MATHAYO 26:38-41
“Ndipo akahuzunika na kusononeka.Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa, kaeni hapa mkeshe pamoja nami. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke, walakini sikama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. Akawajia wale wanafunzi akawakuta wamelala, akawaambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja name hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu. Katika kitabu kile cha Luka 22:42 Bwana Yesu akapiga magoti akaomba akisema, Ee Baba ikiwa ni mapenzi yako uniondolee kikombe hiki walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. Katika somo hili kuna mambo mengi sana ya kujifunza lakini tutafakari mambo machache kati ya hayo. Tutajifunza juu ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo na kuwa mateso yanaweza kumpata muumini wa Yesu Kristo hata leo hii. Tutajifunza pia jinsi ya kuomba ili mapenzi ya Mungu yatimizwe kwetu. Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo yaliyomletea huzuni nyingi kiasi cha kufa yanatokana na mpango wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu na ulimwengu wote kutokana na uasi, kutotii amri za Mungu na kutenda dhambi. Mungu aliufunua mpango huu katika Yohana 3:16-17 “ Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu , hata akamtoa Mwanae pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu bali ulimwengu uokolewe katika yeye.” Katika mpango huo wa Mungu kuma hatua ya mateso na kifo msalabani. Bwana wetu Yesu Kristo alikuwa anaujua mpango huu wa Mungu. Marko 8:31 “Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi na kuuawa na baada ya siku ya tatu kufufuka”. Mungu aliwafunulia manabii wake kuhusu mpango huo na hatua hii ya mateso. Isaya 53:1-12.
Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa BWANA amefunuliwa nani? Maana alikuwa mbele zake kama mche mwororo, na kama mzizi katika nchi kavu, yeye hana umbo wala uzuri; na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni, nyingi, ajuaye sikitiko; na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, amejitwika huzuni zetu; lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa , amepigwa na Mungu na kuteswa, bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu; adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake na kwa kupigwa kwake sisi tumepona , sisi sote kama kondoo tumepotea, kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; na BWANA ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, wala hakufunua kinywa chake kama mwana - kondoo apelekwaye machinjioni, na kama vile kondoo anyamazavyo mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na n chi ya walio hai; alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya;na pamoja na matajiri katika kufa kwake; ingawa hakutenda jeuri, wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Lakini BWANA aliridhika kumchubua; amemhuzunisha utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, ataona uzao wake, ataishi siku nyingi na mapenzi ya BWANA yatafanikiwa mkononi mwake. Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake , na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao. Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa akahesabiwa pamoja na hao wakosao .Walakini alichukua dhambi za watu wengi , na kuwaombea wakosaji.
Unabii wa nabii Isaya ulitimia pale walipomtemea mate ya uso, wakampiga makonde, wengine wakampiga makofi, wakamdhihaki wakisema, Ewe Kristo tufumbulie, ni nani aliyekupiga. Wakafanya shauri juu ya Yesu wapate kumuua; wakamfunga wakamchukua, wakampeleke kwa Pilato aliyekuwa liwali. Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji ya miiba wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume, wakapiga magoti mbele yake wakamdhihaki, wakisema, salamu, Mfalme wa Wayahudi.Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi wakampiga – piga kichwani. Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake wakamchukua kumsulubisha. Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa – tikisa vichwa vyao, wakisema Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako, ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu shuka msalabani. Askari walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu lakini askari mojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki na mara ikatoka damu na maji. Bwana Yesu kando ya kuhuzunishwa na mateso haya alihuzunishwa na kusononeshwa na dhambi zetu ndipo Roho yake ikawa na huzuni nyingi kiasi cha kufa. Katika mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo tunajifunza kuvumilia hata mwisho na kuwasamehe watesi wetu kwa sababu hawajui watendalo. Tunatakiwa kufahamu kuwa waumini wa Yesu Kristo wanaweza kupata mateso katika utumishi wao. Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha kuwa mtu akitaka kumfuata hana budi ajitwike msalaba wake. Marko Mtakatifu 8:34-37“Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake akawaambia, mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injli, huyu ataisalimisha.Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake. Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake.” Msalaba kwetu ni alama ya ushindi kwa hiyo mateso yoyote yale yatakayotupata tutaibuka washindi katika Kristo Bwana wetu. Bwana wetu Yesu Kristo aliwatahadharisha wanafunzi wake juu ya mambo yatakayowatokea.Marko 13:9 “Nanyi jihadharini nafsi zenu maana watawapeleka ninyi mabarazani, na katika masinagogi mtapigwa; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao.” Mateso hayo yatatokea ili Injili ihubiriwe katika mataifa yote.Katika mstari ule wa 13 Bwana Yesu anasema, “Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu, lakini mwenye kusubiri hata mwisho, ndiye atakayeokoka.” Na watakapowachukua ninyi, na kuwasaliti msitafakari kwanza mtakayosema, lakini lolote mtakalopewa saa ile, lisemeni kwa maana si ninyi msemao bali ni Roho Mtakatifu.” Tutafakari matukio machache yanayo dhihirisha maneno haya ya Bwana wetu Yesu Kristo.
