MATHAYO MTAKATIFU 6:25-26 “Kwa sababu hiyo nawaambieni, msisimbukie maisha yenu,mle nini au mnywe nini, wala miili yenu, mvae nini.Maisha je? Si zaidi ya chakula, mwili zaidi ya mavazi. Waangalieni ndege wa angani ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kuliko hao.”
Ili tuweze kuyafahamu vizuri mafundisho haya ya Bwana wetu Yesu Kristo ni vyema tukaanzia mstari ule wa 24 unaosema, “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu. Hamuwezi kumtumikia Mungu na mali.” Haya ni mafundisho ya Bwana Yesu Kristo yeye mwenyewe anayotufundisha kuhusu kumtumikia Mungu au mali.Mabwana hawa wawili ni Bwana Mungu na bwana mali. Katika biblia ya kiingereza neno hili mali limeitwa “Mammon” kwa maana nyingine ni roho wa ibilisi anayetawala mali. Roho huyu wa ibilisi amewakamata watu wengi wanaopenda mali ya haraka haraka. Wamekwenda kwa shetani kutoa sadaka ili kupata mali au fedha. Fedha ni mali na mali ikiwa nyingi ni utajiri na aliye na mali hiyo anaitwa tajiri. Wapenda fedha wengi wanatafuta fedha ili wawe matajiri waishi maisha ya kula na kunywa kwa anasa na wavae vitani safi na kuishi maisha ya ufahari hapa duniani. Katika somo hili hatuongelei matajiri tu bali mtu yoyote mwenye fedha ambaye ameweka moyo wake juu ya bwana fedha kwa maana nyingine ameweka tegemeeo na tumaini lake kwenye mali aliyonayo.Mtu wa aina hii ni mtumishi wa bwana fedha/mali na hataweza kumtumikia Bwana Mungu kwa kuwa hataweza kutumikia mabwana wawili.
Luka 16:13 “Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana , ama atamdharau huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu namali. “Mtumishi anayemtukia shetani atamdharau Mungu na kumsahau, atajenga tabia ya kujisifu na kuwa na kiburi. Katika Agano la Kale, katika nyakati mbalimbali wana wa Israel walipopata vitu wakala, wakanywa na kushiba walimsahau Mungu. Wakamsahau Mungu, Mwokozi wao aliyetenda mambo makuu na ya ajabu katika maisha yao. Kumbukumbu ya Torati 8:11-14 “Jihadharani, usije ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng’ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulichonacho kitapoongezeka, basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako,aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. “Mstari ule wa 17 -18 “hapo usiseme moyoni mwako nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulimpatia utajiri huo bali utamkumbuka Bwana Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri.” Wana wa Israel walipomdharau Mungu na kumsahau na kuiandama miungu mingine na kuitumikia na kuiabudu Mungu aliwaangamiza bila shaka yeyote. Watu wanaotumikia mali wana shida nyingine ya kujisifu wakati neno la Mungu linatutaka tujisifu kwa Bwana kwa sababu tunamfahamu na tena tunaye. Ufunuo 3:17 “kwa kuwa wasema, mimi ni tajiri,nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe umnyonge, na mwenye mashaka, na masikin, na kipofu na uchi”. Mungu huwaita wapumbavu na wajinga hao wanazozitumainia mali zao, na kujisifia wingi wa utajiri wao. Mpumbavu na mjinga hupotea pamoja, na kuwaachia wengine mali zao. Makaburi ni nyumba zao hata milele, maskani zao vizazi hata vizazi. Zaburi 49:16 “Usiogope mtu atakapopata utajiri, na fahari ya nyumba yake itakapozidi maana atakapokufa hatachukua chochote.” Biblia ina mfano wa tajiri mmoja mpumbavu ambaye alijikusanyia utajiri mwingi naye akaimbia nafsi yake una vitu vyema vingi pumzika ule, unywe, ufurahi. Luka 12:16-21 “Akawambia mithali, akisema, shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwaka, akisema, nifanyaje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha nitajiambia, Ee nafsi yangu una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwimbia,mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba,asijitajirishe kwa Mungu.