• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 05 Nov, 2023
  • Admin

-

Luka Mtakatifu 6:37-38 “Msihukumu nanyi hamtahukumiwa, msilaumu, nanyi hamtalaumiwa, achilieni; nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa, kipimo cha kujaa nakushindiliwa, na kusukwa –sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu.Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.”

Bwana Yesu asifiwe wapendwa. Tutatafakari neno hili la Mungu kupitia kwa Mtakatifu Luka chini ya vichwa vidogo vifuatavyo;

  • ·       Msihukumu nanyi hamtahukumiwa.
  • ·       Msilaumu nanyi hamtalaumiwa.
  • ·       Achilieni nanyi mtaachiliwa.
  • ·       Wapeni watu vitu nanyi mtapewa.

 Sehemu ya Kwanza: Msihukumu nanyi hamtahukumiwa.

Neno la Mungu linafundisha kuwa Mungu ana mamlaka na uhalali wa kuhukumu kwa kuwa Yeye ndiye aliyeumba vitu vyote vilivyopo mbinguni na duniani na hivi vyote ni mali yake. Zaburi 24;1”Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao ndani yake.”Mungu ndiye ahukumuye humdhili huyu  na kumwinua huyu; hakika yuko Mungu anayehukumu katika dunia. Mungu anahukumu kwa haki kwa kuwa yeye ni mtakatifu na hutenda kwa uadilifu na kwa rehema iliyo kuu.Mungu katika kitabu kile cha Mwanzo aliwahukumu kwa haki Adamu, Eva/ Hawa na nyoka/ shetani kwa kuvunja agizo lake la kutokula matunda ya mti wa mema na mabaya. Mungu anahukumu wenye dhambi lakini anawarehemu kwa neema yake iliyo kuu wenye haki wale wazishikao amri, sheria na mausia yake. Isaya 3; 10-11 “Waambieni wenye haki ya kuwa watakuwa heri, kwa maana watakula matunda ya matendo yao. Ole wake mtu mbaya, shari itakuwa kwake, kwa maana atapewa ijara ya mikono yake.” Mungu humpatiliza mtu mwovu na kumpa mwenye haki  haki yake, akimjalia kwa kadri ya haki yake. Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu, maagizo yake yote ni amini. Yamedhibitika milele na milele, yamefanywa katika kweli na adili (Zaburi 111:7-8). Najua ya kuwa hukumu zako niza haki na kuwa Wewe ndiye mwenye haki na adili katika kazi zako zote uzitendazo. Kazi zako ni kamilifu maana wewe ni Mungu wa uaminifu asiye na uovu wowote. Yeremia 32:18-19)”. Wewe uwarehemuye watu elfu nyingi, uwalipaye baba za watu uovu wao vifuani mwa watoto wao baada yao; Mungu aliye mkuu, aliye hodari, Bwana wa majeshi ndilo jina lake. Mkuu wa mashauri, mweza katika kutenda, ambaye macho yake yamefumbuka juu ya njia zote za wanadamu, kumpa kila mtu kwa kadiri ya matunda ya matendo yake.”Unahukumu kila mtu sawasawa na kustahili kwake ili kila mtu ajue ya kuwa wewe ndiwe BWANA. Mungu katika Agano la kale aliwahukumu wana wa Israeli kulingana na uovu wao na aliwarehemu na kuwaonea huruma walipotubu dhambi zao. Hata leo hii Mungu anawahukumu wale wote watendao dhambi kwa kuwa dhambi ni chukizo mbele ya Mungu na mshahara wa dhambi ni mauti. Sasa tutapataje kuponya? Yohana 3:16-18 “ Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanae pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili haukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi, asiyemwamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.” Sisi Je? Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitshwa kwetu na wale waliosikia. Huyu ndiye Bwana anayetuambia; Msihukumu nanyi mtahukumiwa au Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi. Ikiwa yeye mwenyewe hakutumwa kuja kuhukumu ulimwengu sisi tulio wake tunapata wapi uhalali na nguvu ya kuhukumu wenzetu? Au wengine? Wakati sisi ni wenye dhambi wala haki haimo ndani mwetu. Warumi 3:23 “Kwa sababu wote wamefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.” Mtu akisema hana dhambi anajidanganya mwenyewe wala kweli haimo ndani yake. Yohana 8:3-5, 9-11 “Waandishi na mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamkehuyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii, nawe wasemaje? Nao walipozidi kumhoji alijiinua akawaambia , yeye asiye na dhambi miongoni mwenu awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Nao waliposikia wakashitakiwa na dhamira zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao, akabaki Yesu pekee, na yule mwanamke amesimama katikati. Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, mwanamke wako wapi wale washitaki wako? Je, hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, hakuna Bwana. Yesu akamwambia, wala mimi sikuhukumu. Enenda zako wala usitende dhambi tena.” Yesu akasema, Ninyi mwahukumu kwa kufuata mambo ya mwilini; mimi simhukumu mtu. Yohana 12:47 Yesu Kristo Mwana wa Mungu anasema, “Na mtu akiyasikia maneno yangu asiyashike,mimi simhukumu, maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu,” Ikiwa Bwana wetu Yesu Kristo hakuja kuhukumu ulimwengu wewe unayehukumu huna udhuru. Warumi 2:1-3 “Kwa hiyo wewe mtu uwaye yote uhukumuye, huna udhuru, kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia, kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale. Nasi twajua ya kuwa hukumu ya Mungu ni ya  kweli juu yao wafanyao hayo. Wewe binadamu uwahukumuye wale wafanyao hayo na kutenda hayo hayo mwenyewe, Je! wadhani ya kwamba utajiepusha na hukumu ya Mungu?” Basi tusizidi  kuhukumiana,bali afadhali toeni hukumu hii, mtu asitie kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha (Warumi 14:13). Tunakosa uhalali wa kuhukumu wengine kwa kuwa tuna dhambi kama hao tunaotaka kuwahukumu. Warumi 14:10 “lakini wewe Je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. “Bwana wetu Yesu Kristo akawaambia mithali hii katika Luka 6:39,41-42. “Akawaambia mithali, Je? Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili ? Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho lake,  nawe huangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako, mwenyewe huiangalii? Au utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lake, nawe huangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ili boriti katika jicho lako mwenyewe ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichopo katika jicho la ndugu yako. Katika neno hili tunajifunza kuwa usihukumu dhambi ya mwenzako wakati wewe mwenyewe hujatubu dhambi zako. Hili linakunyima uhalali wa kuhukumu, kwa kuwa wewe ni kipofu unayejaribu kumwongoza kipofu mwenzako. Wote wawili mtatumbukia katika dhambi kwa maana hakuna hata mmoja wenu mwenye hekima, awezaje kukata maneno ya ndugu yake. Neno la Mungu linatutahadharisha kwamba tusihukumu kwa kuwa hatujui kuhukumu ipasavyo; kuna hatari kubwa ya kupotosha hukumu kwa kuwa sisi tunaangalia vya mwilini na hatujui kuchunguza mioyo. Mungu peke yake ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Katika Biblia takatifu tunayo mifano mingi ya watu waliopotosha hukumu wakawahukumu kifo mitume, manabii na watumishi wa Mungu kama vile Stefano na Yohana Mbatizaji. Wengine wakawatesa na wakawapiga viboko na kuwafunga magerezani bila hatia yoyote. Bwana wetu Yesu Kristo pamoja na Pilato kumwona kuwa hana hatia alihukumiwa kifo cha msalaba. Kumbukumbu la Torati 16:19 “Usipotoe maamuzi wala usipendelee uso wa mtu, wala usitwae rushwa; kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya wenye akili na kugeuza daawa ya wenye haki. “Neno la Mungu linasema, usipotoe hukumu ya mtu maskini katika neno lake, wala usipotoshe hukumu ya mjane, wala ya yatima, wala usitwae mavazi ya mjane yawe rehani. Mioyo yetu imejaa hukumu na visasi wakati neno la Mungu linatutaka kukaripia,kuonyana kwa upole, saburi na nyimbo na kusameheana. Yohana 3:10 “Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru matendo yake yasije yakakemewa.” Lakini yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila kilichodhihirishwa ni nuru. 2 Timotheo 3:16-17 “ Kila andiko lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili , amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” 1 Wathesalonike 5: 14-15 “ Ndugu twawasihi waonyeni wale wasiokaa kwa utaratibu, watieni moyo walio dhaifu, watieni nguvu wanyonge, vumilieni na watu wote. Angalieni mtu awaye yoyote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote lifuateni lililo ema, nyinyi kwa nyinyi na kwa watuwote.” Pamoja na juhudi zote hizo tuwe tayari kusameheana. Badala ya kuwahukumu watu tuwafundishe kufanya toba ya kweli mbele za Mungu kwa kuwa wema wa Mungu unatuvuta kwake tupate kutubu. Tukidharau wema huu wa Mungu tutakutana na hasira ya Mungu siku ile ya ufunuo wa hukumu atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Huu ni ule wakati Bwana wetu Yesu Kristo atakapokuja mara ya pili kuwahukumu walio hai na wafu. Matendo ya Mitume 10:42-43 “Akatuagiza kuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na wafu. Huyo manabii wote humshuhudia ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondeleo la dhambi.” Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua naye amewapa watu wote udhabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu. Mathayo 25:31 “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake,” Mataifa yote yatakusanyika mbele yake, waovu watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.

Neno la Mungu linatuonya kwamba tusihukumu wengine kabla ya wakati wa hukumu ya Bwana haiawadia. 1 Wakorintho 3: 4-5 “ Maana sijui sababu ya kujishitaki nafsi yangu, lakini sihesabiwi haki kwa ajili hiyo, ila anihukumuye mimi ni Bwana. Basi ninyi msihukumu neon kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana, amnaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza na kuyadhihirisha ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu. Neno hili ni kweli na Amini. 

Share This