· Matendo ya Mitume 4:1-4 “Hata walipokuwa wakisema na watu wale, makuhani na akida wa hekalu na masadukayo wakawatokea, wakifadhaika sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri katika Yesu ufufuo wa wafu. Wakawakamata wakawaweka gerezani hata asubuhi, kwa kuwa imekwisha kuwa jioni.” Matokeo ya adha hiyo ni ushindi kwa kuwa wengi katika hao waliosikia lile neno waliamini, hesabu ya watu waume ikiwa kama elfu tano.
· Matendo ya Mitume 5:17-19, 29-42
“Akaondoka kuhani mkuu na wote waliokuwa pamoja naye, wamejaa wivu, wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza. “Ushindi ulipatikana pale malaika wa Bwana alipofungua milango ya gereza usiku akawatoa akasema, enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya uzima huu. Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni wakaanza kufundisha. Watu wakashangaa kuwakuta hekaluni wakifundisha, mtu mmoja akaenda akawapasha habari jemedari wa hekalu na wakuu wa makuhani. Ndipo walipowaleta wakawaweka katika baraza, wakawakataza wasifundishe kwa jina la Yesu. Mstari wa 29 “Petro na mitume wakajibu, wakisema, imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.” Wakawapiga wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao. Mateso haya yakaleta ushindi , nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya jina la Yesu. Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo.
· Matendo ya Mitume 6:8 -15, 7:54 – 60. Hii ni habari ya mtumishi wa Mungu aitwaye Stefano ambaye alikuwa amejaa hekima, neema, uwezo na Roho Mtakatifu akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu, akifundisha juu ya habari njema katika Yesu Kristo. Waliposikia maneno hayo wakachomwa mioyo, wakamsagia meno, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa nje ya mji wakampiga kwa mawe mpaka akalala (akafariki). Mateso ya Stephano yalileta ushindi mkubwa, Matendo ya Mitume 7: 56 “Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu.”
· Matendo ya Mitume 12:1-3
“Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Akamwua Yakobo ndugu yake Yohana, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika Petro”. Akamfunga minyororo na kumweka chini ya ulinzi mkali akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu. Ushindi ulipatikana malaika wa Mungu alipomtokea akafungua minyororo yake, akafungue na milango ya gereza na Petro akatoka na neno la Bwana likazidi na kuenea.
· Matendo ya Mitume 16:19-40
Habari hii inawahusu watumishi wa Mungu Paulo na Sila walipomtoa pepo kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi. Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila mpaka kwa wakuu wa mji na kwa makadhi wakiwashitaki kutangaza habari zisizokuwa halali kwa Warumi.Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora .Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wake watupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. Paulo na sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Katika mateso haya ushindi ulipatikana pale ghafla lilipotokea tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. Naye mlinzi wa gereza pamoja na wetu wa nyumbani mwake wakimwamini Bwana Yesu wakabatizwa na kuokoka.Paulo na Sila wakaachiwa huru wakaendelea kuhubiri juu ya Bwana wetu Yesu Kristo kuteswa na kufufuka katika wafu. Matendo ya Mitume 17:4 “Wengine miongoni mwao wakaamini, wakashikamana na Paulo na Sila; na Wayunani waliomcha Mungu, wengi sana, na wanawake wenye cheo si wachache”. Hivi ndivo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda nguvu.Kwa hiyo wote tunaomtumikia Mungu tunatakiwa kujua kuwa kando ya mateso tutakayopata kuna ushindi mbele yake. Tuwe tayari kushuhudia habari za Bwana Yesu Kristo kwa ujasiri mwingi bila ya aibu yoyote. Neno la Bwana katika Marko 8:38. “Maana kila atakayenionea haya mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu”. Wakati wa mateso tusisahau kuwaaombea watesi wetu kama Bwana wetu Yesu Kristo alivyofanya pale msalabani. Luka Mtakatifu 23:34 “Yesu akasema Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.” Mtumishi wa Mungu Stefano alipopigwa kwa mawe hadi kufa alisema, Matendo 7:60 “Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana usiwahesabie dhambi hii. Akisha kusema haya akalala.” Msamaha ni nguvu ya ushindi na baada ya mateso tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya.
