ISAYA 55:6-7 “Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, mwiteni, maadamu yu karibu .Mtu mbaya na aache njia yake na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, naye atamrehemu; na arejee kwa Mungu wetu naye atamsamehe kabisa."
Katika mistari hii ya Isya 55:6-7 tunapata mafundisho makuu yafuatayo:-
i. Tumtafute BWANA, maadamu anapatikana
ii. Tumwite BWANA maadamu yu karibu.
iii. Tutubu dhambi zetu na kumrudia Mungu naye ataturehemu na kutusamehe maovu yetu yote.
Neno la Mungu linatutaka tumtafute Mungu katika maisha yetu tusichoke kumtafuta Mungu ili atujaze Roho Mtakatifu wake atusaidie kusonga mbele katika kutumikia Mungu.Tumtafute Mungu wakati wa raha na shida kwa kuwa anapatikana .Tumtafute ili tumwabudu katika roho na kweli.Kumbukumbu la Torati 4:29 “Lakini huko kama mkimtafuta BWANA,Mungu wako utampata ukimfuata kwa moyo wako wote na roho yako yote”. 2Mambo ya Nyakati 15:1-4 “ Nisikieni , Ee Asia na Yuda wote wa Benjamini, BWANA yu pamoja nanyi , mkiwa pamoja naye, nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu, lakini mkimwacha atawaacha ninyi. Basi tangu siku nyingi Israel wamekuwa hawana Mungu wa kweli, wala hawana kuhani afundishaye, wala hawana torati , lakini walipomgeukia BWANA, Mungu wa Israeli katika msiba wao na kumtafuta akaonekana kwao”. Mungu anasema kuwa anawapenda wale wampendao na wale wamtafutao kwa bidii nao watamwona .Tunatakiwa kumtafuta Mungu bure kwa njia ya kusoma na kusikiliza neno lake, kwa maombi na dua pamoja na kufunga.Yeremia 29:12-14 “Nanyi mtaniita mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza.Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.Nami nitaonekana kwenu, asema BWANA”.
Zaburi 105:4 “Mtakeni BWANA na nguvu zake utafuteni uso wake siku zote”. Nawe utajifurahisha kwa BWANA, naye atakupa haja za moyo wako.Katika Agano jipya kuna mafundisho mengi yanayotutaka kumtafuta Mungu kwa maana anapatikana Mathayo 7:7-8 “ Ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtaona, bisheni nanyi mtafunguliwa .Kwa maana kila aombaye hupokea, naye atafutaye huona, naye abishaye atafunguliwa’.’
Tunatakiwa tumtafute Mungu kwa njia ya Imani .Waebrania 11:6 “ Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendekeza ; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na kwamba huwapa watu thawabu wale wamtafutao”.Njooni tuabudu , tusujudu, tupige magoti mbele za BWANA aliyetuumba kwa maana yu karibu naye anataka tumwite.Mungu wetu anapatikana wakati wote kupitia kwa Roho Mtakatifu wake.
Tumwite BWANA maadamu yu karibu .Yeremia 23:23-24 “Mimi ni Mungu aliye karibu asema BWANA, mimi si Mungu aliye mbali .Je, mtu yeyote aweza kujificha mahali pa siri, nisimwone? Asema BWANA .Je mbingu na nchi hazikujawa name.“Matendo ya Mitume 17:26-27 “Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani na mipakaya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa papasa, wakamwone ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu Waefeso 2:13, 17-18 “Lakini sasa katika Kristo Yesu , ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Akaja akihubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali na amani kwao waliokuwa karibu kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja” .Ni jukumu letu kumwita kwa kuwa atasikia na kutuitikia.Kumbukumbu la Torati 4:7 “ Kwa maana liko taifa gani kubwa , lililo na Mungu aliye karibu nao, kama BWANA, Mungu wetu alivyo , kila tumwitapo”. Mwimba zaburi anasema BWANA yu karibu na wote wamwitao, wote wamwitao kwa uaminifu.Kwa maana ndiye Mungu wetu na sisi tu watu wa malisho yake na kondoo za mkono wake.Ingekuwa heri leo msikie sauti yake na itakuwa kila atakayeliitikia jina la BWANA ATAOKOLEWA.Yeremia 33:3 “Niite nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa , magumu usiyoyajua”. Katika neno hili Mungu anaahidi kuwafundisha mambo makubwa watakaomwita.Tumeona kuwa tukimwita Mungu anapatikana hebu tunagalie ni wakati gani unaweza kumwita Mungu na asipatikane.Mithali 1:28-29 2 “Ndipo watakaponiita , lakini sitaitika, watanitafuta kwa bidii wasinione.Kwa kuwa walichukia maarifa, wala hawakuchagua kumcha BWANA .Hawakukubali mashauriyangu wakayadharau maonyo yangu”.Tunatakiwa tujiweke tayari kwa ajili ya ujio wa Bwana harusi.Katika wanawali 10 wale walioweka taa zao mafuta tayari kwa kumsubiri waliingia pamoja naye harusini na mlango ukafungwa Mathayo 25:11-13 “Halafu wakaja na wale wanawali wengine wakasema, Bwana,Bwana tufungulie.
