Tusisahahu
kuwa katika somo hili tunajifunza juu ya ahadi za Mungu ambazo tunaweza kuzitumia
kuomba sawasawa na mapenzi yake.Mungu
analinda miili yetu kwa kutuepusha na hatari, ajali na magonjwa.Mungu analinda
watoto wetu pamoja na mali zetu ; mali zile zinazotumika katika kutukuza jina
lake yaani kwa utukufu wake. Tukimtumaini BWANA , yeye ni mwaminifu atakayetufanya
imara na kutulinda na yule mwovu pamoja na kufanya mlango wa kutokea.1 Korintho
10:13 “ Jaribu halikuwapata ninyi isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu , ila
Mungu ni mwaminifu, ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja
na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea ili mweze kustahimili”. Basi Bwana
ajua kuwaokoa watauwa na majaribu na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu
hata siku ya hukumu. Malaika wa BWANA hufanya kituo akiwazungukia wamchao na
kuwaokoa na yule mwovu .Tunalindwa na nguvu ya Mungu ambaye pia aweza kukilinda
kile tulichokiweka amana kwake hata siku ile ya mwisho .Basi tuseme nini juu ya
hayo? Mungu akiwapo upande wetu , ni nani aliye juu yetu (Warumi 8:31) . Bwana
wetu Yesu Kristo hutulinda na hutuombea ulinzi kwa Mungu.Yohana 17:11,12,15 “
Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini uwalinde hawa ili wawe na umoja kama
sisi tulivyo. Nami naja kwako Baba Mtakatifu kwa jina lako ulilonipa.
Nilipokuwa pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza,
wala hapana mmoja wapo wao aliyepotea, ile yule mwana wa upotevu, ili andiko
litimie .Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu , bali uwalinde na yule
nwovu. “ Mungu pamoja na kulinda roho zetu anailinda miili yetu kutokana na
maadui zetu, hatari na ajali mbalimbali. Isaya 354:15 “ Tazama, yamkini
watakusanyana lakini si kwa shauri langu.Watu wowote watakaokusanyana juu yako
wataanguka kwa ajili yako “ Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako
kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa
njia saba(kumb. Torati 28:7) .Yeye atalinda miguu ya watakatifu wake, bali
waovu watanyamazishwa gizani, maana kwa nguvu hakuna atakayeshinda ,
washindanao na BWANA watapondwa kabisa.Yeremia 1:19 “ Nao watapigana nawe lakini
hawatakushinda ; maana mimi nipo pamoja nawe aseme BWANA , ili nikuokoe”. Mungu
anatuahidi kuwa tukimpenda na kuliinua jina lake tukamwita ataitikia na atakuwa
pamoja nasi taabuni, atatuokoa na kutuweka palipo juu.Mabaya hayatakupata wewe,
kwa kuwa atakuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote .Mikononi
mwako watakuchukua, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe (Zaburi 91:10-15)
.Kwa siku nyingi nitamshibisha , nami nitamwonyesha wokovu wangu. Isaya 49:10
“ Hawataona njaa wala hawataona kiu; hari haitawapiga wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemichemi za maji atawaongoza”. Hatutaona njaa wala kiu kamwe kwa kuwa Yesu Kristo Bwana wetu anacho chakula cha uzima Yohana 6:35 “ Yesu akawaambia , mimi ndimi chakula cha uzima , yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe”. Mungu anatuahidi kutulinda na hatari za wanyama na wadudu wakali tukimwamini na kumtegemea yeye. Zaburi 91:13 “ Utawakanyaga simba na nyoka , mwana samba na joka utawaseta kwa miguu”. Hutaogopa hofu ya usiku wala mshale urukao mchana .Luka 10:19 “ Tazama , nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za yule adui , wala hakuna kitu kitakachowadhuru” Amri hii inatupa uwezo na mamlaka ya kumpinga na kumkanyaga shetani pamoja na mapando yake yote.Jambo lolote linalofunga na kuzuia baraka na mafanikio yako unayo mamlaka ya kulikanyaga chini ya miguu yako nalo lisiibuke na kudhuru maisha yako iwe ugonjwa , umaskini, utasa na kila aina ya pando ambalo shetani amelipanda katika maisha yako.Wakati mwingine pando la shetani linakuwa juu ya mali zako kama alivyofanya kwa mtumishi wa Mungu Ayubu .Ayubu alipoteza watoto na mali zake nyingi lakini hakumkufuru BWANA na BWANA akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza Kumbukumbu la Torati 28:4 “ Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wan chi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo , maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo zako”. Ukimcha Mungu kwa moyo wako wote atalinda nyumba yako na mashamba yako. Zaburi 127:1 “ Bwana asipoienga nyumba wajengao wafanya kazi bure. BWANA asipoulinda mji yeye aulindaye akesha bure”. Shamba lako BWANA atalilinda na kulitia maji kila dakika asiye mtu akaliharibu ; usiku na mchana atalilinda (Isaya 27:3). Yoeli 2:23-27 “ Furahini basi , enyi wana Sayuni mkamfurahie BWANA, Mungu wenu kwa kuwa yeye huwapa ninyi mvua ya masika kwa kipimo cha haki, naye huwanyeshea mvua, mvua ya masika na mvua ya vuli, kama kwanza na sakafu za kupepeta zitajaa ngano na mashinikizo yatafurika kwa divai na mafuta.Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu , na tunutu, jeshi langu kubwa nililolituma kati yenu.Nanyi mtakula chakula tele na kushiba , na kulihimidi jina la BWANA , Mungu wenu” Na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA , Mungu wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani . Litabarikiwa kapu lako na chombo chako cha kukandia unga. Utabarikiwa uingiapo na utokapo (Kumb la Torati 28:2,3,5,6).Mungu katika neno lake takatifu ametuahidi utajiri na mafanikio ikiwa tutaenenda katika uchaji wa neno lake ,tukizishika amri , maagizo na mausia yake.Kumbukumbu la Torati 15:4-5. “ Lakini hawatakuwepo masikini kwenu; (kwa kuwa BWANA atawabarikia kweli katika nchi akupayo BWANA , Mungu wako, uimiliki, iwe urithi wako) kwamba utaisikiliza tu kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako , uyatunze maagizo haya yote nikuagizayo leo kufanya”. Mungu katika Yoshua 1:7-8 alimwahidi mtumishi wake Yoshua mwana wa Nuni kuwa akitenda sawa sawa na sheria ya Mungu atafanikiwa sana kila aendapo maana ndipo atakapofanikisha njia yake, kisha ndipo atakapostawi sana kwa kuwa BWANA , Mungu wake atakuwa pamoja naye kila aendako .Neno la Mungu linasema kuwa heri mtu yule ambaye hakusimama katika njia ya wakosaji bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo .Zaburi 1:3 “ Naye atakuwa kama mti uliopandwa kando kando ya vijito vya maji , uzao wa matunda yake kwa majira yake, wala jani lake halinyauki na kila alitendalo litafanikiwa”. Bwana wetu Yesu Kristo anasema kuwa yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao . 2 Wakorintho 8:9 “ Maana mmejua neema ya Bwana wetu YESU Kristo , jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu , Ingawa alikuwa tajiri ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umasikini wake”. Mungu atatujaza kila kitu tunachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu , ndani ya Kristo Yesu .Tukumbuke kuwa vitu vyote yeye ndiye aliyeviumba na ni mali yake naye humpa mtu atakavyo kwa ajili ya utukufu wake. Bwana wa majeshi anatuahidi ya kuwa tutakuwa nchi ya kupendeza sana na yenye heri na baraka tele ikiwa tutamtolea zaka kamili.Malaki 3:10-11 “ Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwepo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye , wala hataharibu mazao ya ardhi yenu, wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wala katika mashamba , asema BWANA wa majeshi” . Mungu anapokubariki hivi shetani anaweza kuleta pando la ugonjwa au maradhi ili usiweze kufurahia baraka hizi za Mungu.Tuangalie ahadi za Mungu kuhusu afya njema , ugonjwa na tiba ili tuweze kumwomba Mungu sawaswa na mapenzi yake tukimkumbusha ahadi hizo.Na itakuwa utakapozisikiliza amri na sheria za Mungu na kuzishika na kuzitenda , basi BWANA Mungu wako atakurehemu na kukupa afya njema.Kumbukumbu la Torati 7:15 “ Na BWANA atakuondolea ugonjwa wote, wala hatatia juu yako maradhi yoyote mabaya uyajuayo ya Misri, Lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao”. Mungu anasema hatatia juu yako maradhi yoyote aliyowatia Wamisiri, kwa kuwa yeye ndiye BWANA akuponyaye.Mabaya hayatakupata wewe wala tauni iharibuyo haitaikaribia hema yako, kwa kuwa atakuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako. Zaburi 103:3 “ Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote, aukomboa uhai wako na kaburi, akutia taji ya fadhili na rehema”. Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako , asema BWANA, kwa sababu wamekuita , mwenye kutupwa, wakisema ni Sayuni ambao hapana mtu autakaye (Yeremia 30:17). Katika Agano Jipya kuna ahadi nyingi za Bwana wetu Yesu Kristo kuhusu afya njema, uponyaji wa maradhi au magonjwa na uponyaji wa hayo yote kwa kuwa mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu .Mathayo 9:35 “ Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao , na kuihubiri habari njema ya ufalme , na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali , akatoa pepo wengi hakuwaacha pepo kunena kwa sababu walimjua (Marko 1:34) .Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao na misiba na pepo wabaya na vipofu wengi aliwakirimia kuona, viwete wakatembea wenye ukoma wakatakasika , viziwi wakasikia, wafu wakafufuliwa, masikini wakahubiriwa habari njema (Luka 7:21-22) .Bwana Yesu ametutuma kwenda kwenye miji na vijiji kuwaponya wagonjwa waliomo na kuwahubiria juu ya ufalme wa Mungu kuwa umewakaribia .Bwana wetu Yesu Kristo ametuahidi kuwa wale wamwaminio wataweka mikono yao juu ya wagonjwa nao watapata afya (Marko 16;18 ). Mtu wa kwenu amekuwa hawezi ? na awaite wazee wa kanisa, nao wamwombee na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule , na Bwana atamwinua hata ikiwa amefanya dhambi , atasamehewa (Yakobo 5:14-15). Katika Yohana Mtakatifu 14:12 Bwana wetu Yesu Kristo anasema “ Amini amini nawaambieni, yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi yeye naye atazifanya, naam na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba” Mungu Baba wa Mbinguni atakuwa pamoja na wateule wake nao watakuwa watu wake. Ufuno. 21:4 “ Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwepo tena , wala maombolezo , wala kilio wala maumivu hayatakuwepo tena, kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita “ Tazama atayafanya yote kuwa mapya. Ili mambo yote yawe mapya tunatakiwa kuomba kwa bidii na juhudi nyingi ; tukidumu katika maombi na sala bila kuchoka wala kukata tamaa.