“Mungu hamwezeshi kula hiyo mali kwa sababu nafsi yake haikushiba mema. Neno la Mungu linasema hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, zitawatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la ubaya wa kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakitamani hiyo wamefarakana na imani, na kujichoma kwa maumivu mengi (1Timotheo 6:9-10). Matajiri wanaomtumikia bwana mali/fedha wana mashaka mengi juu ya maisha yao wanaweka akiba wakidhani itawasaidia siku za mwisho. Katika Waraka wa Yakobo 5: 1-3 Neno la Mungu linasema, “Haya basi enyi matajiri, lieni mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mnajiwekea akiba katika siku za mwisho. Mstari ule wa tano unasema, “mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tama mmejilisha mioyo yenu kama siku za machinjio.” Haya ni matokeo mabaya kwa wale wote wanaosumbukia maisha yao, wale nini au wanywe nini au wavae nini bila ya kumtanguliza Mungu.Wanapenda fedha na mali na anasa au tama za ulimwengu huu, ndiyo maana neno la Mungu linasema huwezi kuwapenda mabwana wawili bila ya upendeleo wowote kwa maana utamchukia huyu na kumpenda huyu. Neno la Mungu linatutaka kumpenda Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote ;na jirani kama nafsi yako (Luka 10;27).Yesu Kristo anathibitisha maneno haya kwa kijana mmoja alipomwendea akamwambia, mwalimu nitende jambo gani jema ili nipate uzima wa milele? Mathayo 19:21-22. “Yesu akamwambia ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo uwape masikini, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate. Yule kijana aliposikia neno lile akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi”. Kwa kujua mambo yote haya ndiyo maana Bwana Yesu akasema kuwa itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni. Mathayo 19:23-24 “Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amini, nawaambieni, ya kwamba itakua shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni. Nawaambia tena, ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. “Bwana Yesu hasemi kuwa hawezi kuingia, anachosema ni kwamba itakua shida kwa sababu anavyo vikwako vingi vya kuvuka kama tulivyoviona katika somo hili. Katika sehemu hii ya pili ya somo hili tuangalie mambo yatapasayo kufahamu kuhusu mali na utajiri ili tuweze kurithi ufalme wa Mungu, tupate uzima wa milele.
Tunatakiwa tufahamu ya kwamba nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakao ndani yake (zaburi 24:1) . Neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai 2:8 “ Fedha ni mali yangu , na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi.” Mungu ametupa mamlaka ya kutiisha na kutawala vitu vyote alivyoviumba. Sisi ni mawakili wa siri za Mungu na tutatoa hesabu ya uwakili wetu. Mungu ametupa mamlaka ya kutumia vitu vyote kwa ajili ya utukufu wake, kwa maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyake na ufalme ni wake. 1 Mambo ya Nyakati 29:12 “Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. “ Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha sawa sawa na mapenzi yake.
Humpa mtu kama apendavyo yeye humdhili huyu na kumwinua huyu kwa utukufu wake. Kama tunakiri kuwa Mungu ndiye mwenye mali na ndiye mwenye mamlaka na nguvu ya kumpa mtu ni kwa nini tunasumbukia maisha yetu namna hii tule nini, tunywe nini na tuvae nini wakati Bwana Mungu wetu anafahamu mahitaji yetu yote na tena anajishughulisha na mambo yetu?
Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Basi mlapo au mnwapo, au mtendapo neno lolote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu. Wakolosai 3:17 “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye. “Nawe utakapo kula ukashiba unatakiwa umshukuru Mungu wako. Jina la Yesu ni kubwa zaidi ya fedha na dhahabu ndiyo maana mtume Petro alipoombwa sadaka na yule kiwete alisema, “Mimi sina fedha, wale dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. “Yule kiwete akasimama akaenda zake kwa kuwa jina la Yesu limemtia nguvu. Mungu hatatupungukia wala hatatuacha tukimtwika fadhaa zetu. Yeye ni mwaminifu na wa haki tukimtumainia na kumtegemea yeye na kuishi maisha ya utulivu, na amani katika utauwa wote na ustahivu. Wakolosai 4:13 “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Kwa kuwa pasipo yeye sisi hatuwezi kufanya neno lolote. Tujifunze kuwa radhi na hali yeyote ya maisha ambayo Mungu ametukirimia kwa upendo wake mkuu. 1 Timotheo 6: 6-8 “Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula nguo tutaridhika na vitu hivyo.”
Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa na ule utakaokuwepo baadaye. Mungu anapenda tuwe na mali tuliyoipata kwa haki kutoka kwake na tuitumie mali hiyo kumtumikia yeye na tumtumaini na kumtanguliza katika mambo yetu yote. Mathayo 6;33. “Bali utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”. Katika 1 Timotheo 6:17-19 kuna maagizo ya Mungu kwa matajiri, “Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune “Wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha. Watende wema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mazao, washirikiane na wengine kwa moyo, huku wakijiwekea akiba iwe msingi mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli “Utajiri wake Yesu Kristo usiopimika ni neema inayopatikana katika neno lake takatifu. Yesu Kristo mwenyewe anatufundisha yanayotupasa katika kutunza akiba zetu na hazina zetu.Mathayo Mtakatifu 6:19-21 “Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaitii, kwa kuwa hazina yako ilipo ndipo utakapokuwako na moyo wako.“Mali uzidipo usiiangalie sana moyoni mwako kwa kuwa mali hazifaidi kitu siku ya ghadhabu ya Mungu bali neno la Mungu na likae kwa wingi ndani yako. Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia zangu, neno lako ni bora kuliko maelfu ya dhahabu na fedha. Neno lako lasimama imara mbinguni hata milele.
Ni aina gani ya hazina tunayotakiwa kuweka mbinguni?
Hazina ni kitu cha thamani ambacho mtu anaweka kama akiba ya kutumia wakati ujao , wakati wa uhitaji .Watu wanaoweka hazina yao ulimwenguni wanaweka fedha , dhahabu, mashamba, nyumba, mifugo, watoto, ndugu, wazazi na vitu vingine vingi vya thamani kwao .Vitu hivyo vyote ni vile ambavyo vinaharibika, vinakufa, vinaliwa na kutu na nondo, vinaibiwa wala havidumu hata milele.Bwana Yesu katika somo hili anatufundisha tuweke hazina zetu mbinguni .Swali tunalojiuliza katika somo hili ni kuhusu aina gani ya hazina tunayotakiwa kuweka mbinguni? Tunaweza kuweka aina mbalimbali ya hazina mbinguni, katika somo hili tutatafakari aina chache za hazina hiyo, hii ni pamoja na; sadaka, kumtumikia Mungu, maombi, matendo ya upendo na huruma , imani na kumcha Mungu .Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha katika neno lake kuwa ukitoa sadaka kwa wahitaji unaweka hazina yako mbinguni .Matoleo yako kwa Mungu ni hazina yako mbinguni .Mfano mzuri wa fundisho hili tunaupata katika Luka 19:1-9 Zakayo mtoza ushuru aliyekuwa tajiri amesikia habari za Yesu na juu ya ufalme wa Mungu akawa tayari kutoa mali yake ili apate wokovu unaopaikana kwa kumwamini Yesu Kristo .
“Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, tazama Bwana nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.” Zakayo akatangaziwa wokovu na Bwana Yesu saa hiyo hiyo. Katika Luka 12:32-33 “ Msiogope enyi kundi dogo; kwa kuwa baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme, viuzeni mlivyo navyo , mtoe sadaka .Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu , mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu.Kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakuwapo na mioyo yenu.”
