MATHAYO 15:28 “ Ndipo Yesu akajibu , akamwambia , mama imani yako ni kubwa , na iwe kwako kama utakavyo .Akapona binti yake tangu saa ile.”
Katika somo hli tutajifunza mambo makuu mawili; moja ni nguvu ya imani na jambo la pili ni nguvu ya uponyaji ndani ya Yesu Kristo Bwana wetu.
Neno la Mungu katika Waebrania 11:1 linasema, “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo , ni bayana ya mambo yasiyoonekana.” Imani katika Yesu Kristo Bwana wetu ni jambo la muhimu sana kwa kila mkristo kwa sababu zifuatazo; tunapokea wokovu kwa imani, tunapokea majibu ya maombi yetu kwa imani, tunapokea Roho Mtakatifu kwa imani na tunapokea uponyaji kwa imani. Katika somo hili tutafakari zaidi nguvu ya imani katika uponyaji.
Kuna aina mbili za imani; imani ndogo , chache au haba na imani kubwa au timilifu .Imani ndogo ni ile inayoambatana na wasiwasi, hofu, woga, shaka na kusitasita. Mambo hayo ni maadui wa imani kwa kuwa imani ya namna hiyo aiwezi kuleta mafanikio yaliyotarajiwa .Imani kubwa au kuu ni kuwa na uhakikia wa kile unachotarajia kukipata.Kuwa na uhakika ni kutokuwa na mashaka au wasiwasi wowote kuhusu kupokea unachotarajia kukipata .Kuwa na uhakika ni kutokuwa na mashaka au wasiwasi wowote kuhusu kupokea unachotarajia .Imani hii kubwa au kuu ndiyo anayoihitaji Bwana wetu Yesu Kristo na ndiyo inayompendeza Mungu.Imani hii ndiyo yenye matokeo makubwa ya miujiza ya uponyaji na mingine mingi. Baada ya mafundisho hayo sasa tuangalie nguvu ya imani katika uponyaji . Na tazama mwanamke Mkananayo akatokea, akampazia sauti akisema, unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.Naye akamsujudia akisema Bwana nisaidie. Mama huyu amesikia juu ya uweza wa Bwana Yesu naye akamjia kwa unyenyekevu akamsujudia .Imani yake inaonekana kuwa kubwa pale Bwana Yesu aliyepomwambia si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Naye akajibu akasema, “Ndiyo Bwana , lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa Bwana zao.” Mama huyu anaamini kuwa makombo ya Bwana Yesu yanatosha kuleta uponyaji wa mwanae.Ndipo Yesu akajibu, akamwambia , Mama imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo.Akapona binti yake tangu saa ile (Mathayo 15:22-28). Mama huyu hakuwa na shaka moyoni mwake juu ya binti yake kupata uponyaji, aliamini kuwa atapokea na kweli akapokea .Marko 11:24 “ Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote myaombayo mkisali aminini kwamba mtapokea, nayo yatakuwa yenu”. Tuangalie tukio jingine linaloonyesha nguvu kubwa ya imani iletayo uponyaji katika Mathayo 8:8-10 .Hiki ni kisa cha akida mmoja huko Kapernaumu aliyemjia Yesu akimwomba amponye mtumishi wake ugonjwa wa kupooza. Yesu akamwambia nitakuja nimponye. Yule akida akamjibu, akasema , Bwana , mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona.Yesu aliposikia hayo akawaambia wale waliomfuata “Amin, nawaambieni, sijaona imani kubwa namna hii kwa yeyote katika Israeli. Naye Yesu akamwambia yule akida , nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona saa ile ile.” Katika Biblia Takataifu kuna watu wengi walioponywa kwa kadri ya imani zao.Hebu tuangalie tukio jingine linaloonyesha nguvu ya imani iletayo uponyaji; katika kitabu cha Marko Mtakatifu 2:3-6, 11-12 “Wakaja watu wakimletea mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wane.Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolalia yule mwenye kupooza. Naye Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Nakuambia, ondoka ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako.Mara akaondoka akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, namna hii hatujapata kuiona kamwe. Katika matukio haya matatu ya uponyaji tunajifunza kuwa imani ya mtu mwingine au watu wengine inaweza kumponya mtu. Imani ya wale waliombeba mgonjwa ina nguvu mbele ya Bwana wetu Yesu Kristo. Natujifunze kuwabeba wahitaji na kuwapeleka kwa Yesu wakapate uponyaji wa mwili na roho zao. Katika matukio haya tunajifunza kuwa imani huja kwa kusikia neno la Mungu . Watu hawa waliowaleta wagonjwa kwa Bwana Yesu walisikia habari zake, habari njema za ufalme wa Mungu na kazi ambazo alizifanya wakawa na imani kuwa Bwana Yesu anaweza kuponya wagonjwa ndio maana wakamjia kwa imani kubwa waliyopewa na Mungu.Warumi 12:3 “ Kwa maana kwa neema niliyopewa nawaambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia, bali awe na nia ya kiasi , kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani. “Kwa maana tumeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, ambayo hiyo haikutokana na nafsi zetu, ni kipawa cha Mungu. Tunaweza kuongeza kiwango chetu cha imani kwa kusikia na kutii habari njema kwa maana imani chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo .Wanafunzi wa Bwana Yesu walimwomba awaongezee imani.Luka 17:5-6 “ Mitume wakamwambia Bwana, tuongezee imani.Bwana akasema, kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, ng’oka ukapandwe baharini nao ungewatii.” Wanafunzi wa Yesu walionyesha pia kupungukiwa na imani waliposhindwa kumtoa pepo. Mathayo 17:18-20 “ Yesu akamkemea pepo naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akamwambia , kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin nawaambia , mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, ondoka hapa uende kule; nao utaondoka wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu .(Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga)!
Hatuna budi kumtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu.Wagalatia 2:20 “ Nimesulubiwa pamoja na Kristo , lakini ni hai wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu, na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu , ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu .”Katika Kristo Yesu kuna imani itendayo kazi kwa upendo kwa kuwa imani bila upendo si kitu. 1 Wakoritho 13:2 “Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. “ Imani inakuwa na nguvu pale inapoambatana na matendo mema kwa kuwa imani bila matendo imekufa. Yakobo 2:17, 26 “Vivyo hivyo imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake. Imani pasipo matendo haizai.Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa”.Pamoja na kumwomba Mungu atuongezee imani, tumwombe atupe roho ya upendo yenye kutenda matendo mema yanayompendeza yeye na wanadamu.