• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 05 Nov, 2023
  • Admin

Luka 19:43-44 “Kwa kuwa siku zinakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako. "

Maneno ya mistari hii ni ya Bwana wetu Yesu Kristo alipoulilia mji wa Yerusalemu kwa kutojua yapasayo amani. Tuanze kutafakari neno hili kwa kuangalia maana ya neno majira na maana ya kujiliwa kwako . Majira ni zawadi kutoka kwa Mungu. Mungu alipoumba dunia aliweka majira kwa kila jambo. Mwanzo 8:22 “Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku havitakoma.” Mhubiri 3:1 “Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.” Majira ya kujiliwa kwako ni pale Mungu anapokuonyesha kusudi lake katika maisha yako. Neema hii hutegemea mahusiano yako na Mungu. Yohana 9:31 “Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu na kuyafanya mapenzi yake humsikia huyo.”

Katika somo hili tutatafakari mambo makuu matatu;

  • ·       Kutambua majira ya kujiliwa kwako.

  • ·       Madhara ya kutotambua majira ya kujiliwa kwako.

  • ·       Kurudi kwa Bwana wetu Yesu Kristo.

Katika ulimwengu wa mwili watu wanatambua majira mapya yanapowadia kutokana na dalili mbalimbali zinazojitokeza. Mkulima anatambua majira ya kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kuvuna mavuno. Dalili zinazomwongoza kujua majira ni pamoja na kuangalia mzunguko wa hali  ya hewa, pepo, jua, baridi, mawingu na mwezi. Mkulima ana namna ambayo akiona dalili hizi anatambua kuwa mvua zinakaribia naye anaanza maandalizi ya kilimo. Mungu anathamini umuhimu wa utambuzi wa majira kwa watu wake, hivyo akaweka juu ya Israeli wana wa Isakari wanaojua kutambua nyakati. 1 Mambo ya Nyakati 12:32 “na watu wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuwajua yawapasayo Israeli wayatenge; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao.” Ni muhimu sana kusoma majira au nyakati na dalili zake ili uweze kutumia vizuri fursa zinazo ambatana na majira hayo. Katika Ulimwengu wa roho zipo dalili zinazoweza kukujulisha majira ya kujiliwa kwako na fursa zilizoachiliwa. Kuna mambo ya msingi ambayo yakitokea katika maisha yako utatambua  kuwa ni majira ya kujiliwa kwako;

·       Kiwango cha nguvu unachopokea kwa BWANA.

·       Kiwango cha utendaji kazi wa Roho Mtakatifu.

·       Kiwango cha amani uliyonayo moyoni mwako.

·       Kiwango cha utendaji kazi wa adui.

Hatuna budi kukiri kuwa Mungu wetu ni Mungu mwenye nguvu. Neno lake lenye nguvu ndilo lililofanya kazi ya kuumba mbingu na nchi na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele (Ufunuo 7:12). Ufalme ni wa Mungu wetu na nguvu na utukufu. Mfalme Daudi alijua nguvu hizi za Mungu naye akaimba akisema, “ni nani Mfalme wa utukufu? BWANA mwenye nguvu, hodari, BWANA hodari wa vita. BWANA ni nguvu zangu na ngao yangu, moyo wangu umemtumaini, heshima na adhama ziko mbele zake, nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake.” Ni nguvu  hizi ambazo Mungu kwa neema yake huwapa wale wamchao, ili majira ya kujiliwa kwao waweze kutenda sawasawa na kusudi la Mungu katika maisha yao. 1 Nyakati 16:11 “mtakeni BWANA na nguvu zake; utafuteni uso wake siku zote.” Hatimaye tutaweza kuzidi kuwa hodari katika BWANA na katika uweza wa nguvu zake. Kiwango cha nguvu ya Mungu itendayo kazi ndani yako ni dalili nzuri ya kujiliwa kwako. Waefeso 3:20 “basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu.” Nguvu hii Mungu alimkirimia Mwanawe Yesu Kristo ili wale wote waliompokea wapate nguvu hii. Yohana 1:12 “bali wote walio mpokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.” Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, bali kwetu  sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. Pasipo hiyo nguvu hakifanyiki kitu chochote maishani mwako. Nguvu hii inatuwezesha kuyafanya mambo yote katika yeye atutiaye nguvu. Majira ya kujiliwa kwako Mungu atakujalia nguvu ili uweze kuhudumu kwa nguvu ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Imani yako ndio nguvu anayoitumia Mungu kufanya kazi ndani yako. Mungu anaangalia kiwango chako cha imani, imani yako ikiwa kubwa na nguvu za Mungu zinakuwa kubwa vivyo hivyo. Mathayo 17:20 “Yesu akawaambia kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana amini nawaambia, mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu ondoka hapa na uende kule, nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.” Dalili nyingine itakayokusaidia kutambua majira ya kujiliwa kwako ni nikiwango cha utendaji kazi wa Roho Mtakatifu ndani yako.

