• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 13 Oct, 2023
  • Admin

ISAYA 48:17 ''BWANA, mkombozi wako, mtakatifu wa Israel asema hivi, mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata’’

Neno hili lina mafundisho mengi katika maisha yetu, kwanza linatufundisha kuwa BWANA ni mtakatifu nani mkombozi wetu .Mambo ya Walawi 19:1 ‘‘BWANA akanena na Musa , akamwambia , Nena na mkutano wote wa wana wa Israel , uwaambie, mtakuwa watakatifu, kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wenu ni mtakatifu .Katika maono haya ya Isaya mwana wa Amozi tutatafakari, mambo makuu mawili. Tutaangalia jinsi BWANA, Mungu anavyotufundisha na faida zake (faida za kufundishwa na BWANA) pamoja na njia tunayopaswa kuifuata. Tuanze kwa kuangalia ni kwa jinsi gani Mungu anatufundisha. Zaburi 32:8 ‘‘nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, nitakushauri, jicho langu likikutazama‘‘Mungu anawatumia manabii na watumishi wake kuwafundisha wengine juu ya amri na sheria zake. Kutoka 18:20 ‘‘Nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utaonyesha njia ambayo inawapasa kuiendea na kazi ambayo inawapasa kuifanya’’.Na sisi tunaofundishwa mambo yanayompendeza Mungu tunatakiwa tuyashike , tukatende yale yote yatupasayo maana hiyo ndiyo hekima na akili machoni pa BWANA ,Mungu wetu. Tunatakiwa pia kuwafundisha wale wasiozijua amri za Mungu ili kumcha Mungu. Zaburi 25:4-5 ‘‘Ee BWANA , unijulishe njia zako unifundishe mapito yako , uniongoze katika kweli yako, na kunifundisha.Maana wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu, nakungojea wewe mchana kutwa’’ Maandiko yote hayo yanatufundisha kuwa Mungu anatufundisha kupitia Neno naye Neno alikuwepo pamoja na Mungu. Yohana 1:1-5, 14 ‘‘Hapo mwanzo kulikuwako Neno naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyu mwanzo alikuwako kwa Mungu.Vyote vilifanyika kwa huyo, wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika.Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima , nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.Nayo nuru yanga’a gizani wala giza haliwezi .Naye neno alifanyika mwili, akakaa kwetu , nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwaBaba amejaa neema na kweli’’.

Neno la Mungu ni taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu. Bwana wetu Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani aliwafundisha watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanafunzi wake na makutanoYesu Kristo wakati mwingine alifundisha kwa njia ya mifano, mafumbo na miujiza.Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri , na kusema tubuni, kwa maana ufalme wa Mbinguni umekaribia (Mathayo 4:17). Kwa maana alikuwa akifundisha kama mtu mwenye amri , wala si kama waandishi wao kwa kuwa amepewa mamlaka yote mbinguni na duniani .Yesu akawafundisha wanafunzi wake mambo mengi pamoja na kusali sala ya BWANA.Bwana Yesu alizunguka sehemu mbalimbali akifundisha na kukuhubiri habari njema ya ufalme wa Mungu, Mathayo 4:23 ‘‘Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu’’. Mathayo 5:1-10 ‘‘Naye alipowaona makutano alipanda mlimani na alipokwisha kuketi , wanafunzi wake walimjia , akafumbua kinywa chake akawafundisha akisema:

1.    Heri walio maskini wa roho, Maana ufalme wa mbinguni ni wao

2.    Heri wenye huzuni , Maana hao watafarijika

3.    Heri wenye upole , Maana hao watairidhi nchi

4.    Heri wenye njaa na kiu ya haki , Maana hao watashibishwa

5.    Heri wenye rehema , maana hao watapata rehema

6.    Heri wenye moyo safi , maana hao watamwona Mungu

7.    Heri wapatanishi , maana hao wataitwa wana wa Mungu

8.    Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao.

Mafundisho ya Yesu Kristo yalilenga katika upatanisho wetu na Mungu wetu kwa njia ya damu yake iliyomwagika pale msalabani .Alitufundisha njia ya kuendea ili kupata wokovu na uzima wa milele unaopatikana kwa kumwamini yeye kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yetu. Kwa maana Kristo aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi , mwenye haki kwa ajili ya wasio haki, ili atulete kwa Mungu .Yesu ndiye njia ya pekee Yohana 14:6, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi’’. Na huu ndiyo ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele, na uzima huu umo katika Mwanae.Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima , asiye naye mwana wa Mungu hana huo uzima. Uzima huo ni kwa wale wanaloliamini jina la Mwana wa Mungu na kuomba sawa sawa na mapenzi yake. Baada ya Yesu Kristo kuondoka duniani alituletea Roho Mtakatifu iliatufundishe kuyashika yote aliyotuamuru.

