• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 05 Nov, 2023
  • Admin

Luka 15:29 “Akamjibu baba yake, akasema, Tazama mimi nimekutumikia miaka mingi hii, wala sijakosa amri yako wakati wowote, lakini hujanipa mimi mwana - mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu.” Maneno  haya yamesemwa na kaka mkubwa wa mwana mpotevu alipoona nyimbo, machezo, mashangilio na shangwe kwa ajili ya mwana huyu aliyekula urithi wake na makahaba. Kaka yake anaona kuwa hakustahili heshima kubwa namna hii. Anaona kuwa yeye aliyemtumikia baba yake kwa uaminifu na kwa miaka mingi ndiye anayestahili heshima. Katika mstari huu tunayo mambo mengi ya kujifunza, kati ya hayo ni haya yafuatayo.

·       Tunatakiwa kuwasamehe waliotukosea. Kaka mkubwa hakuwa tayari kumsamehe mdogo wake. Mathayo 6:14-15 “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipo wasamehe watu makosa  yao wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.”

 

·       Tusinung’unike na kukasirika mtu anaposamehewa makosa au dhambi. Katika kisa hiki cha mwana mpotevu kaka yake mkubwa alikasirika akakataa kuingia ndani na kunung’unika ni kwa nini baba yake amemchinjia yeye ndama  aliyenona. Baba yake akamjibu katika Luka 15:32 akasema, “Tena kufanya furaha na shangwe ilipasa kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka, alikuwa amepotea naye ameonekana .” Hebu fikiri ndugu yako aliyekufa huku akiwa ametenda dhambi akafufuka, utakasirika na kunung’unika  au utafurahi pamoja naye? Hii ni sawa na mwenye dhambi mmoja akitubu kwa kuwa adhabu ya dhambi ni mauti ukikwepa mauti hii kwa kutubu kunakuwa na furaha mbele ya malaika wa Mungu mbinguni. Katika Luka 15:1-2 Mafarisayo walinung’unika BWANA Yesu alipowakaribisha watoza ushuru. “Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wanamkaribia wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung’unika wakisema, mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi tena hula nao.” Bwana Yesu alipoingia nyumbani kwa Zakayo mtoza ushuru watu walipoona walinung’unika wote wakisema, ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. Bwana Yesu akamtangazia Zakayo wokovu kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.

 

·       Tusijihesabie haki mbele za Mungu. Kaka mkubwa wa mwana mpotevu ajihesabia haki kwa kuwa amemtumikia baba yake kwa miaka mingi tena kwa utii wakati wote. Kwa hiyo aliona   kwamba kutokana na matendo yake mema anastahili kupewa mwana mbuzi afanye sherehe na rafiki zake. Neno la Mungu linatufundisha kuwa tusijihesabie haki wenyewe  isipokuwa  tumwache Mungu atuhesabie haki. Mafarisayo walijihesabia haki kwa sababu wameshika sheria na torati ya Musa. Bwana Yesu katika Luka 16:15 “Akawaambia, ninyi ndinyi mnaojidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu awajua mioyo yenu, kwa kuwa lililo tukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu.” Usijihesabie mwenye haki machoni pako mwenyewe, usijisifu sababu ya matendo yako mema na kujiona wewe ni mwema sana unayestahili. Usijihesabie haki chini ya jua kwa kuwa hakuna mkamilifu wote tumetenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu. Mungu peke yake ndiye mwenye haki na nguvu katika kazi zake zote azitendazo. Zaburi 129:4 “Bwana ndiye mwenye haki, amezikata kamba zao wasio haki.” Kutoka 9:27 “Farao akatuma watu na kuwaita Musa na Haruni, na kuwaambia, mimi nimekosa wakati huu; Bwana ni mwenye haki, na mimi na watu wangu tu waovu.” 2 Mambo ya Nyakati 12:6 “Ndipo wakajinyenyekeza wakuu wa Israel na mfalme; wakasema, BWANA ndiye mwenye haki.” Haki hii ya Mungu ndiyo aliyompa Mwanae Yesu Kristo. 2 Wakorintho 5:21 “yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate haki ya Mungu katika Yeye.” Warumi 1:17 “Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, mwenye haki ataishi kwa imani.” Hii ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Tumehesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki Yeye umwaminie Yesu (Warumi 3:24-26). Tunahesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria, na tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake tutaokolewa na ghadhabu kwa Yeye. Kuhesabiwa haki na Mungu inamaanisha kusamehewa dhambi zetu zote kwa sababu Kristo alibeba dhambi zetu pale msalabani. Wagalatia 2:15-16 “Sisi tulimwamini Yesu Kristo ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki.” Mfalme Daudi katika Zaburi 143:1-2 anasema “Ee BWANA uisike sala yangu, uzisikilize dua zangu, kwa uaminifu wako unijibu kwa haki yako. Wala usimhukumu mtumishi wako, maana kwako hakuna aliye hai mwenye haki.” Kwa kuwa hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema asifanye dhambi. Msamaha wa dhambi na haki ya Mungu ni zawadi za bure za neema zitokazo katika upendo wa Mungu. 1 Yohana 4:16 “Nasi tumelifahamu pendo alilonalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini, Mungu ni pendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu na  hukaa ndani yake,” na kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake,  naye ndani ya Mungu. Kila mwenye pumzi akiri hivyo. Haleluya.   

Share This