• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 13 Oct, 2023
  • Admin

ISAYA 55:1-3 “Haya kila aonaye kiu, njoni majini.Naye asiye na maziwa, bila fedha na bila thamani .Kwani kutoa fedha kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni kwa bidii mle kilicho chema, na kujifurahisha nafsi zeni kwa unono.Tegeni masikio yenu , na kunijia , sikieni na nafsi zenu zitaishi, nami nitafanya nanyi agano la milele , Naam rehema za Daudi zilizo imara."

Unabii wa Isaya 55:1-3 unatoa mwito wa kuja kula na kunywa bure .Anasema watakaoitikia wito huu watakula kilicho chema na nafsi zao zitaishi kwa furaha.Atafanya nao agano imara na la milele .Maono haya ya nabii Isaya yalitimia pale Bwana Yesu alipokuwa anazungumza na mwanamke Msamaria.Yohana 4:10, 13-14 “Yesu akajibu akamwambia, kama ungalijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye naye angalikupa maji yaliyo hai. Yesu akajibu akamwambia, kila anywaye maji haya ataona kiu tena, walakini yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele, bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani ya chemchemi ya maji yakibubujikia uzima wa milele’’. Yesu akajifunua kwa yule mwanamke .Yohana 4:25-26 “ Yule mwanamke akamwambia , najua ya kuwa yuaja Masihi (aitwaye Kristo), naye atakapokuja yeye atatufunulia mambo yote.Yesu akamwambia , Mimi ninayesema nawe, ndiye’’ Yesu anatuita tuje kwake ili tunywe maji ya uzima. Yohana 7:37 “ Hata siku ya mwisho , siku ile kubwa ya sikukuu , Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema , mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe .Aniaminiye mimi kama vile maandiko   yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake .Na neno hilo alisema katika habari ya roho , ambaye wale wamwaminio watapokea baadaye; kwa maana roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa .Basi wengine katika mkutano waliposikia maneno hayo, walisema , hakika huyu ndiye nabii yule .Wengine walisema ,huyu ndiye Kristo .Mungu anasema kuwa atatoa uzima wa milele bure.Ufunuo 21:6 -17 “ Akaniambia imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho.Mimi nitampa yeye mwenye kiu ya chemchemi ya maji ya uzima bure.Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake , naye atakuwa mwanangu.Na roho wa Bibi arusi wasema Njoo! Njoo! Naye asikiaye na aseme, njoo! Naye mwenye kiu na aje, nay eye atakaye na ayatwae maji ya uzima bure .Bwana Yesu azidi kutuita tuje kwake tupate raha nafsini mwetu.Mathayo 11:28-30 “Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu , kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi nitapata raha nafsini mwenu kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.’’

Unabii wa Isaya kwa upande wa chakula ulitimia katika Yohana 4:31-36 “Huko nyumba wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule. Akawaambia mimi ninacho chakula msichokijua ninyi. Basi wanafunzi wake wakasemezana, je, mtu amemletea chakula? Yesu akawaambia, chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake.Hamsemi ninyi, bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama mimi nawaambieni , inueni macho yenu myatazame mashamba ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno.Naye avunaye hupokea mshahara na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja’’Wasamaria waliposikia maneno ya Yesu waliamini na kujua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.Je, wewe ndugu yangu unayesoma maneno haya ya Bwana wetu Yesu Kristo unasemaje kuhusu Bwana Yesu?.Uko tayari kumshuhudia kwa wengine kuwa ni Mwokozi wa maisha yako na ni Mwokozi wa ulimwengu?.Bwana Yesu aliimaliza kazi ya Mungu aliyomtuma pale msalabani Calvary alipotangaza kuwa Imekwisha .Akainama kichwa akaisalimu roho yake.

Mungu kupitia unabii huu wa nabii Isaya anasema kuwa atafanya agano imara na la milele na wale watakaotega masikio yao na kumjia .Mungu katika Agano la Kale alifanya maagano mengi na wale wamchao na moja katika hayo ni jinsi alivyomrehemu mtumishi wake Daudi na kumuahidi kuwa atamfanyia jina kuu kama jina la wakuu walioko duniani (2Samwel 7:8-9) Utakumbuka pia ya kuwa ujio wa Yesu Kristo ulitabiriwa kupitia katika uzao wa Daudi.Nabii Yeremia alitabiri ujio wa Agano Jipya. Yeremia 31:31, 40 “Angalia siku zinakuja , asema BWANA nitafanya agano jipya na nyumba ya Israel na nyumba ya Yuda.Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israel , baada ya siku zile, asema BWANA.Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaandika; nami nitakuwa Mungu wao , nao watakuwa watu wangu .Nami nitafanya agano la milele pamoja nao, kwamba sitageuka wala kuwaacha ili niwatendee mema, nami nitatia kicho changu mioyoni mwao, ili wasiniache.Agano jipya limekuja kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.Ni agano la upatanisho kati yetu wanadamu wenye dhambi na Mungu wetu aliye mtakatifu ili tupate wokovu kwa kupitia kwa kifo cha Bwana Yesu Kristo .Mathayo 26:27-28 “ Akakitwaa kikombe akashukuru akawapa akisemanyweni nyote katika hiki, kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi’’.

Agano hili jipya ni bora zaidi kuliko lile la zamani kwa kuwa limeamuriwa juu ya ahadi zilizo bora zaidi.Basi kwa kadiri hii Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi .Waraka wa Waebrania 9:12-16 “Wala si kwa damu ya mbuzi na ndama , bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika patakatifu , akiisha kupata ukombozi wa milele.Kwa maana , ikiwa damu ya mbuzi na mahafali na majivu ya ndama ya ng’ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili, basi si zaidi damu yake Kristo , ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa , itawasafisha dhamira zenu na matendo mafu , mpate kumwabudu Mungu aliye hai .Na kwa sababu hii ni mjumbe wa agano jipya ili mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya agano la kwanza , hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele .Maana agano la urithi lililopo, lazima iwepo mauti yake aliyelifanya’’

Kwa hiyo ndugu zangu tukila chakula cha Bwana hatuna budi kukumbuka kuwa kikombe hiki ni agano jipya katika damu ya Yesu itolewayo kwa ajili ya wokovu wetu na uzima wa milele. Maana kila tunapokula mkate huu na kukinywea kikombe hiki, twatangaza mauti ya Bwana hata ajapo.

Share This