Akajibuakasema, Amini nawaambia siwajui ninyi.Basi kesheni kwa sababu hamjui siku wala saa”. Katika mstari wa 27 “ naye atasema , nawaambia , siwajui mtokako, ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu .” Yohana Mtakatifu 9:31 “Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi, bali mtu akiwa mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo”. Maovu yetu yametufarakanisha na Mungu wetu na dhambi zetu zimeuficha uso wake tusiuone, hata hataki kusikia” . Ili tusije tukakaliwa na Bwana akakataa kutujibu tutakapomwita ni lazima tuzitengeneze njia zetu .Tutubu dhambi zetu na kumrudia Mungu naye ataturehemu na kutusamehe uovu wetu wote. Kumbukumbu la Torati 4:30-31 “Na wakati uwapo katika mashaka ukiisha kupatswa na mambo haya yote , siku za mwisho, utamrudia Bwana , Mungu wako na kusikiliza sauti yake; kwa kuwa BWANA Mungu wako ni Mungu mwenye rehema, hatakukosa wala kukuangamiza wala hatalisahau agano la baba zako alilowaapia.” Kutoka 34:6-7 “BWANA akapita mbele yake (Musa) akatangaza, BWANA Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili si mwepesi wa hasira mwingi wa rehema na kweli, mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi”. Mungu katika kitabu cha Nehemia 1:9 anasema, “Bali mkinirudia mimi, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, watu wako waliofukuzwa wajapokuwa katika pande za mwisho za mbingu hata hivyo nitawakusanya kutoka huko, na kuwaleta mpaka mahali pale nilipopachagua ili kuliweka jina langu hapo’’.Nabii Isaya katika Isaya 43:25 Mungu anasema hivi “ Mimi naam, mimi ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe , wala sitazikumbuka dhambi zako, na katika Isaya 44:22 anasema, “Nimeyafuta makosa yako kama wingu zito na dhambi zako kama kama wingu, unirudie maana nimekukomboa”. Katika agano jipya Neno la Mungu limewekwa wazi kuwa tunakombolewa kwaneema kwa damu ya Yesu Kristo iliyomwagika pale msalabani Golgota. Waefeso 1:6-7 “Na usifiwe utukufu wa neema yake ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa.Katika yeye huyo, kwa damu yake tunaoukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake”. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake, ambaye katika yeye tunaukombozi yaani msamaha wa dhambi .Naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote (Wakolosai 1:13-14).Katika mstari wa 20 Neno la Mungu linasema kuwa na kwa yeye (Yesu Kristo) kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake, kwa yeye ikiwa ni vitu vyote vilivyo juu ya nchi au vilivyo mbinguni.Waefeso2:6-10 “Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu, ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake ,upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu.Kwa maana mmeokolewa kwa neema kwa njia ya imani ambayo hiyo haikutokana na nafsi zetu ni kipawa cha Mungu wala si kwa matendo mtu awaye yote asiye akajisifu. Maana tu kazi yake tuliumbwa katika Kristo Yesu tutendematendo mema ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo”. Tumejifunza katika somo hili kuwa tunatakiwa kumtafuta BWANA, tumwite na ili atuitikie tutubu dhambi zetu na kumrudia .Mahusiano haya na mawasiliano hayo tunaweza kuyafanya kwa njia ya maombi.Maombi ni njia ya mawasiliano kati yetu na Mungu. Uhusiano wetu na Mungu ulifanywa kwa damu ya Mwana kondoo Yesu Kristoaichukuaye dhambi ya ulimwengu.Katika maombi tunapata mahitaji yetu ya kiroho na kimwili .Wafilipi 4:6-7 “ Msijisumbue kwa neno lolote, bali katika neno kwa kusali na kuomba ,pamoja na kushukuru haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu ipitayo akili zote itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu”.Katika maombi tunamkumbusha Mungu, tunahojiana naye kwa kumweleza mambo yetu ili atupe haki yetu. Isaya 1:18 “Haya njoni tusemezane asema BWANA dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana zitakuwa nyeupe kama theluji, zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”. Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki na masikio yake hukielekea kilio chao .Maombi ya mtu mnyofu ni furaha kwa BWANA na BWANA husikia sala ya mwenye haki.Mungu hasikilizi maombi ya mwenye dhambi kwa hiyo unapoanza kufanya maombi lazima utubu kwanza makosa yako yote kwa kuwa Mungu anasema maombi ya mwenye dhambi ni kelele mbele zake na maombi ya mwenye haki ni kama manukato.Yohana Mtakatifu 9:31“ Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambibali mtu akiwa ni mcha Mungu na kufanya mapenzi yake humsikia huyo”. Ili maombi yako yawe manukato mbele za Mungu ni lazima uombe sawa sawa na mapenzi yake. 1 Yohana 5:14-15 “Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, kuwa tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atatusikia.Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba”.Tunamhitaji Roho Mtakatifu kwa kuwa roho iradhi lakini mwili ni dhaifu na kwa kuwa hatujui kuomba itupasavyo. Warumi 8:26-27 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hatuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa’’.
