MADHABAHU
Katika Biblia tunasikia habari mbalimbali zinazoonyesha umuhimu wa kuwa na madhabahu pakiwa na mahali ambapo tunaweza tukapeleka mahitaji yetu na kuliitia jina la BWANA, na kuwasiliana na Mungu wetu aliye hai tukiwa bado humu duniani.Baadhi ni kama mifano michache ifuatayo;
Pale Ibrahimu alipoulizwa na Mungu kumtoa Isaka mwanawe kuwa sadaka ya kuteketezwa.Ee Ibrahimu umchukue mwanao mwana wako wa pekee umpendaye Isaka ukamtoe sadaka ya kutekelezwa huko juu ya mlima nitakaokuambia.Ibrahimu anaitii sauti ya Mungu na kuchukua hatua,tena inadhihirisha hata hakuweka jambo hili wazi kwa mkewe,na hata majaribu ya njiani toka kwa watumwa wake na kwa mwanawe mwenyewe.Anaulizwa maswali,moto upo,kuni zipo,kisu kipo lakini yuko wapi kondoo wa sakada? wa sadaka?Bado akajibu kwa unyenyekevu mkuu BWANA atajipatia mwana-kondoo.Alipofika mahali alipoambiwa na Mungu akaijenga madhabahu huko ili amchinje mwanawe kuwa sadaka.Na sauti ya Mungu inamjia kutoka madhabahuni ikimuita Ibrahim na kumshukuru kwa sadaka ile ‘Iwapo hukunizuilia mwanao wa pekee sasa nimejua ya kuwa unanipenda nawe usimtendee neno mwanao,akamwona mwana-kondoo mume yuko nyuma yake akamtwaa kuwa sadaka mahali pa mwanawe (Mwa.22:1-14) .Hali hii haikuwa njozi wala maono lakini ilikuwa ni sauti ya Mungu mwenyewe tena ya wazi inayodhihirisha kuwa MUNGU yuko mahali hapo.
Mahali pengine ilikuwa pale ambapo Yakobo alikuwa amelala usiku ndipo alipoota ndoto na tazama ngazi imesimamishwa juu ya nchi na ncha yake yafika mbinguni tena malaika wa Mungu wanapanda na kushuka juu yake.Na juu yake Mungu wa Ibrahimu na Isaka amesimama.Yakobo; anazinduka usingizini ndipo Mungu anapoweka agano akimwambia Yakobo.Nchi hii uilalayo nitakupa wewe na wanao,Uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi,na kwa ajili yako jamaa zote za dunia watabarikiwa, na jina lako hutaitwa Yakobo tena ila utaitwa Israeli.Ndipo Yakobo akasema kweli BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua’.Naye akaogopa sana na kusema,Mahali hapa panatisha kama nini,Bila shaka hapa ni nyumba ya Mungu,napo ndipo lango la mbinguni.Yakobo akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake akalisimamisha kama nguzo na kumimina Mafuta juu yake (Yakobo akajenga madhabahu) naye akaweka ahadi ya kumtolea BWANA sehemu ya kumi ya mapato yake.(Mwa. 28:16-22).Yakobo anashuhudia MUNGU yuko mahali hapa wala mimi sikujua.Ni kweli wako watu wengi hata leo hawajui kwamba Mungu yuko madhabahuni,na kwamba ni mahali ambapo mwanadamu huyapeleka mahitaji yake wakati wowote na kuwa mahali ambapo anakutana na Mungu wake (Mwa. 28.10-17) Baada ya Yakobo kutambua kuwa Mungu yupo hapo alijenga madhabahu na kufanya Agano na Mungu.Hii inaonyesha pia kuwa madhabahu ni mahali Mungu anapofanya Agano na mwanadamu.Na mar a zote Agano lilithibitishwa kwa kumwaga damu.Na Agano la kwanza likathibitika kwa kumwaga Damu ya kila mwanamume kwa njia ya tohara (Mwa. 17:10-14).Agano la Mungu na watu wake katika Misri usiku ule aliowapiga wazaliwa wa kwanza wa wamisri wa Israeli wanaokolewa kwa Damu ya kondoo wa pasaka (Kut.12:21-31).Na mara zote Musa alipohitaji kuwakumbusha Agano la Mungu Pamoja nao alitumia Damu (Kut:24:8).Baada ya agano la Damu za wanyama kutumika kwa muda wote Mungu anaahidi kufanya agano jipya na mwanadamu; Mungu mwenyewe anasema si kwa mfano wa agano lile la kwanza nililofanya na baba zao (Yer.31:31-34).
Agano jipya la Yesu mwenyewe anajiita Mwana kondoo wa Mungu.Anajinyenyekesha na kuwa mtii hata mauti,naam mauti ya msalaba .Na hivyo kutolewa kuwa fidia kwa dhambi zetu; kuwa sadaka ya kuteketezwa badala ya mafahali.Kalvari pale kwenye kilima cha Golgotha ndipo ilipo madhabahu kuu iliyopokea damu ya huyu Mwana kondoo wa Mungu sadaka hii ilitolewa mara moja tu na haitarudiwa.Ndipo mwana kondoo wa Mungu akatumia mazao ya ardhi ‘’Mkate (uwe mwili wake)na Divai (kikombe cha Agano jipya katika Damu yake)na likawa ni agizo n ahata sasa tunaendelea kuikumbuka na kuiadhimisha sadaka hii katika Sakramenti ya Chakula cha Bwana ‘’Fanyeni hivi kila mlapo na kila mnywapo kwa ukumbusho wangu’’.(Mt. 26:26-28;Mk.14:22-24;Ebr.13:20-21:1Kor.11:23-25).
Wakati huu tunayo majengo (Makanisa) na ndani yake yapo maeneo yaliyotengwa maalumu na kusimikwa msalaba na kupewa jina la Madhabahu;Tafsiri yake ikiwa ni kuonyesha mazingira ya kukumbuka kwamba yuko mmoja aliyetolewa mara moja tu kuwa fidia ya wote.Mara zote mahali hapo husogelewa kwa maombi na maombezi,sadaka, shukrani,na mahitaji ya watu ili yaguse damu ya huyu Mwana kondoo wa mungu kwa Imani(Uf.11:1).Nasi tunapaswa kuwafahamisha watu wetu kuwa huduma inayotolewa madhabahuni ni ya Mungu mwenyewe,Yesu Kristo akatoa angalizo la kuikaribisha Madhabahu kwani ni ya Mungu mwenyewe:Yesu Kristo akatoa angalizo la kuikaribisha Madhabahu kwa utakatifu (Mt.5:23-24).Na ni katika Madhabahu majibu ya haki kwa watu wa Mungu hupatikana (Uf.16:7).
Na nyumba yoyote inapotumika kutolea shukrani,sifa na utukufu kwa Mungu kwa njia ya Maombi na maombezi hata kama nyumba hiyo ni ya familia na wanaishi humo;kiroho nyuma hiyo imesimika madhabahu na mahali hapo Mungu yuko wala wao hawakujua.
Katika mafundisha mazuri ya Kikristo tunayofundisha wakristo wetu ni kwamba wawe na tabia ya kufanya maombi na mombezi wakati wote pamoja na familia zao wawapo nyumbani mwao.Wayajenge madhabahu ya MUNGU katikati ya familia zao nao watashuhudia Baraka za Mungu zitakazoenenda pamoja nao.