Katika sehemu hii ya pili ya somo letu tutatafakari jinsi ya kuomba ili mapenzi ya Mungu yatimizwe kwetu. Bwana wetu Yesu Kristo alikuwa anayajua mapenzi ya Mungu kuwa ni kukamilisha kazi ya ukombozi ambayo yeye mwenyewe alijitolea kuifanya. Yohana 4:34. “Yesu akawaambia, chakula changu ndicho hiki niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake.” Bwana Yesu alipowafundisha wanafunzi wake kusali akawaambia semeni hivi; Mathayo Mtakatifu 6:10 “Mapenzi yako yatimizwe hapa duniani kama huko Mbinguni” Ni mapenzi gani haya ambayo Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha tuyaombe yatimizwe kwetu. Mapenzi ya Mungu ni mengi sana lakini katika somo hili tutatafakari machache kati ya hayo. Ni mapenzi ya Mungu kuwa tuachane na dhambi na kuishi maisha matakatifu.1Petro 4:2-3.” Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani .Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa na ulevi na karamu za ulafi na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali. “Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana, kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi. Kila mmoja kwa kadiri alivyopokea karama, itumieni kwa kuhudumiana kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu.Waefeso 2:4-5 “Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu. Alituhuisha pamoja na Kristo, yaani tumeokolewa kwa neema.” Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya. 1Wathesalonike 4:2 “Maana hayo ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweka mwili wake katika utakatifu na heshima.”Maana Mungu hakutuitia uchafu, bali tuwe katika utakaso. Ni mapenzi ya Mungu kuwa tuenende ulimwenguni kote tukaihubiri Injili kwa watu wote na kuwabatiza katika jina la utatu Mtakatifu. Marko 16:15-16 2. Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini atahukumiwa.” Mathayo 28:19-20 “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote nilivyo waamuru ninyi, na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Ni mapenzi ya Mungu kuwa hawa wanaohubiriwa Injili waamini jina lake na Neno lake la wokovu na kumpokea Bwana Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yao. Yohana 1:13 “waliozaliwa si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUngu.”Waliozaliwa kwa mapenzi ya Mungu ni wale waliozaliwa mara ya pili. Mtu asipozaliwa mara ya pili hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapa mema, yaani wale walioitwa kwa kusudi lake. Mungu hutuwazia mambo mema tukimtumainia yeye wala si mambo mabaya. 1Wathesalonike 18 “Shukuruni Kwa kila jambo, maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu”. Neno la Mungu linatutaka kumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo, hali tunanyenyekea katika kicho cha Kristo. Ni mapenzi ya Mungu kuwa shukrani zetu ziambatane na maombi. 1 Timotheo 2:1-4 “ Basi kabla ya mambo yote nataka dua, na sala na maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani katika utauwa wote na ustahivu. Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.” Wakati wote tukimwomba Mungu mahitaji yetu ya kimwili na kiroho tukumbuke wakati wote kuruhusu mapenzi yake yatimizwe kwetu sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake. Tena nafsi yake ilitakalo ndilo afanyalo. Yohana 2:17 “Na dunia inapita pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.” Neno la Mungu linasema si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, ataingia katika ufalme wa mbinguni; bali yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni (Mathayo 7:21). Tunatakiwa tuyapokee na kuyafanya mapenzi ya Mungu kwa furaha mioyoni mwetu. Yeremia 15:16 “Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu, maana nimeitwa kwa jina lako, Ee BWANA, Mungu wa majeshi.” Furahini katika Bwana siku zote, na tena nasema, furahini. Amani ya Mungu ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.