Roho Mtakatifu akiwa ndani yako unapata nguvu na ujasiri wa kumtumikia Mungu. Matendo ya Mitume1: 8 “lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi  mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Nguvu hii ya Roho mtakatifu inapoongezeka, unapokuwa jasiri kumshuhudia Kristo ujue kwamba hayo ni majira ya kujiliwa kwako. Dalili utakazoziona majira ya kujiliwa ni kujazwa Roho Mtakatifu na kuongezeka viwango vya utendaji kazi wa Roho Mtakatifu kiasi cha kuweza kuondolea watu dhambi. Yohana 20:22-23 “Naye (Yesu)  akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, pokeeni Roho Mtakatifu. Wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa: na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.” Wale wanaompokea Roho Mtakatifu wanapata fursa ya kupokea karama za Roho Mtakatifu.1 Wakorintho 12:4, 9-11 “Basi pana tofauti za karama, bali Roho ni yeye Yule, na mwingine hupewa karama za kuponya, na mwingine matendo ya miujiza, na mwingine unabii, na mwingine kupambanua roho, mwingine aina za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye Yule akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.” Karama za Roho Mtakatifu zinapoanza kutenda kazi kwa viwango vya juu katika maisha ya mtu ni dalili na ishara ya majira ya kujiliwa kwake. Kazi za karama hizi ni kumsaidia mtu katika kutekeleza kusudi la Mungu katika maisha yake. Karama hizi zinasaidiana katika kuujenga mwili wa Kristo. 1Wakorintho12:7 “ Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.” Katika 1 Petro 4:10 Neno la Mungu linasema, “kila mmoja kwa kadiri alivyopokea karama, itumieni kwa kuhudumiana, kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu,” “ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Tumwombe Mungu na tutake sana karama zilizo kuu tukitambua kuwa utukufu na uweza una yeye hata milele na milele.

Dalili nyingine ya kutambua majira ya kujiliwa kwako ni kiwango cha amani kilichopo ndani ya moyo wako. Kiwango cha amaniyako kitakuwa na kuongezeka sanaikiwa unajua yapasayo amani. Bwana wetu Yesu Kristo aliulilia mji wa Yerusalemu kwa sababu watu wake hawakujua yapasayo amani. Luka 19:41-42 “Alipofika karibu aliuona mji akaulilia, akasema , laiti ungejua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani. Lakini sasa yamefichwa machoni pako.” Katika mstali wa 44 anasema, adui watainuka juu ya mji ule na kuuharibu kwa sababu watu wake hawakutambua majira ya kujiliwa kwao. Amani ni tunda la Roho ambalo tunapewa na Mungu mwenyewe kwa neema yake na pia amani tunapewa na Bwana wetu Yesu Kristo. Hesabu 6:26 “BWANA akuinulie uso wake, na kukupa amani .” Atukuzwe Mungu juu mbinguni,na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia. Warumi 15:13 “Basi Mungu wa tumaini na awajaze ninyi furaha yote na amani katika kuamini, mpate kuzidi sana kuwa na tumaini, katika nguvu za Roho Mtakatifu.” Bwana wa amani mwenyewe na awape amani daima kwa njia zote. Amani ya Mungu imedhihirika kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Wafilipi 4: 7 “Na amani ya Mungu ipitayo akii zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Bwana wetu Yesu Kristo ndiye anayetupa amani yake. Yohana 14; 27 “Amani nawaachieni, amani yangu nawapa, niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.” Majira ya kujiliwa kwako Bwana Yesu ataachilia amani ndani ya moyo wako, ataondoa mafadhaiko yote na woga wote. BWANA wetu Yesu Kristo anatupatia amani yake kwa njia ya msalaba. Wakolosai 1:19-20 “Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi au vilivyo mbinguni. Bwana wetu Yesu Kristo alikufa pale msalabani ili tupate amani tuliyoipoteza kwa matendo yetu mabaya. Isaya 53:5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu alichubuliwa kwa maovu yetu; adhabu ya maovu yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake tumepona.” Yatupasa kufanya nini majira ya kujiliwa kwetu? Neno la Mungu linasema “iweni na amani ninyi kwa ninyi na tafuteni kuwa na amani na watu wote. Waebrania 12:4 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona BWANA asipokuwa nao.” Amani ni dalili nzuri au ishara nzuri ya kujiliwa kwako. Hivyo yatupasa kutenda mambo yale yaleteyo amani kwa njia ya Roho Mtakatifu. 1 Wakorintho 2:10 “Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.” Mambo ya Mungu na siri za Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. Yote hayo yatawezekana tu pale tutakapo kuwa na mahusiano mazuri na Mungu wetu. Dalili nyingine itakayokufanya utambue au ujue majira ya kujiliwa kwako ni kiwango cha utendaji kazi wa adui. Adui tunayezungumza habari zake hapa ni shetani/ ibilisi ambaye atainuka kwa viwango vikubwa kukupiga vita ili ushindwe kutambua fursa zilizopo katika kujiliwa kwako. Majila ya kujiliwa kwako yanabeba kusudi la Mungu katika maisha yako kwa hiyo huna budi kupigana vita hii kwa uhodari hadi umshinde shetani. Waefeso 6:12 “ Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote kusimama.” Silaha za Mungu ni darii ya haki, injili ya amani, ngao ya imani, neno la Mungu na sala. Ikiwa tutamtegemea Mungu na ikiwa tuna mahusiano mazuri naye, Yeye anasema vita yetu ni ya kwake sisi tunyamaze kimya. Anasema tusiogope wala tusifadhaike kwani vita si vyetu bali ni vya BWANA Mungu wetu ambaye atatusaidia na kutupigania mapigano yetu. Kutoka 14:13-14 “Musa akawaambia watu, msiogope simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakao wafanyia leo; kwa maana hao wamisiri mliwaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.” Jambo la msingi katika majira ya kujiliwa kwako ni utii kwa Roho Mtakatifu kwa maana ndiye mwenye dhamana ya kukuongoza katika kujua mapenzi ya Mungu. BWANA ajipatie utukufu wakati wa kujiliwa kwako. Imetupasa kutambua kuwa Mungu anazo njia nyingi anazoweza kuzitumia katika kuwasilisha neno lenye kusudi lake katika majira ya kujiliwa kwako. Majira hayo unatakiwa uwe makini sana chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu usije ukapoteza neema ya kujiliwa kwako. Amani ya Mungu Baba ikae nasi sote siku zote za maisha yetu.

Share This