ISAYA 55:12-13 “Maana mtatoka kwa furaha, mtaongozwa kwa amani, mbele yenu milima na vilima vitatoa nyimbo, na miti yote ya kondeni itapiga makofi .Badala ya michongoma utamea msonabari, na badala ya mibigili, mhadesi; Jambo hili litakuwa la kumpatia BWANA jina, litakuwa ishara ya milele isiyokatiliwa mbali”.
Tuanza kutafakari unabii wa nabii Isaya kwa kuanzia ule mstari wa Isaya55:11.“Ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu, halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma”.Hii inamaanisha kuwa Mungu amelituma neno kazi na halitamrudia hadi likamilishe kazi lililotumwa , yaani limzalie BWANA matunda mema. Unabii huu ulitimia kupitia Yesu Kristo aliyetumwa ulimwengu kuwakomboa watu na dhambi zao ili wapate wokovu kwa kupatanishwa na Mungu aliye Mtakatifu.Yohana 3:16-17. “ Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu , hata akamtoa mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye”. Yesu Kristo mwenyewe katika Yohana 20:21 anasema, “ Basi YESU akawaambia tena (wanafunzi wake), Amani iwe kwenu kama baba alivyonituma mimi nami nawapeleka ninyi”.Yesu Kristo ametumwa ulimwenguni ili aiishuhudie kweli na kila aliye wa hiyo kweli huisikia sauti yake nayo itamweka huru kweli kweli.Yohana 8:31-32 “ Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamau kweli , nayo hiyo kweli itawaweka huru”. Baada ya Bwana Yesu kufundisha hiyo kweli alimzalia BWANA matunda mema, hivyo basi neno lililotaka kinywani mwa BWANA halikumrudia bure .Bwana Yesu aliwaombea wale aliowaleta kwa Mungu wale waliomwamini .Yohana 17:15-20. “Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu, bali uwalinde na yule mwovu. Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndiyo kweli kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni .Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli.Wala si hao tu ninaowaombea, lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao.Wote wawe na umoja, kama wewe Baba ulivyo ndani yangu, hao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kusadiki ya kuwa wewe ndiwe uliyenituma”. Na sisi sote tumejua ya kuwa Yesu Kristo ametumwa ulimwengu na Mungu , Baba mwenye enzi yote. Mtume Paulo katika Wakolosai 1:10 anasema “Mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa, mkizaa matunda kwa kazi njema na kuzidi katika maarifa ya Mungu’’. Na sisi wakristo wa leo tunatakiwa tumzalie Bwana matunda mema yanayompendeza.
Katika mistari ile ya Isaya 55:12-13 tunaonyeshwa kuwa ujio wa Bwana Yesu utaleta furaha, amani na shangwe ulimwenguni mwote .Ubaya utashindwa kwa wema na jambo hili litakuwa la kumpatia BWANA jina litakalodumu milele.
Yesu Kristo anasema amekuja ulimwenguni ili wale wanaoamini wawe na furaha mioyoni mwao na furaha yao hakuna awaondoleaye .Wafilipi 4:4-6 “ Furahini katika Bwana siku zote tena nasema , furahini.Upole wenu na ujulikane na watu wote.Bwana yu karibu .Msijisumbue kwa neno lolote , bali katika kila neno kwa kusali na kuomba pamoja na kushukuru , haja zenu na zijulikane na Mungu”. Mungu hufurahi mtu mmoja akitubu dhambi zake na kumrudia .Luka 15 :7 “ Nawaambia ,vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambalo hawana haja ya kutubu”. Kwa maana huyo Mwana –kondoo , aliye katikati ya kiti cha enzi , atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchem za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao.