Sadaka nyingine inayompendeza Mungu ni ile unayotoa kwa ajili ya wahitaji na kwa ajili ya watakatifu. Luka 14:13-14 “ Bali ufanyapo karamu waite maskini ,vilema, viwete, vipofu nawe utakuwa heri , kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki. “Sadaka ya kuwapa watakatifu vitu ni harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu.Mtu mwingine ambaye sadaka yake ilikumbukwa mbinguni ni Kornelio aliyetoa sadaka kwa wahitaji Mungu akazikumbuka sadaka zake zote na kuzitakabali. Dhabihu zako sadaka yako haitakuwa bure. Tunao wahitaji wengi wanaotuzunguka, tukiwasaidia hawa tunaweka hazina yetu mbinguni .Hazina nyingine tunayoweza kuweka mbinguni ni kumtumikia Mungu katika kweli yote sawasawa na Neno lake. Tutumike wakati unaofaa hata wakati usiofaa yaani wakati wa maudhi na wa mateso tuidhihirishe kweli ya Mungu iliyo ndani ya Mwanae Yesu Kristo. Neno la Mungu katika Mathayo 5:11-12 linasema. “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo kwa ajili yangu .Furahini , na kushangilia; kwa kuwa dhawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.” 2 Wakoritho 4 : 7 “Lakin siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyoipokea kwa Bwana Yesu , kuishuhudia habari njema ya neema ya Mungu.” Ndugu zangu wapendwa katika Kristo Yesu, tuweke hazina zetu mbinguni kwa kujitahidi kwa bidii kuhubiri watu habari njema ya Bwana wetu Yesu Kristo , tupate kulilisha kanisa lake alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.
Marko 10:29-30 “Yesu akasema Amin, nawaambieni , hakuna mtu aliyeacha nyumba au ndugu waume au ndugu wake, au mama au baba au watoto au mashamba kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume na ndugu wake, na mama na watoto na mashamba pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.” Hazina ya mbinguni ijae maombi yako ukimkumbusha Mungu ahadi zake zinazopatikana katika Neno lake takatifu. Ili uwe na neno la kumkumbusha Mungu hakikisha ya kwamba Neno la Kristo limekaa kwa wingi ndani yako.Hazina yako ya mbinguni ijae imani yako katika Yesu Kristo Bwana wetu . Imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo , ni bayana ya mambo yasiyoonekana.Waraka wa Waebrania 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” Tuwe na imani katika Yesu Kristo kwa kuwa kushutumiwa kwake ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri. Tunapewa yote kwa imani na wote waaminio tunakombolewa kwa imani. Waefeso 2:8-9” Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo mtu awaye yote asije akajisifu.” Imani inatenda kazi pamoja na matendo mema na imani inakamilishwa kwa njia ya matendo.” Yakobo 2:14 “ Ndugu zangu , yafaa nini , mtu akisema ya kwamba anayo imani lakini hana matendo” Imani ya aina hii imekufa na haiwezi kuzaa matunda mema .Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa (Yakobo 2:26) . Hazina yako ya mbinguni ijae matendo ya upendo na huruma kwa watu wengine kama vile wagonjwa, wenye njaa na kiu , waliofungwa magerezani, walioko uchi na kupungukiwa na riziki .1Yohana 3:17-18. “ Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia , kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji , akamzuilia huruma zake, Je ! upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo”.Tusipoweka hazina yetu katika upendo na huruma Bwana wetu Yesu Kristo anasema hatuwezi kuingia katika ufalme wa milele. Mathayo 25:42 “Kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula, nalikuwa na kiu msininyweshe, nalikuwa mgeni msinikaribishe, nalikuwa uchi msinivike, nalikuwa mgonjwa na kifungoni, msije kunitazama.” Nao watamjibu Ni lini tulikuona tusikufanyie mambo yote hayo? Katika mstari wa 16 “Naye atawajibu akisema Amin, nawaambia kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi”. Hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele bali wenye haki walioweka hazina zao mbinguni watakwenda katika uzima wa milele.Ndugu zangu wapendwa katika Kristo Yesu natuweke hazina zetu mbinguni ambako haiwezi kuliwa, kuibiwa wala kuharibiwa kwa kuwa kule mbinguni imefichwa sirini chini ya ulizni wa Mungu mwenyewe ambaye ataitunza hata siku ya mwisho ya ukamilifu wa dahari.