Marko Mtakatifu 6:47-48 “Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya bahari, na yeye yu peke yake katika nchi kavu. Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa mbiso, hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea, juu ya bahari, akataka kuwapatia.”
Habari hii ya Bwana Yesu kutembea juu ya bahari ya Galilaya na kutuliza dhoruba na upepo imeandikwa pia katika Injili ya Mathayo Mtakatifu 14:22-28 na Yohana Mtakatifu 6:16-21. Utakumbuka kuwa kuna wakati mwingine tena Bwana Yesu alikemea na kunyamazisha upepo baharini; Mathayo 8:23-24, Marko 4:35-41 na Luka 8:22-25. Katika muujiza wa kwanza kuna mambo mawili makubwa; moja ni Bwana Yesu kutembea juu ya bahari na la pili Bwana Yesu kutuliza dhoruba na upepo mkali baharini. Hii ni kati ya miujiza mingi aliyoifanya Bwana wetu Yesu Kristo kuonyesha uweza wake wa kudhibiti vitu vya asili kama vile bahari na upepo. Hata upepo na bahari vinamtii Yeye. Marko 4:41 “ Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana; Ninani huyu basi, hata upepo na bahari humtii.” Tunajifunza kuwa tukimtegemea Yesu Kristo kwa ukamilifu wote hatutaogopeshwa na jambo lolote lile. Yeye akiwa upande wetu na pamoja nasi tutashinda woga, hofu na mashaka wakati tukimfuata Bwana wetu Yesu Kristo. Zaburi 27:1 “ Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu nimwogope nani/ Bwana ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani? Katika habari hii tutafakari mambo mawili makubwa kama ifuatavyo;
· Upepo wako na dhoruba yako ni kitu gani?
· Ni mimi msiogope.
Katika maisha yetu hapa duniani tunakumbwa na matatizo ya kila aina ambayo yanatuvunja moyo na kutudhoofisha imani yetu kwa Mungu. Je, dhoruba yako na upepo anaokumbana nao ni nini? Umasikini, ugojwa, njaa, kukosa kazi, kuoa na kuolewa, mauti, hofu, woga.
Katika shida, matatizo na taabu yako usiviangalie vitu hivyo vinavyokusumbua bali muangalieni na mfuate Bwana Yesu anayekuja kwako kwa upendo na huruma nyingi naye hatakupita ikiwa utamwita. Yeremia 33:3 “Niite nami nitakuitikia, name nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua” Atakuja kukuokoa kwa njia ambayo hukutegemea kama alivyowaendea wanafunzi wake akitembea kwa miguu juu ya bahari. Akapanda mle chomboni walipo, upepo ukakoma, wakashangaa sana mioyoni mwao. Utamshangaa Bwana Yesu atakapokutoa katika shida na masumbuko na misukosuko yako. Je, itakapotokea kwako Bwana Yesu akakuokoa utasemaje? Wanafunzi wake wao walisema; Mathayo 14:33 “Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.” Unatakiwa kutambua na kumkubali Yesu Kristo kuwa ni mkombozi wa maisha yako naye ni Mwana-kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu. Matendo 4:12 “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” Aukuomba uhai wako na kaburi, akutia taji ya fadhili na rehema, akusamehe maovu yako yote, akuponya magojwa yako yote. Mkabidhi BWANA njia yako na kazi zako, na mawazo yako yatathibitika; pia umtumaini na kumtegemea naye atafanya. 1Petro 5:6-7 “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake, huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.” Jambo lolote linalokutaabisha usiogope kwa kuwa Bwana wetu Yesu Kristo yupo pamoja nawe Yesu anasema, Ni mimi msiogope. Mathayo 14:27 “Mara Yesu alinena akawaambia; Jipeni moyo ni mimi msiogope.” Bwana wetu Yesu Kristo anawataka wanafunzi wake wachangamke baada ya kuwaona wakipiga yowe kwa hofu na kufadhaika mioyoni mwao. Anawataka wajipe moyo na waweke tumaini lao, kwake kwa kuwa amekuja kuwaokoa. Bwana Yesu atakapokuja kukuokoa anaweza kujitambulishakama; mchungaji mwema, njia kweli na uzima, mzabibu wa kweli, ufufuo na uzima. Yesu akawaambia; Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.” Yohana 14:6 Yesu akawaambia; Mimi ndimi njia na kweli na uzima, mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi.” Yohana 15:1-2 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa, na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa.”Yohana 11:25” Yesu akawaambia; Mimi ndimi huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiaye mimi, ajapokufa, atakua anaishi, naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele.”Huyu ndiye Bwana wetu Yesu Kristo anayesema Ni mimi msiogope. Inasemekana kuwa neno usiogope katika Biblia takatifu limetajwa mara 365. Kwa maana nyingine kila siku iendayo kwa BWANA unaambiwa usiogope. Tujiulize swali kwa nini tusiogope? Isaya 41:10,13 “Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe, usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako, nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Kwa maana mimi, BWANA Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia; Usiogope Mimi nitakusaidia .” Zaburi 23:4 “Naam, nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya, kwa maana Wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji.” Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapo badilika nchi, ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari (Zaburi 46:1-2). Je, tumwogope nani? Luka 12:4-5 “Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuwao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi. Lakini nitawaonya amtakaye mwogopa; mwagopeni Yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uwezo wa kumtupa katika Jehanum, naam, nawaambia mwogopeni huyo.”Ukitaka kushinda woga, hofu na mashaka ili uweze kupata ujasiri na akili njema lazima uongozwe na Neno la Mungu kupitia Roho Mtakatifu wake. Maisha ya ujasiri na ushindi ni ya kumwamini Mungu na kumpenda kwa moyo wako wote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na mpende jirani yako kama nafsi yako. Kaa nyumbani mwa BWANA siku zote za maisha yako ukimtumaini na kumtegemea kwa kuwa yeye yupo pamoja nawe hata milele. Tito 2:13-14“Tukilitazama tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema. “Mungu alibariki neno lake likamzalie matunda mengi mema tena sana.