Tuhitimishe sehemu hii ya unabii kwa kuangalia amani ya Kristo ambayo hupatikana katika neno lake na katika kuomba sawasawa na mapenzi yake. Utakumbuka kuwa Yesu Kristo alipozaliwa wachungaji makondeni walipashwa habari na Malaika kuwa amewaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote.Luka 2:13-14 “ Mara walipokuwapo pamoja na huyo Malaika, wingi wa jeshi la mbinguni , wakimsifu Mungu na kusema, Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia’’. Wakolosai 3:15-16 “ Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu, ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja, tena iweni watu wa shukrani .Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo na tenzi za rohoni , huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu’’. Yesu Kristo katika Yohana 14:27 anasema,” Amani nawaachieni, amani yangu nawapa, niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo’’. Kwa kuwa amani ya Mungu inapita akili zote, inatuhifadhi mioyo yetu na nia zetu katika Kristo Yesu.Mungu ametuita katika amani, tuwe na amani kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.Amani ndani ya Ysuni amani ndani ya Neno la Mungu na Yesu Kristo ni neno la Mungu.Mungu anatutaka tukae katika amani na watu woteanaposema .Iweni na amani ninyi kwa ninyi. Neema na iwe kwako, na rehema na amani zitokazo kwa Mungu, Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.
Tumalize somo hili la unabii kwa kuangalia sehemu ile ya mstari wa 13 inayoonyesha kuwa ubaya utashindwa kwa wema na jambo hili litakuwa la kumpatia BWANA Jina litakalodumu milele.Ubaya ni mambo yasiyompendeza Mungu yaani dhambi .Kushinda ubaya au dhambi ni kumwamini Yesu Kristo kwamba ni Bwana na mwokozi wa maisha yako. Luka 6:27“
Lakini nawaambia ninyi mnaosikia , wapendeni adui zenu , watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawaonea ninyi .Akupigaye shavu moja , mgeuzie la pili, naye akunyang’anyaye joho yako, usimzuilie na kanzu. Mpe kila akuombaye na akunya’ganyaye vitu vyako , usitake akurudishie .Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vyvyo hivyo’’ Katika mistari ile ya 35 na 36 Bwana Yesu anasema, “ Bali wapendeni adui zenu , tendeni mema na kukopesha msitumaini kupata malipo na thawabu yenu itakuwa nyingi , nanyi mtakuwa wana wa Mungu aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru , na waovu.Basi iweni na hurumaa, kama Baba yenu alivyo na huruma’’ Warumi 12:19 – 21 “ Wapenzi msijilipize kisasi bali ipisheni ghadhabu ya Mungu , maana imeandikwa kisasi ni juu yangu mimi, mimi nitalipa, anena BWANA .Lakini adui yako akiwa na njaa, mlishe, akiwa nakiu mnyweshe, maana ufanyavyo hivyo utampatia makaa ya moto kichwani pake. Usishindwena ubaya , bali uushinde ubaya kwa wema”.Hapa tunajifunza kwamba tuwasamehe wale wote waliotukosea kama vile Bwana wetu Yesu Kristo anavyotusamehe dhambi zetu. Tusamehe bila kuombwa wala kubembelezwa wala kulazimishwa.Kazi njema aliyofanya Bwana wetu Yesu Kristo imempatia Mungu jina litakalo dumu milele pamoja na jina la Yesu , jina lipitalo majina yote.Nao wakamwitaYesu jina lake Imanueli; yaani Mungu pamoja nasi na ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao .Yesu Kristo katika Yohana Mtakatifu 17:26 anasema “Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo, ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao”. Bwana wetu Yesu Kristo katika mafundisho yake alifundisha mapenzi ya Mungu na ufalme wa Mbinguni kwa kuonyesha mapenzi ya Mungu na kusudi lake la ukombozi wa wanadamu .Yohana 14;12-14 “ Amin , amin nawaambia , yeye aniaminiye mimi kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya , naam na kubwa kuliko hizo atafanya kwa kuwa mimi naenda kwa Baba .Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu , hilo nitalifanya , ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.Mkiomba neno lolote kwa jina langu nitalifanya”Bwana Yesu anamwambia Baba yake kuwa amewadhihirishia watu wake jina lake.Yohana 17:6-8 “Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu , walikuwa wako, ukanipa mimina neno lako wamelishika .Sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka kwako .Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa hao nao wakayapokea , wakajua hakika ya kuwanalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma’’. Bwana Yesu alimtukuza Mungu alipotufundisha kusali Mathayo 6:9-13 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni , jina lako litukuzwe, ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi tuwasamehevyo wadeni wetu.Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu.Kwa kuwa ufalme ni wako na nguvu , na utukufu , hata milele.Amina.Mtu akimtumikia Bwana Yesu na kumfuata atakuwepo pamoja naye tena mtu akimtumikia anasema kuwa Baba atamheshimu.Wanafunzi wake walipomuuliza tuambie ni nini dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia? Mathayo 24:36 “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni , wala Mwana ila Baba peke yake’’. Hata hivyo akawaonya kuwa mwenye kuvumilia hata mwisho ndiye atakayeokoka .Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote , hapo ndipo ule mwisho utakapokuja. Ili hili litimie Bwana Yesu anawaagiza wanafunzi wake waende ulimwenguni pote wakiihubiri Injili Mathayo 28:18-20” Yesu akaja kwao akasema nao akawaambia, nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani .Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi, na tazama , mimi nipo pamoja nanyi siku zote , hata ukamilifu wa dahari”.
Tunajifunza katika sala ya Bwana kuwa jina hili lina nguvu na utukufu na litadumu hata milele .Nguvu ya jina hili tunaiona katika maombi. Mathayo 18:19-20 “Tena nawaambia ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lolote watakaloliomba, watafanyiwana Baba yangu aliye mbinguni.Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu , nami nipo papo hapo katikati yao”. Yesu Kristo katika Yohana 14:13 anasema hivi “Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu , hilo nitafanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana”. Utukufu wa Mungu ulionekana katika Yesu Kristo Bwana wetu. Yohana 17:4-5 “ Mimi nimekutukuza duniani , hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye .Na sasa, Baba unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako”. Mungu alisikia maombi ya Mwanae kama tunavyosoma katika Wafilipi 2:9-11” Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina ; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni , na vya duniani , na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwautukufu wa Mungu Baba”.
Bwana Yesu anatoa nguvu iliyoko kwenye jina lake kwa wale wamwaminio na kukiri kuwa yeye ni Bwana .Marko Mtakatifu 16:17-20’’ Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio, kwa jina langu watatoa pepo, watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka , hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa , nao watapata afya.Basi Bwana Yesu baada ya kusema nao akachukuliwa juu mbinguni , akaketi mkono wa kuume wa Mungu .Nao wale wakatoka wakahubiri kote , Bwana akitenda kazi pamoja nao na kulidhibitisha ile neno kwa ishara zilizofuatana nao”. Tuangalie jinsi neno hili lilivyootekelezwa naMitume na ambalo linatekelezwa hata hivi leo. Matendo ya Mitume 8:7-8 “ Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu, na watu wengi waliopooza na viwete wakaponywa .Ikawa furaha katika mji ule”. Paulo alimuamuru na kumtoa pepo wa uuguzi wa kijakazi mmoja.Matendo 16:18 (b) “ Lakini Paulo akasikitika akageuka akamwambia yule pepo, nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo mtoke huyu.Akamtoka saa ile ile”. Jina hili la Yesu Kristo kando ya kuponya linaokoa. Warumi 10:9’’. Kwa sababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako kuwa ni Bwana na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka “wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu waliopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. Ukimwamini Yesu na ukiokoka unakuwa chombo kiteule kwake, unayechukua jina lake mbele ya mataifa na wafalme na watu wote Falme zingine zinaanza na kuisha lakini ufalme wake hauna mwisho.Luka 1:33. “Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa mwisho”. “Kwa kuwa yeye ndiye yeye yule na miaka yake haitakoma.Sisi Je, tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii?.