kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye anamuona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye ya kwamba yeye ampendaye Mungu ampende na ndugu yake.

1Yohana 3:15

Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji nanyi mnajua ya kuwa kila muuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake.

2.      SADAKA

Mathayo 5:21-24

Basi ukileka Sadaka yako madhabahuni na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu, kisha rudi uitoe sadaka yako.

3.      CHAKULA NA VINYWAJI

Warumi 14:1-23

Mungu anaonya kuhusu chakula, vinywaji na siku, anaonya juu ya kumhukumu ndugu yako au kumdharau na kumkwaza. Tufuate mambo ya amani, haki na furaha na upendo katika roho mtakatifu. Kwani ufalme wa Mungu sio katika kula na kunywa, lakini wewe ukila huku una mashaka moyoni kwako wewe ni dhambi kwa sababu hukula kwa imani.

4.      MALI NA FEDHA

1Kor 6:9 (a)

Ndugu kushitakiana tena kwa wasio amini.

Afadhali kudhulumiana kuliko kushitakiana.

Afadhali kunyang’anywa mali zenu

Tena mnadhulumu na ndugu zenu

Wadhalimu hawataurithi uzima wa milele.

5.      KUHUKUMIANA

Yakobo 4:11-12

Ndugu msisingiziane

Kuhukumiana

Unani wewe umhukumuye mtu mwingine.

Luka 6:39-42

Toa kwanza boriti kwenye jicho lako ndipo utaona kibanzi kwenye jicho la mwenzako.

6.      MAONYO

Wagalatia 5:13

Kutokufuata Mwili

Kutumikiana kwa upendo

Angalieni msije mkaangamizana

Efeso 6:1-4

Enyi watoto watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki.

Waheshimu baba na mama yako, hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi upate heri, ukae siku nyingi katika dunia.

Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana.

7.      MWISHO

1Kor 13:1-8 (a)

Nijaposema kwa lugha za wanadamu na malaika kama sina upendo nimekuwa shaba iliyo na upatu uvumao.

Nijapokuwa na unabii na kujua siri zote na maarifa

Nijapokuwa na imani kiasi cha kuhamisha milima

Nikitoa mali zangu zote niwape maskini

Tena nikitoa mwili wangu niungue moto kama sina upendo mimi si kitu (hainisaidii kitu).

Bali upendo:-  Huvumilia, huhifadhi, upendo hauhusudu, upendo hautakabari, haujivuni, haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, hauoni uchungu, hauhesabu mabaya, hauufurahii udhalimu.

Upendo:-hufurahi pamoja na kweli, huvumilia yote, huamini yote, hustahimili yote, hutumaini yote, upendo haupungui neno wakati wowote.

1Petro 3:8-12

Neno la Mwisho ni hili, Muwe na nia moja wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu, watu wasiolipa baya kwa baya au laumu kwa laumu, bali wenye kubariki, kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi Baraka.

Kwa maana atakae kupenda maisha, na kuona siku njema, auzuie ulimi wake usinene mabaya na midomo yake isiseme hila.

Na aache mabaya, atende mema, atafute amani, aifuate sana.

Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, na masikio yake husikiliza maombi yao, bali uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya.

Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na Ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote.

Amina.


 MAOMBI KWA AJILI YA UPENDO WA KINDUGU

Ee Bwan wa majeshi, Baba yetu wa mbinguni, muumba wa mbingu na nchi mwenye enzi yote , sisi tulio watoto wako tunakuomba utupe upendo wako ili nasi tupendane kama Yesu alivyotufundisha. Tangu mwanzo ulivyotuumba umetuonyesha upendo wako kwa kumtoa mwanao mpendwa kufa kwa ajili yetu.

Kwa kufa kwake sisi tumepona. Yote tunayotaka watu watufanyie na sisi tuwafanyie kwa upendo na huruma. Tutumikiane wema kwa upendo na nguvu ya neno lako. Tuzae matunda yanayokupendeza wewe Mungu wetu. Tupe uwezo wa kumsaidia ndugu kwa hiari akiwa shidani, kwa kuwa hata sisi twapewa vyote na wewe Baba yetu wa mbinguni. Tusiwachukie ndugu waliotukosea ila tupatane vyema tena tusameheane kwa kila jambo.

Tusiwahukumu ndugu waliokosa sana tukumbuke hata sisi tuna makosa mengi.

Tusiwahukumu wengine ili nasi usije ukatuhukumu. Mwneye dhambi tumwonye kwa upole na upendo tumsaidie ajue njia ya kweli. Bwana utuvike sote mavazi ya uongofu. Ututengeneze vyema tule karamu yako pamoja na watakatifu wako. Tuwe na mwisho mwema wenye furaha na uzima wa milele.

Ee Mungu, tuwezeshe kuwa mfano mwema kwa wale tunaoishi nao, tuwe wa kweli katika kila tufanyalo, tuwe makini na waangalifu katika kutimiza kila wajibu. Tuwe safi na kutenda kwa kiasi katika mambo yote. Tuwe na huruma, unyenyekevu na ukarimu kwa wote, ili moyo wa Kristo ndani yetu uonekane na watu wote watambue kuwa tu wafuasi wako. Baraka na heshima na utukufu na uweza una wewe Mungu wetu uketiye juu ya kiti chako cha enzi, pamoja na Mwana - Kondoo, hata milele na milele. Katika jina lako Yesu tumeomba.

Amen

Share This