Roho Mtakatifu pamoja na kazi zingine zote anatusaidia tuombe kwaimani .Mathayo 17:19-21 “Kisha wale wanafunzi wakamwambia Yesu kwa faragha wakasema, mbona sisi hatukuweza kumtoa (pepo)? Yesu akawaambia kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana amin nawaambia mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu ondoka hapa uende kule nao utaondoka, wala halitakuwepo neno lisilowezekana kwenu (lakini namna hii haitoki (pepo) ila kwa kusali na kufunga)”.Hakuna neno lolote litakaloshindikana kwetu ikiwa tutaomba kwa imani kwa jina la Yesu Kristo peke yake.Yohana 14:13-14 “Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya’’ ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiomba neno lolote kwa jina langu nitalifanya. Tukikesha na kuomba kwa jina la Yesu hatutaingia majaribuni na lolote tumwombalo Baba atatupa.1 Petro 5:14-16 “Mtu wa kwenu amekuwa hawezi ? Na awaite wazee wakanisa, nao wamwombee na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule na Bwana atamwinua hata ikiwa amefanya dhambi atasamehewa.Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana mpate kuponywa”. Tunatakiwa kudumu sana katika kuomba tukikesha katika kuomba kwa bidii na kushukuru bila kuchoka. 1 Wathesalonike 5:16-18 “Furahini siku zote; ombeni bila kukoma shukuruni kwa kila jambo, maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu”. “Tukumbuke kuwaombea wengine hata adui zetu. Mathayo 5:43-44 “Mmesikia kwamba imenenwa umpende jirani yako na umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia wapendeni adui zenu waombeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni, maana yeye huwaangaziejua lake waovu na wema huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki”.Yesu Kristo mwenyewe alitufundisha neno hili pale msalabani alipowaombea msamaha wale waliomsulubisha Luka 23:34 “Yesu akasema Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo’’.
Tuhitimishe neno hili kuhusu kuomba kwa kumwangalia Yesu Kristo ambaye alidumu katika kusali na kuomba .Alipoanza kazi ya kuchagua Mitume ilimbidi aombe kwanza . Luka 6:12-13 “ikiwa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu .Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake, akachagua kumi na wawili miongoni mwao ambao aliwaita mitume’’.Tunajifunza kutoka kwa Bwana Yesu kuwa tunapotaka kufanya jambo lolote tufanye maombi kwanza .Katika Biblia kuna sehemu nyingi zinazoonyesh jinsi Bwana Yesu alivyodumu katika kuomba (Mathayo 14:13, 26:44 Marko 1:35, Luka 3:21 na Luka 9:28 na sehemu zingine nyingi. Ndugu zangu katika Kristo Yesu tudumu katika kuomba daima kwa kuwa Mungu hatawaacha wale wote wanaodumu katika kuomba kwa imani na kwa jina la Yesu jina pekee tulilopewa kuomba kwalo .Ombeni nanyi mtapata furaha yenu iwe timilifu .Tukumbuke maneno ya sala ya Bwana utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe waliotukosea.Marko 11:26 “Lakini kama ninyi hamsamehe, wala baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu”.Neno hili limetoka kwa Bwana nalo ni ajabu machoni petu.Mwenye kusikia naasikie maneno haya ambayo Bwana analiambia Kanisa.