EZEKIEL 36:25-28 “Nami nitawanyunyizia maji safi, nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa nyinyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, na kuzitenda.Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu”.
Nabii Ezekiel aliinuliwa na Mungu wakati wana wa Israeli walipokuwa chukizo mbele ya BWANA. Wana wa Israeli waliabudu miungu mingine, walifanya uzinzi na uasherati, wauaji, waasi na walifanya mioyo yao kuwa migumu kama jiwe. Kwa hiyo Mungu alimwaga hasira yake juu yao, kwa ajili ya damu waliyoimwaga juu ya nchi na kwa sababu wameitia uchafu kwa vinyago vyao. Mungu akawatawanya katika nchi nyingi na akawaadhibu kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na njaa, tauni, vita, vifo na hata kuchukuliwa mateka na maadui zao. Walitia jina la BWANA unajisi kwa kuwa watu walinena wakisema, watu hawa ni watu wa BWANA nao wametoka katika nchi yake. Lakini Mungu aliwahurumia kwa ajili ya jina lake takatifu akaamua kulitakasa jina lake walilolinasi ili watu wa mataifa wajue kuwa Yeye ndiye BWANA, Bwana Mungu wao. BWANA akawatwaa kati ya mataifa, akawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yao wenyewe. Hapa ndipo BWANA anapowaahidi kuwatakasa na kuwapa moyo na roho mpya na kuwa hapo ndipo watakuwa watu wake naye atakuwa Mungu wao. Katika somo hili nataka tujifunze mambo makuu matau;
Huruma na upendo wa Mungu kama ulivyoonekana kwa wana wa Israeli ndivyo ulivyo kwetu hata leo hii. Yohana Mtakatifu 3:16-17 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanaye wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele”. Mungu alimtuma Mwanaye Yesu Kristo baada ya wanadamu kuasi; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Hakuja kuhukumu ulimwengu bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Hapa tunaona huruma na upendo wa Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni pendo. Mungu alitupenda sisi ndio maana akamtuma Mwanaye kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu. Bwana wetu Yesu Kristo anazo sifa za kuwa na huruma na upendo kama Baba yake. Yeye alijitolea na kutumwa kuja ulimwenguni kuokoa watu na dhambi zao. Kwa kuwa anatupenda aliubeba msalaba na kufa kwa ajili yetu. Upendo wa Kristo unaonyesha kikamilifu upendo wa Baba yake, huruma yake na utayari wa kusamehe. Yohana Mtakatifu 15:13. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake”. Yesu alipokuwa hapa duniani aliwahurumia watu wenye shida mbalimbali za magonjwa, mapepo, njaa, misiba na dhambi. Upendo wake na huruma zake zilimfanya awaponye wagonjwa, awatoe mapepo, awape chakula wenye njaa, afufue watu kutoka kwa wafu na awasamehe watu dhambi zao. Warumi 8:35, 37-39 “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida au adha, au njaa au uchu, au hatari, au upanga?”
Lakini katika mambo hayo yote tunashinda na zaidi ya kushinda kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu. Ili tuweze kujaa ujasiri na ushupavu wa namna hii tunahitaji kuwa na nguvu ya roho wa Mungu.
Katika sehemu hii inayofuata tunajifunza kuhusu roho wa Mungu anayekaa ndani yetu. Mungu katika neno lake anasema atatia roho yake ndani yetu. Warumi 8:14 “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu”. Roho wa Mungu ni nguvu za utendaji wa Mungu ambazo anawajaza watu wake kupitia Neno lake ili wapate nguvu ya kumshuhudia kuwa yeye ni Bwana Mungu wa wote wenye mwili. Ukijazwa na nguvu hii unajaa hukumu na uwezo wa kuwahubiri watu maovu yao na dhambi zao .Ni nguvu hii ambayo Bwana Yesu aliwaahidi wanafunzi wake na hatimaye kutenda siku ya Pentecoste. Yohana Mtakatifu 15:26-27 “Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, yeye atamshuhudia. Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwepo pamoja name.” Matendo ya Mitume 2:1-4.“Hata ilipotimia siku ya Pentecoste walikuwepo wote mahali pamoja. Kukaja ghafla toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaze nyumba yote waliyokuwa wameketi.Kukawatokea ndimi zilizogawanyika kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine kama Roho alivyowajalia kutamka”. Neno la Mungu linasema kuwa naye akiisha kuja huyo atauhakikishia ulimwengu kwa habari ya dhambi na haki na hukumu. Naye Roho ndiye ashuhidiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli na huu ndio ushuhuda ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanaye.Yeye aliyenaye Mwana anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima kwa kuwa Mungu alimtuma Mwanaye pekee ulimwenguni ili tupate uzima katika yeye tena tuwe nao tele. Hata hivyo Mungu anatutahadharisha tusiamini kila roho. 1Yohana 4:1-3 “Wapenzi msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo, wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua Roho wa Mungu, kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu. Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja na sasa imekwisha kuwako duniani” Katika hili wanaojua Roho ya kweli na roho ya upotevu ni watu wa Mungu wale anaosema kuwa watakuwa watu wake naye atakuwa Mungu wao. Tuangalie kwa undani kidogo ni kwa namna gani tunakuwa watu wa Mungu naye anakuwa Mungu wetu. Wakati mwingine watu wa Mungu wanajulikana kama watoto wa Mungu. Hawa ni wale ambao wameitikia wito wa kutubu na kumwamini Yesu Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yao. Kwa hiyo katika imani hiyo wanakiri na kubatizwa katika jina la Mungu wa utatu. Wamekata shauri la kumkataa Shetani na mambo yake yote na kazi zake zote, wamejitoa kwa Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ili wamtegemee na kumtumikia kwa uaminifu hata watakapokufa.Bwana amejaa huruma na neema. Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhila. Kama vile Baba awahurumiavyo watoto wake, ndivyo BWANA awahurumiavyo wamchao. Huwasamehe dhambi zao na kuwaingiza katika kundi lake. Yohana Mtakatifu 1:12-13 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu”. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Rooho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu .Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu na warithi wa ufalme wa Mungu pamoja na Kristo.Tazameni ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Wewe uliye mwana wa Mungu huna budi kumpenda Mungu kwa moyo wako wote, roho, akili na nguvu zako zote. Tena mpende jirani yako kama nafsi yako. Wapenzi ikiwa Mungu alitupenda hata akamtuma Mwanaye pekee ulimwenguni ili tupate uzima kwa yeye, imetupasa na sisi kupendana. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu. Na amri hii tumepewa na yeye ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.
Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema kwa maana fadhili zake ni za milele. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwenye upendo, huruma na rehema nyingi. Amina.