LUKA 15:18 “Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako”.
Mambo muhimu ya kutafakari.
Katika kisa hiki tunaelezwa kuhusu mtoto mpotevu aliyedai kutoka kwa baba yake sehemu ya mali inayomwangukia, akaondoka akaenda kuitapanya mali hiyo kwa maisha ya uasherati hadi akawa mhitaji. Mtoto huyu mpotevu alitambua kosa lake akachukua hatua kwa kuamua kwenda kwa baba yake na kuomba msamaha, akasema ,” nitaondoka, na kwenda kwa baba yangu na kumwambia Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako,” Kwa unyenyekevu mkubwa akasema sistahili kuitwa mwana wako tena. Baba yake alimwonea huruma akamsamehe na msamaha wake uliambatana na furaha kubwa, wakafanya sherehe kubwa wakala na kushangilia. Je, utawezaje kutambua kosa lako ili utubu? Kwa kuwa kwa upande mwingine shetani anakutoa ufahamu ili usitambue kosa lako usije ukatubu. Sisi kwa bidii zetu na akili zetu za kibinadamu hatuwezi kupata ufahamu wa kuzitambua dhambi zetu. Mungu kwa neema yake iliyo kuu inayopatikana katika Mwanae Yesu Kristo na upendo wake kwetu na huruma zake ndivyo vinavyotuwezesha kutambua dhambi zetu na kuzitubu. Waefeso 1:7 “Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake “. Kwa maana tumeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, ambayo hiyo haikutokana na nafsi zetu, ni kipawa cha Mungu, wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu (Waefeso 2:8-9). Mungu katika Isaya 43:25 anasema, “Mimi, naam,ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako”. Kwa sababu wote tumefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; tunahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa, apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki amwaminiye Yesu. (Warumi 3:23-26). Kwa maana hiyo dhambi haitatutawala sisi kwa sababu hatuko chini ya sheria, bali chini ya neema Tunaamini kwamba tutaokolewa kwa neema ya Bwana Yesu. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu ambaye alitumwagia kwa wingi ili tuhesabiwe haki kwa neema yake , tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu. Tito 2:11-13 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, tupate kuishi kwa kiasi, na haki na utauwa katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu.” Neema hii ya msamaha wa dhambi inapatikana kwa kuwa Mungu wetu ni mwenye upendo na mwenye huruma nyingi. Kama ilivyokuwa kwa mtoto mpotevu nasi twende mbele ya Baba yetu wa mbinguni kwa unyenyekevu mkubwa na kutubu dhambi zetu. Twende mbele za BWANA kama mfalme Daudi katika Zaburi 51:1-3 “Ee Mungu , unirehemu, sawasawa na fadhili zako, kiasi cha wingi wa rehema zako, uyafute makosa yangu. Unionyeshe kabisa na uovu wangu, unitakase dhambi zangu. Maana nimejua mimi makosa yangu na dhambi yangu mbele yangu daima. Nimekutenda dhambi wewe peke yako, na kufanya maovu mbele ya macho yako.“ Zaburi 51:11 & 7 “Usinitenge na uso wako, wala Roho wako mtakatifu usiniondolee.” “Unisafishe kwa hisoponami nitakuwa safi, unioshe nami nitakuwa mweupe kuliko theluji.” Uzifute hatia zangu zote. Mungu mwenye upendo wa ajabu hapendi mtu yoyote apotee, bali wote wafikilie toba ya kweli. 1 Yohana 1:9 “Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na kutusafisha na udhalimu wote.” Kwa kuwa yeye amesema atusamehe maovu yetu, na dhambi zetu hatazikumbuka tena kwa maana, wewe Bwana, U mwema, umekuwa tayari kusamehe, na mwingi wa fadhili, kwa watu wote wakuitao. Pendo kuu la Mungu tunaliona katika Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Upendo wa Mungu utakamilika ndani yetu ikiwa tutalishika neno lake na amri zake na kumwamini Yesu Kristo kuwa ni mwokozi wa maisha yetu na kipatanisho kati yetu na Mungu Baba, mwenye enzi yote . 1 Yohana 2:1-2 “ Watoto wangu wadogo , nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu, wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.” Yeye anatupenda na yupo tayari kutuosha dhambi zetu katika damu yake. Katika kisa cha mwana mpotevu Baba yake alimhurumia na kisha akamsamehe. vivyo hivyo na Mungu wetu ni Mungu mwenye huruma nyingi. Kutoka 34:5-7 “BWANA akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la BWANA. BWANA akapita mbele yake akatangaza, BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili , si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi.” Wenye dhambi rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie BWANA, Mungu wenu, kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya (Yoeli 2:13). Huruma na wema wa Mungu na ustahimili wake vyatuvuta ili tupate kutubu na kumrudia Mungu. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, na waliopondeka roho huwaokoa. Maombolezo 3:22-23 “Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, kwa kuwa rehema zake hazikomi. Ni mpya kila asubuhi, uaminifu wako ni mkuu.” Mungu amesema atamrehemu yeye amrehemuye, atamhurumia yeye amhurumiaye na tena atamhurumia aliye dhaifu na maskini, na nafsi za wahitaji ataziokoa. Tuhitimishe somo hili kwa kutafakari furaha inayoamatana na msamaha wa dhambi. Katika kisa cha mtoto mpotevu baada ya baba yake kumsamehe makosa yake aliagiza liletwe upesi vazi lililo bora, avikwe na atiwe pete kidoleni mwake na viatu mguuni, aletwe ndama yule aliyenona achinjwe ili wale na kufurahi. Luka 15:7,10 “Nawaambia vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya wenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu. Nawaambia, vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye. Mfalme Daudi alitambua kuwa msamaha wa dhambi unaambatana na furaha naye akasema; Zaburi 51:8,12 “Unifanye kusikia furaha na shangwe mifupa uliyoiponda ifurahi. Unirudishie furaha ya wokovu wako, unitegemeze kwa roho ya wepesi.” Zakayo yule mtoza ushuru alimkaribisha Yesu nyumbani kwake kwa furaha. Alipotubu dhambi zake Bwana Yesu akamwambia: “Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. Ikiwa Mungu na malaika zake wanafurahia na kufanya shangwe mwenye dhambi mmoja akitubu; Je furaha yetu sisi sio zaidi sana tunapo mwona mwenzetu ametubu na kumrudia Mungu? Mungu atusaidie kutambua dhambi, kujutia dhambi na kutubu na hatimaye kuingia katika furaha na shangwe ya Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu.