1 WAFALME 17:10-11 “Basi akaondoka akaenda Sarepta, hata alipofika langoni pa mji, kumbe! mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni, akamwita, akamwambia, niletee nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako”.
Katika neno hili Mungu anamuamuru Nabii Eliya aende Serepta akae huko.Wakati huo nchi ile haikuwa na umande wala mvua kwa miaka mingi, njaa na kiu ya maji vikatawala. Ndipo Neno la BWANA likamjia (Eliya) kusema, ondoka uende Serepta, ulio mji wa Sidoni ukae huko.Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe. Mafundisho yaliyomo kwenye Neno hili ni mengi lakini leo tutafakari jinsi Mungu anavyo walinda na kuwatunza wenye haki wake.Tuanze kwa kuangalia watu wenye haki ni watu wa namna gani?na wanapataje haki hiyo.Warumi 3:21-26“Lakini sasa haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria, inashuhudiwa na torati na manabii,ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti kwa sababu wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wamehesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa, apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu”. Neno hili linatufundisha kuwa haki ni ya Mungu mwenyewe na kwa neema yake tunahesabiwa haki kwa iman katika Yesu Kristo ikiwa tutamwamini yeye kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yetu .Warumi 1:17“Kwa kutii kwa Bwana wetu Yesu Kristo watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki, ili kwamba, kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya haki neema itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu. 2 Wakorintho 5: 21 “ Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye”. Mtume Paulo katika Wafilipi 3:9 anasema,“tena nionekana katika yeye nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani”. Neno la Mungu katika Waraka kwa Waebrania 10:38-39 linatufundisha kuwa, mwenye haki wangu ataishi kwa imani, naye akisita sita roho yangu haina furaha naye. Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.
Baada ya kujua kuwa wenye haki ni watu wa namna gani, sasa tuangalie jinsi Mungu anavyowalinda na kuwatunza wenye haki. Katika mfano wa Eliya, Neno la BWANA likamjia kusema; Ondoka hapa, geuka uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani. Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko (1Wafalme 17:2-4) Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito. Kile kijito kilipokauka, Mungu akamwandaa mjane wa Sarepta amlishe na kumnywesha Eliya. Hebu tuangalie katika nyakati hizi Mungu anatulinda na kututunza kwa jinsi gani?
Neno la Mungu linayo mifano mingi ya jinsi Mungu anavyowalinda watu wake.Waraka kwa Waebrania 11:32-34 “Nami niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gidion na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii, ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba; walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni”. “Mwimba Zaburi ya 91 anasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini kwa kuwa atakuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote. Malaika wa BWANA hufanya kituo, akiwazungukia wamchao na kuwaokoa. Mungu anawaahidi wenye haki wake kuwa kila silaha itakayofanyika juu yao haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yao katika hukumu ataukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA (Isaya 54:17). Katika kitabu hicho hicho Isaya 43:1-2 asema hivi “Usiogope, maana nimekukomboa, nimekuita kwa jina lako wewe u wangu .Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito haitakugharikisha, uendapo katika moto hutateketea wala mwali wa moto hautakuunguza”.
Zaburi 121:1-8 “Nitayainua macho yangu niitazame milima msaada wangu utatoka wapi? msaada wangu u katika BWANA aliyezifanya mbingu na nchi. Asiuache mguu wako usogezwe, asisinziye akulindaye, naam hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israel BWANA ndiye mlinzi wako, BWANA ni uvuli mkono wako wa kuume. Jua halitakupiga mchana, wala mwezi wakati wa usiku.
BWANA atakulinda na mabaya yote, atakulinda nafsi yako BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, tangu sasa na hata milele”.
Pamoja na ulinzi wote Mungu anaotupa tusisahau kumwomba atusaidie kuzilinda roho zetu. Mithali 4:23 “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo, maana ndiko zitokako chemchem za uzima”. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama, bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho, kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni hali mmejifunga kweli viunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa injili ya amani6. Zaidi ya yote mkitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote (Waefeso 6:12-18). Moyo ni muhimu sana kwa kuwa moyoni mwa mtu hukaa Yesu Kristo na moyo ni makao ya Roho Mtakatifu .
Katika sehemu hii ya mwisho ni vyema tukiangalia ni kwa jinsi gani Mungu anatunza hata hivi leo. Tumeona jinsi alivyomtunza Nabii Eliya, Je, na sisi anatutunzaje? Zaburi 34:9-10 “Mcheni BWANA, enyi watakatifu wake, yaani wamchao hawahitaji kitu. Wanasimba hutindikiwa, huona njaa, bali wamtafutao BWANA hawatahitaji kitu chochote kilicho chema” Mungu wangu atawajazeni kila mnachohitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu ndani ya Kristo Yesu (Wakolosai 4: 19). Ukimcha BWANA, BWANA anakuahidi kuwa hawatakuwepo maskini kwenu kwa kuwa BWANA atakubarikia kweli katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako. Kumbukumbu la Torati 28:1-6 “ Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya dunia, na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako.Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani, utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Litabarkiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga.Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa utokapo”. Mwimba Zaburi ya kwanza anasema mtu mwenye haki atakuwa kama mti uliopandwa kando kando ya vijito vya maji, uzaao matunda yake kwa majira yake, wala jani lake halitanyauka; na kila alitendalo litafanikiwa. BWANA ni mwenye utajiri kwa wote wamwitao. 2 Wakoritho 9: 10-12, “Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu, mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao MUNGU shukrani kwa kazi yetu”. Mungu ashukuriwe kwa sababu ya kipawa chake, Tusichoweza kukisifu kama ipasavyo.
Tumeona ni kwa jinsi gani Mungu anatukirimia mahitaji yetu ya kimwili .Tuangalie sasa jinsi Mungu anavyotutunza kiroho na kutukirimia vipawa vyake. Waraka wa Pili wa Petro 1:3-8 “Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa. Naam, na kwa sababu hiyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema na katika maarifa yenu kiasi na katika wema wenu maarifa na katika kiasi, chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
Mungu anatutunza kiroho kupitia Neno lake takatifu naye anasema hivi katika Wafilipi 4:4-7 “ Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema, furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote .Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lolote, bali katika kila neno kwa kusali na kuomba” pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.
Na imani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu”. Neno la Mungu katika kitabu cha Mathayo Mtakatifu 6:19-21, 25, 32-33 linasema, “Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo na wevi huvunja na kuiba, bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibii, kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwako na moyo wako. Kwa sababu hiyo nawaambieni, msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote .Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake, na hayo yote mtazidishiwa” Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani. Tumtwike yeye fadhaa zetu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yetu, tusifadhaike mioyoni mwetu wala tusiwe na woga. Kwa kuwa tunaye Roho Mtakatifu, ambaye atatufundisha yote na kutukumbusha yote.
“Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya staha, yoyote yaliyosafi yo yote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini hayo (Wakolosai 4:8)”.