Yohana 14:16-17 ‘’Nami nitamwomba Baba, naye atawapa msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele, ndiye roho wa kweli, ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea kwa kuwa haumwoni wala haumtambui bali ninyi mnamtambua maana anakaa kwenu , naye atakuwa ndani yenu.

‘‘Kazi kubwa ya Roho Mtakatifu ni kutufundisha yote na kutukumbusha yote Bwana wetu Yesu Kristo aliyotuambia.Kwa njia ya Roho Mtakatifu Bwana wetu YesuKristo anatutuma tuwafundishe watu neno lake.Wakolosai 3;16 ‘‘Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi , na nyimbo , na tenzi za rohoni, huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Tuhitimishe mafundisho ya kufundishwa na Mungu kwa kuangalia ni faida tutakazozipata kwa kukubali kufundishwa na Mungu kupitia Neno lake Isaya 48:18-19‘‘Laiti ungalisikiliza amri zangu .Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji na haki yako kama mawimbi ya bahari .Tena wazao wako wangelikuwa kama mchanga, na hao waliotoka katika tumbo lako kama chembe zake; jina lake lisingalikatika , wala kufutwa mbele zangu’’.

Katika Neno hili tunaona faida kubwa ambazo ni amani, haki na baraka za uzao wa tumbo lako. Yohana 8:31-32 ‘‘Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi walioamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli, tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru’’. Maana yake ni kuwa hatutakuwa tena watumwa wa dhambi bali tutakuwa huru katika Yesu Kristo, Bwana wetu.Katika mistari ile ya 34-36 ‘‘Yesu akawajibu, Amin, Amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi wala mtumwa hakai nyumbani siku zote, mwana hukaa siku zote.BasiMwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kwelikweli. ‘‘Amani ya kweli hupatikanakwa Mungu ndio maana imeandikwa katika Walipi 4:7. ‘‘Na amani ya Mungu ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenuna nia zenu katika Kristo Yesu’’ Neema na rehema na amani zinatoka kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu’’ Bwana wetu. Wakolosai 3:15 ‘’Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu, ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja , tena iweni watu wa shukrani’’. Ukiwa na amani ya Kristo utaweza kuamua mambo mbalimbali kwa kumuomba Mungu akupe ufumbuzi au macho ya rohoni.Tena ukiwa na amani utaweza kufanya kazi kwa haki. Isaya 32:17-18 ‘‘Na kazi ya haki itakuwa amani, na mazao ya haki yatakuwa ni utulivu na matumaini daima.Na watu wangu watakaa katika kao la amani , na katika maskani zilizo salama na katika mahali pa kupumzikia penye utulivu. ‘‘Siku zake yeye , mtu mwenye haki atastawi na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma (Zaburi 72:7).Neno la Mungu linatuonyesha kuwa mwenye haki ana faida nyingi. Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki na masikio yake hukielekea kilio chao. Wenye haki watairithi nchi, nao watakaa humo milele na kazi yake mwenye haki huuelekea uzima.Mwenye haki hataondolewa milele, bali wasio haki hawatakaa katika nchi. Mithali 14:34 ‘’ Haki huinua taifa bali dhambi ni aibu ya watu wote ‘’Wenye haki watakwenda katika uziima wa milele.Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani na kufungwa miguu utayari tupatao kwa injili ya amani. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye.Mwenye haki na azidi kufanya haki, na mtakatifu na azidi kutakaswa . Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki , maana ufalme wa mbinguni ni wao.

Faida nyingine tutakayoipata ni kuwa Mungu huubariki uzao wa wenye haki ambao wanazishika amri zake. Mithali 3:1-2 ‘‘Mwanangu, usisahahu sheria yangu, bali moyo wako uzishike amri zangu.Maana zitakuongezea wingi wa siku na miaka ya uzima na amani’’ Mungu anatuagiza kumpenda , kuenenda katika njia zake na kushika maagizo yake, na amri zake na hukumu zake ili tupate kuwa hai na kuongezeka (Kumbukumbu la Torati 30:16).Ndugu zangu, natutafute kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao .Tuutafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake yote na hayo mengine yote tutazidishiwa.Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu atufanye kuwa wakamilifu katika kila tendo jema, tupate kuyafanya mapenzi yake.

Share This