Katika maisha ya kawaida mkulima akishindwa kutambua majira ya mvua atachelewa kuandaa shamba, kupanda na kupalilia. Madhara ya jambo hilo ni kukosa mavuno na kama ni shamba la miti ya matunda atakosa matunda, kipato na chakula na hivyo kuingia katika shida ya njaa yeye na watoto wake au familia yake. Jambo hili litamnyima furaha na amani kwa kuwa atakuwa katika mahangaiko makubwa. Vivyo hivyo katika ulimwengu wa roho, kosa la kutotambua majira ya kujiliwa kwako yana madhara kwako na kwa watu wako. Wakazi wa mji wa Yerusalemu walishindwa kujua majira ya kujiliiwa kwao, hawakujua pia yapasayo amani. Matokeo yake ni vita pande zote, vita vilivyoathiri wazazi wao na watoto wao na mali zao, hakuna jiwe lililobaki juu ya jiwe. Pamoja na kukosa amani ukishindwa kutambua majira ya kujiliwa kwako utashindwa kujua kusudi la Mungu katika maisha yako na kwa ajili hiyo utashindwa kumzalia BWANA tunda la Roho. Mungu analo kusudi katika kila mwanadamu aliyemuumba. Waefeso 1:11-12 “na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake. Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu.” Katika Biiblia takatifu tunayo mifano mingi ya watumishi wa Mungu ambao Mungu aliwachagua kufanya kusudi lake. Yeremia 1:10 “angalia nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung’oa, na kubomoa, na kuharibu na kuangamiza, ili kujenga na kupanda.” Usipojua kusudi la Mungu katika maisha yako utashindwa kumzalia BWANA tunda la Roho, tunda ambalo ndani yake kuna mbegu tisa. Wagalatia 5:22 “lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi, juu ya mambo kama hayo hakuna sheria." Ili tumzalie BWANA tunda la Roho hatuna budi kujazwa maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni utakaotuongoza kutambua wakati wa kujiliwa kwetu. Wakolosai 1:10-11 “ mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa BWANA, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha.” Ukifanya mapenzi ya Mungu utakuwa kama mti uliopandwa kando kando ya vijito vya maji, uzaao matunda yao kwa majira yake wala jani lake halinyauki, na kila ulitendalo utafanikiwa. Mji wa Yerusalemu ulishindwa kujua majira ya kujiliwa kwake kwa ajili ya ukombozi kwa sababu macho yao yalifichwa kuona neema ya Mungu. Unabii wa nabii Isaya ulitimia hapa. Yohana 12:40 “Amewapofusha macho, ameifanya mizito mioyo yao; wasije wakaona kwa macho yao;, wakafahamu kwa mioyo yao, wakaongoka, nikawaponya.” Jambo lililofichwa maana yake ni siri ambayo haijafunuliwa kama vile siku na saa ya mwisho wa dunia lakini ziko siri nyingi za Mungu ambazo zimefunuliwa kwetu kupitia neno lake na Mwanae Yesu Kristo. Kutoka 8:10 Bwana Yesu, “Akasema, ninyi mmepewa kuzijua siri za ufalme wa Mungu; bali wengine kwa mifano, ili wakiona wasione, na wakisikia wasielewe.” Bwana Yesu alifundisha siri za ufalme wa Mungu kwa mifano mblimbali kama vile mfano wa mpanzi aliyepanda mbegu, mbegu ni neno la Mungu (Marko 4:2-20). Akawatolea mfano mwingine, akisema, ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake, lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake (Mathayo 13:24). Akawatolea mifano mingine akafananisha ufalme wa Mbinguni na chachu aliyoitwaa mwanamke, na mwingine akafananisha ufalme wa Mbinguni na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake (Mathayo 13:31-33).
Marko 4:33-34 “ Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia, wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha. Siri za Mungu hujulikana kwa ufunuo kwa wale wanaomtii na kulishika neno lake. Luka 8:17 “kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitojulikana na kutokea wazi.” Mungu kwa kupitia Roho Mtakatifu wake huwafunulia watu siri za mbinguni kama inavyompendeza Yeye. Mambo mengine amewaficha wenye hekima na akili; akawafunulia watoto wachanga kwa kuwa ndivyo ilivyompendeza. Ili tuweze kujua siri za Mungu na maarifa ya Mungu hatuna budi kuwa na upendo (1 Wakorintho 13:1-8). Tumwombe Mungu atupe macho ya rohoni ili tuweze kutambua au kujua majira ya kujiliwa kwetu. Macho yangu yamtazame BWANA daima niuone uzuri wake na ukuu wake. Msaada wangu u katika BWANA, aliyezifanya mbingu na nchi.
Tuhitimishe somo hili kwa kutafakari jambo moja kubwa sana katika maisha yetu, tutafakari majira ya kurudi kwa BWANA wetu Yesu Kristo. Yohana 14:3 “Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi muwepo.”Ni kweli kuwa hatujui siku wala saa atakayo kuja Mwana wa Adamu lakini Mungu ametupa dalili ambazo tukiziona hizo tutatambua kuwa majira ya kujiliwa kwetu yamekaribia. Mathayo 24:3 “Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema tuambie mambo hayo yatakuwa lini? Yesu akajibu akawaambia; watakuja watu wakisema mimi ni Kristo nao watadanganya wengi, mtasikia habari za vita na matetesi ya vita, taifa litaondoka kupigana na taifa na ufalme kupigana na ufame, kutakuwa na njaa na matetemeko ya nchi mahali mahali. Hayo yote ndio mwanzo wa utungu. Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki nao watawaua, ninyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. Ndipo wengi watakapojikwaa nao watasalitiana na kuchukiana. Na manabii wengi wa uongo watatokea na kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapotea. Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakuja (Mathayo 24:3-14). Ni jambo la muhimu sana kutambua kuwa sisi tunaoishi wakati huu tunaishi katika majira ya kurudi kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Swali kubwa la kujiuliza ni tufanye maandalizi gani kwa ujio huu mkubwa ili Mwana wa Adamu atakapokuja atukuke atakuta tupo tayari. Yesu Kristo anatuonya kwamba tusije tukakubali kudanganywa na watakao jiita wao ni Kristo wala manabii wa uongo habari za vita na matetemeko visitutishe wala mateso na machukizo yatakayotokea kwa kuwa mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Neno la Mungu linatutaka tukeshe kwa kuwa hatujui siku wala saa. Mathayo 24:36 “walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna ajuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake.” Neno la msingi kwetu ni kukesha wakati tumeziweka taa zetu mafuta tayari kwa kumlaki Bwana harusi wetu. Tufue mavazi yetu kwa damu ya Mwana-kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu. Lakini sisi tunaokesha tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu. Ufunuo 3:11 “Naja upesi, shika sana ulichonacho, asije mtu akaitwaa taji yako.” Bwana wetu Yesu Kristo atusaidie tujue kuzihesabu siku zetu. Amina.