• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 13 Oct, 2023
  • Admin

MAOMBOLEZO 3; 22-26 “Ni huruma za BWANA kwamba hatuangamii, kwa kuwa rehema zake hazikomi. Ni mpya kila siku,asubuhi,uaminfu wako ni mkuu. BWANA ndiye fungu langu, husema nafsi yangu, kwa hiyo nitamtumaini yeye. BWANA ni mwema kwa hao wamngojeao, kwa hiyo nafsi imtafutayo. Ni vyema mtu autarajie wokovu wa BWANA na kumngojea kwa utulivu”.

Katika maombolezo ya nabii Yeremia tunajifunza mambo mengi katika neno hili lakini kwa leo tutaangalia mambo machache tu. Tunajifunza kwamba Mungu ni mwenye huruma na rehema nyingi kwetu na ndio maana hatuangamii. Huruma za Mungu ni mpya kila siku na hazikomi. Kila siku Mungu anatupa nafsi ya mwanzo mpya. Tunaweza kuanza upya kila siku kwa sababu ya upendo wake,huruma,rehema, na uaminifu wake kwetu. Mungu ni mwenye huruma ndio maana hatamtupa mtu hata milele. Maombolezo 3; 31-33. “Kwa kuwa BWANA hatamtupa mtu milele. Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu wala kuwahuzunisha”. BWANA Mungu ni mwingi wa rehema, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli. Zaburi 72; 13-14. “Atamhurumia aliye dhaifu na masikini, na nafsi za wahitaji ataziokoa. Atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimu,na damu yao ina thamani machoni pake”. Kama vile Baba awahurumiavyo watoto wake, ndivyo BWANA anavyo wahurumia wamchao. Bwana wetu Yesu Kristo ni mwenye huruma nyingi; aliwaonea huruma wagonjwa, wenye mapepo na wenye njaa naye aliwaponya na kuwalisha. Mathayo 9:36. “Na alipowaona makutano, aliwahurumia kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji”. Kama Mungu asingelikuwa mwingi wa rehema, mwenye huruma wanadamu tungeangamia kwa ajili ya uovu wetu. Tunatakiwa tujinyenyekeshe mbele za Mungu na kufanya toba ya kweli na kuomba huruma yake na rehema zake zikae juu yetu. Maombolezo 3:40-41. “Na tuchunguze njia zetu na kuzijaribu na kumrudia BWANA tena. Na tumwinulie Mungu aliye mbinguni mioyo yetu na mikono.” Mungu utusamehe kwa kuwa tumekosa na kuasi. Hapo ndipo tutakapouona uaminifu wake kwetu kwa kuwa anasema katika neno lake atatusamehe na kuzisahahu dhambi zetu. Mungu ni mwaminifu katika Neno lake tena anatimiza ahadi zake kwetu Kama BWANA alitimiza kila neno alilosema juu ya nyumba ya Israel, atatimiza hata kwako wewe amini na tembea kwa utii. Warumi 4:20-21“Lakini (Abrahamu) akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani , akimtukuza Mungu, huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale alivyoahidi”. Natulishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke, maana yeye aliyeahidi kutusamehe dhambi zetu ni mwaminifu. Isaya 1:18-20 “Haya, njoni tusemezane asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji, zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi, bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya. Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi na kutusafisha na udhalimu wote.

Tuhitimishe mafundisho haya kwa kuangalia watu wanaomngojea BWANA .BWANA ni mwema kwa hao wanaomtafuta na kumngojea kwa utulivu wakitarajia wokovu wa BWANA. Wakati Nabii Yeremia akiandika neno hili alikuwa anatoa unabii wa kuja kwa Bwana wetu Yesu Kristo.

Nabii Yeremia alitambua kuwa wokovu wetu unapatikana katika Yesu Kristo aichukuaye dhambi ya ulimwengu. Je wewe unaamini Neno hilo? Matendo 4:12 “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo”. Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi na Mwana Kondoo. Wamngojeao Bwana ni wale waliofua mavazi yao kwa damu ya Mwana Kondoo yakawa meupe kama sufu. Ni wale waliojaza taa zao mafuta wakimngojea Bwana Harusi atakapokuja mara ya pili kuwachukua kwenda mahali alipowaandalia makao ili alipo yeye nao wawepo pamoja naye. Yohana Mtakatifu 4:1-3 “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi, kama sivyo ningeliwaambia; maana naenda kuwaandalia, mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu, ili nilipo mimi nanyi muwepo. Katika Yohana 12:26 Bwana wetu Yesu Kristo anasema, “Mtu akinitumikia na anifuate, nami nilipo ndipo na mtumishi wangu atakapokuwepo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu”. Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja, wataaibika watendao uhaini bila sababu. Maana wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu nakungoja wewe mchana kutwa. Mwimba Zaburi 62:1-2 anasema, “Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya, wokovu wangu hutoka kwake. Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, ngome yangu, sitatikisika sana”. Tumngojee Bwana kwa utulivu bila kuchoka kwa kuwa Neno la Mungu linasema, Isaya 40:31 “Bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai, watapiga mbio wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia”. Umngojee Bwana, uwe hodari, upige moyo konde, naam umngojee Bwana. Mungu alibariki Neno lake na akubariki wewe unayemngojea . Amina.

Share This